Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami kama ilivyo ada nianze na neno la shukurani. Mimi ni Mjumbe kutoka TAMISEMI, kwa hiyo, kwa kiwango kikubwa, haya ambayo tumeyaona yanaakisi yale ambayo tulishiriki katika Kamati. Kwa hiyo, mchango wangu nitajielekeza katika maeneo machache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema naanza na shukurani. Awali ni kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia naomba kwa namna ya pekee, najua tunaye Waziri wetu na Manaibu Waziri; mkononi mwangu hapa ninayo barua ambayo Mheshimiwa Waziri ametupatia Wabunge wote ikiieleza taarifa za fedha za miradi ya maendeleo na matumizi mengineo kwa kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023. Mheshimiwa Waziri, jambo hili ni jema. Kwetu sisi, hiki ni kitendea kazi. Mimi mtu wa Mpanda Manispaa, kwa taarifa hii ya fedha ambayo umetuelekeza Wabunge, ikawe kitendea kazi. Takribani Shilingi bilioni 5.9 ikilenga maeneo mbalimbali. Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba, Wabunge tunafahamu, nami shukurani hizi nilizozitoa kwako naomba pia nizipeleke wa Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri, Mameya na Madiwani. Kwa sababu gani? Mabilioni haya peke yetu hatuwezi, ni lazima iwe kwa kupitia ushirikiano.

MBUNGE FULANI: Ndiyo!

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Kwa hiyo, ndiyo maana wapo Madiwani, wapo Wenyeviti, wapo Mameya, na kwa pamoja tunalisukuma hili gurudumu. Kwa hiyo, naomba huko Madiwani huko waliko, wapokee shukurani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nijikite katika eneo la TARURA, najua kweli wanafanya kazi nzuri na siku zote hapa tumekuwa tukawasifia, bila kumsahau Engineer Seif. Nami nimesemaje? Siku zote yule ndugu yetu ni mtu rahimu. Ukimsifia mtu, unamtia moyo kwamba siku nyingine anajipanga vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, najua kwa maana eneo letu la Katavi, Manispaa ya Mpanda, Mheshimiwa Waziri kipindi hiki cha mvua yapo maeneo katika nchi hii hayana mvua za kutosha. Sisi tumebahatika kupata mvua za kutosha. Sasa neema ile ya mvua imepelekea uharibifu mkubwa wa miundombinu. Nikiomba fedha Mheshimiwa kupitia TARURA lengo langu ni nini? Mazao mazuri yaliyozalishwa Katavi yaweze kukufikieni nyie ambao hamkubahatika kupata mvua. Kwa hiyo, nikiomba fedha, tafsiri yangu ni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwa maana ya matengenezo, tumetengewa Shilingi bilioni 1.1, ndiyo maana tulikuwa tunaomba watu wa TARURA waongezewe fedha. Kwa jinsi mvua ilivyoharibu miundombinu, ukija kwangu utanionea huruma. Nimesema wale watu wemelima vizuri, tunatamani mazao yatoke kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dada yangu Mheshimiwa Lupembe, yeye amebahatika kupata boost, wametengenea barabara ya lami mpaka kuisogeza kwenye mpaka na Manispaa. Nimeletewa kuchonganishwa na wananchi kule, wanasema, angalia mwenzake wa vijijini kapata lami, yeye wa mjini hana lami. Kwa hiyo, Waziri nafikiri ukilisikia hili, na wananchi kule wananisikia, kwamba jamani, mimi niliwasemeeni Bungeni. Ni kilometa chache tu Mheshimiwa Waziri. Ni kilometa kama nane hivi. Lengo ni nini? Lami nzuri iliyotengenezwa kule, isipounganika kuja mjini, inapoteza tafsiri. Jambo hilo nafikiri unaweza ukaliona na ukaona namna ya kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni MSD. Tumezunguka maeneo mbalimbali katika nchi hii, ni kweli najua nao wana changamoto kama Serikali, lakini naomba, kwa kuwa kuna fedha nyingi zimepelekwa huko, mimi tu kwa upande wa Katavi kuna zaidi ya shilingi bilioni tano kwa maana ya vifaa. Wanajitahidi kwa kiwango chake, lakini wafanye zaidi, kwa sababu kuna fedha imewekezwa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni upungufu wa watumishi. Nina upungufu wa watumishi 969 katika maeneo yafuatayo: Walimu wa shule ya msingi 265, sekondari 148, watumishi afya 405, huo ni upungufu wa watumishi katika eneo letu la Katavi. Najua Serikali imefanya kazi nzuri kwa maana ya miundombinu, tumejengewa madarasa, vituo vya afya, lakini bila uwepo wa watumishi, kazi inakuwa ni ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna suala la upembuzi yakinifu kuhusiana na suala la miradi, Naomba sana wataalamu wetu, tumepita pale Mwanza tukaliona hilo, kama suala la upembuzi yakinifu ni jambo la kuanza nalo, nashangaa pale ambapo kazi imeshakwenda, inafika mwisho, mtu anawarudisha nyuma akisema kuna gharama moja, mbili, tatu. Hili jambo linatuchelewesha kama Serikali. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana katika eneo hilo tena Serikali ijitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa maana ya SEQUIP; najua kuna Shilingi milioni 470. Kama walivyozungumza wazungumzaji wengine, naomba kwa maana ya thamani halisi ya fedha, Mheshimiwa Wizara yako iliangalie hili kwa jicho la pekee, ni kweli haiwezekani ikawa sare nchi zima, uwiano nchi nzima, na najua hilo kama Kamati tumelijadili na tukaomba mwangalie watu na jiografia za maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu anaweza akawa anapata mchanga sehemu ya karibu lakini akakosa cement. Kuna mtu anaweza akapata kokoto, lakini akakosa mchanga, hivyo; mabati na vitu vingine kwa upande wa vifaa hivyo vya ujenzi. Kwa hiyo hilo nalo ilikuwa ni vizuri tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo la Watendaji wa Kata, Vijiji kupata mafunzo kutoka Chuo cha Utumishi. Ni kwanini tunasema hili? Tunazungumzia Chuo cha Utumishi kwa sababu ndilo eneo ambalo watendaji wetu wanaweza wakapata ladha ya utumishi bora. Eneo la utumishi wa umma ni maeneo ambayo wanawaandaa watu wetu wajue Serikali inataka nini? Kwa hiyo, tukikuomba Mheshimiwa Waziri kwamba watu wetu hawa wapelekwe kwenye Chuo cha Utumishi wa Umma, tafsiri yake ni hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali, mpaka mwananchi akakukute wewe huko Wizarani, anaanza kucheza na Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji. Kwa hiyo, kule ndiko ambako taswira sahihi ya Serikali inajionesha. Kwa hiyo, tukiwa na mtu ambaye amefanya kazi vizuri katika ngazi ile, anamsaidia Mheshimiwa Rais, anakusaidia wewe na nchi inakuwa na ustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CSR, kama ilivyozungumzwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya muda, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)