Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia Hotuba nzuri ya Wizara ya TAMISEMI na niweze kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze kwa ujumla Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri wanazozifanya. Pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, bado tuna changamoto nyingi. Nitachangia maeneo matatu lakini naomba nianze na TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana TARURA kwa kazi nzuri zinazofanywa na sisi wananchi tunaotoka mikoa ambayo maeneo mengi ni vijijini hasa Mkoa wa Tabora maeneo mengi ni vijijini tunatumia sana barabara za vumbi ambazo TARURA zinafanya kazi. Pamoja na kazi nzuri zinazofanywa lakini bado tuna changamoto kwenye maeneo ya majimbo yetu na wilaya zetu. Kwa mfano; naweza nikatoa mfano wa maeneo ambayo bado yana changamoto ili Serikali iweze kuchukulia hatua katika bajeti hii ambayo tunaenda kuipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Jimbo la Igalula Wilaya ya Uyui. Jimbo hili ni jimbo ambalo limekaa vibaya sana, yaani wilaya imekaa vibaya lakini vile vile bado kuna changamoto katika Kata ya Loya kuna daraja ambalo Mheshimiwa Rais mwaka jana 2022 alitoa ahadi pale lakini nashukuru Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Jenista jana amesemea yeye anahusika sana na ahadi za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuomba Mheshimiwa Waziri ulichukue hili. Wananchi wa Loya wanateseka ni kama wapo kisiwani kwa sababu daraja kipindi hiki cha masika na ardhi ile inashika maji kwa muda mrefu na bahati nzuri kwa Mkoa wetu wa Tabora mvua zinanyesha sana mpaka hivi sasa mvua ni nyingi na kuja kukauka inaweza maji yakaanza kupungua kuanzia mwezi wa nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa shughuli zao za uchumi ni mpunga. Sasa ule mpunga ambao wameuivisha kuanzia miezi hii ya mavuno watautoaje kule kwenda kupeleka kwenye maeneo ya kufanyia masoko? Kwa sababu daraja linakuwa limekatika watu wako visiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna kijiji ambacho kiko kwenye hiyo hiyo kata…

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ndiyo, taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE.VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri ambao anaendelea kuutoa dada yangu hapa amezigusia katika Jimbo la Igalula. Ni kweli Mheshimiwa Rais alifika tarehe 17 mwezi wa tano na akatoa maelekezo Wizara ya Ujenzi ianze kujenga Daraja la Loya. Nataka nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Rais ahadi hiyo imeanza kutekelezeka lakini walianza kufanya mchakato, mchakato huo kwa sasa umesimama. Niiombe Serikali waendelee kusukuma kwa sababu maafa yanaendelea.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jacqueline Kainja unapokea taarifa ya Mheshimiwa Venant Protas?

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipokee, naomba niendelee. Katika hiyo kata imebahatika kuwa na kituo cha afya lakini kuna kijiji ambacho kinaitwa Mama Bona. Kutoka kwenda kupata huduma za afya na za maendeleo ya jamii kwa ajili ya kijiji chao ni changamoto. Hawana mahusiano kwa sababu pale kuna mto ambao kuuvuka tumeshapata hasara ya wananchi ambao wameshafariki katika mto ule. Kwa hiyo, nilikuwa naiomba Serikali iweke nguvu ya kuhakikisha daraja lile linatengenezwa na kata ile ina wananchi wengi karibia 38,000. Kwa hiyo, tukihakikisha daraja hilo linatengenezwa bajeti hii ipeleke nguvu katika lile daraja la Kata hiyo Loya katika Jimbo la Igalula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado jimbo hilo hilo ambayo Jografia yake ni mbaya kuna kata ambazo kufikika kwake ni lazima mwananchi akiwa Tabora mjini mkoani kurudi kwenye makazi yake ni lazima apite Nzega – Ndala ndiyo aende kwenye lile eneo. Inakuwa ni mzunguko mrefu sana. Wakati kuna barabara ambayo ingemuwezesha kutoka Tabora mjini kuingia jimboni kwake wilayani kwake kwenye kilometa 89 ikitengenezwa kwa kiwango cha changarawe wananchi wale wataweza kufaidika katika suala zima la uzalishaji wa uchumi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie kwenye suala zima la huduma za afya. Tunaendelea kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri zinazofanya hasa kuhakikisha wanatuwekea majengo ya vituo vya afya ikiwepo zahanati. Lakini vituo vya afya hivi ambavyo ni Sera ya Afya inayosema zahanati kwa kila kijiji, vituo vya afya kwa kila kata. Bado tuna changamoto nyingi ya vifaatiba ambayo Wabunge wengi kila tukisimama hapa tunaongelea suala la vifaatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano naweza nikatoa kwa Mkoa wangu, bado tuna changamoto hiyo unakuta mfano Wilaya ya Igunga tumepata vituo vya kutolea huduma nane. Katika nane, viwili ni vituo vya afya na sita ni zahanati, bado tuna changamoto ya vifaatiba na wahudumu wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumejenga yale majengo lakini bado hatujawatendea haki hawa wananchi. Nilikuwa naomba niishauri Serikali, tunapoendelea kukamilisha hii sera ya zahanati kila kijiji na vituo vya afya kwa kila kata, hebu tu-focus zaidi kwenye quality wakati tunaenda kuendelea kumaliza quantity kwa maana ya kwamba unakuta kuna vijiji vimepangana na jiografia yake viko mashariki pamoja; vijiji kama vinne, vitano vina zahanati kila kijiji lakini zahanati hizo tano mgonjwa anapoenda anaambulia kupata paracetamol na ataambulia kupata labda Alu lakini vipimo hapati kwa sababu vifaatiba hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu tupunguze badala ya kujenga vituo vyote vile vitano ambavyo vimejipanga kwa upande wa mashariki ikiwa magharibi hakuna hata kituo kimoja, vile vitano ile nguvu tukamilishe kwanza kimoja tu-deal kwenye quality service ambayo mtu akienda pale atapata huduma moja kwa moja kuliko mtu anaenda pale huduma hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuanenda kwenye suala la watumishi. Naipongeza Serikali imetoa watumishi 21,200. Bado ni wachache sana lakini niombe kwa Mkoa wetu wa Tabora ambao bado ni mkubwa, tunaomba watumishi tupate idadi ya kutosha. Kwa mfano, mahitaji yetu kwa sasa hivi tunaohitaji ni watumishi 6,299 lakini mapungufu tuliyonayo ni watumishi 3,860 sawa na 61% na waliopo ni 2,439 sawa na 39%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali katika bajeti hii ya watumishi idadi hii ya watumishi basi kwa Tabora tufanye vice versa ile 39% ndiyo yawe mapungufu na 61% iwe ndiyo mahitaji ambayo tutakuwa nayo, niombe Serikali izingatie hilo. Lakini pia katika hizi ajira muangalie namna nzuri ya kutoa ajira, tupunguze ile michongo. Kila maeneo yapate hizo ajira, ajira zinaenda kwa michongo sana. Watu wasiokuwa na mabavu hawapati ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnakuja na suala la kusema tunaangalia intake labda ya 2019,2018,2020 lakini utakuta kuna watu wame-apply wenye hivyo vigezo vya intake ya 2019 halafu anaajiriwa mtu wa intake ya 2022 ambaye amefanyiwa mchongo, inakatisha tamaa kwa vijana ambao tumewaomba wajiajiri. Serikali tunaomba mfuate vigezo na masharti ambavyo mmejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)