Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Gairo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mmoja wa wachangiaji kwenye Wizara yetu ya TAMISEMI. Mimi leo nitachangia vitu vichache tu; lakini kwanza kabla sijachangia naunga mkono hoja ya TAMISEMI. Si kwamba naunga mkono hoja ya TAMISEMI kwamba wanafanya vizuri, hapana isipokuwa naona wageni. Kwa hiyo kwa hili safari hii tunaunga mkono hoja kwa sababu tunajua kuna dada yetu Kairuki, kuna akina Deo na mwenzetu Dugange huwa ni wazuri wanapokea simu zetu wa Wabunge. Kwa hiyo na mkiona makofi haya msivimbe kichwa halafu muache kupokea tena. Kwa hiyo tunaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ila tunaka kusema, kwamba mmekabidhiwa gari bovu, ambapo hili gari ni la tani 30 lakini lina injini ya bodaboda, huo ndio ukweli, tusitake kila kitu tunasifu. Kwa hiyo dada yangu hapa pana kazi ya ziada na pana kazi ya ziada kuanzia kwako TAMISEMI kwa watumishi wa TAMISEMI. Nimeona Wabunge hapa waliochangia, hawa wawili kabla yangu nimeona wamezungumza kwa uchungu hata yale niliyotaka kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mgao wa watumishi hasa walimu, watumishi wa hospitali ukiangalia mara nyingi ukiona jimbo la Waziri utaona lina mgao mkubwa, jimbo la Mbunge lina mgao mdogo. Hiki kitu kiko wazi; na juzi niliongea na wewe na ndiyo maana leo nimekuwa mpole, na nilikuonesha mfano nikakutajia mahali fulani, na mimi huwa naongea kitu kwa uchunguzi. Utakuta, kwa mfano vituo vya afya; sisi Gairo kuna Kata ya Chanjare, iko umbali wa kilometa 90 mpaka kufika Gairo Mjini. Tumeomba kituo cha afya, Naibu wako hapo Dkt. Dugange hapo anafahamu, amenisaidia sana, lakini kile kituo hakijapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikamwonesha sehemu vituo vya afya vimejengwa kuna watu hata 2,000 hawafiki kuna kituo cha afya. Mwenyekiti wako wa Kamati, Mheshimiwa Londo anajua. Sasa, hivi kweli, mama,Mheshimiwa Rais, anatoa vituo vya afya kwa ajili ya kusaidia wananchi wake; hivi vituo mvifanye viwe vya mkakati. Muangalie, si lazima iwe kila kata inapata kituo cha afya lakini at least muangalie kwamba hapa pana kata labda tatu kimkakati kwamba wapi tuweke kituo cha afya ambapo watu wana shida. Sasa ninyi wenyewe kwa wenyewe huko mnagawana tu vituo. Waheshimiwa Wabunge nachosema ni kweli, wengine tumepata kimoja, viwili lakini kuna watu wamepata vinne, kumi, sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naombeni sana jamani, dada yangu naomba sana uwe makini na hilo. Kama Kata yetu ya Chanjari sisi ni lazima tupate kituo cha afya hata kama havimo kwenye mpango mkakati, mkatafute hela mtuletee kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye watumishi walimu hivyo hivyo ukiona mtu anapelekwa Sumbawanga, anapelekwa wapi, ujue anapelekwa tayari hapo TAMISEMI wameshamwajiri halafu wao ndio wanaandika vimemo huyo mpe uhamisho, msaidie arudi huku. Utakuja kukuta ile wilaya imepelekewa walimu 50 baadaye unakuja kukuta ina walimu 24, wale wote wametoka. Safari hii kwenye mgao huu mimi kwenye shule za msingi nina uhaba wa walimu takriban 800, huwezi ukaja ukanipa walimu 100 ukaniambia eti tunapunguza polepole wakati mijini wamejaa huko, wachumba, wote mmewaweka kwenye miji huko, hii haitowezekana. Mtupe, na muhakikishe kabisa wakija hawatoki sio mnawaleta halafu mnaandika vimemo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninavyo vimemo nitakuletea apewe mkurugenzi huyo. Fanyeni uchunguzi huko mnakosema kwamba walimu wanahamishwa, wanahamishwa kutoka TAMISEMI. Wale mabosi huko wanaandika tu vimemo basi wanaondoka. Kwa hiyo wanajiajiri kwa undugu halafu wanawatoa ndugu zao wanawapeleka sehemu nzuri hawataki wakae vijijini.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamelalamika sana hapa kuhusu habari ya wale walimu wanaojitolea…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby subiri kidogo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge wa Nyang’hwale.
T A A R I F A
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nimpe taarifa mchangiaji, ameizungumzia ile Kata ya Chanjale. Mimi nimefanya ziara kutembelea maeneo yale, ukweli kuna shida kubwa na mimi namuunga mkono namwongezea Mheshimiwa Waziri alifikirie hilo la kuweka Kituo cha Afya Chanjale. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shabiby unapokea taarifa.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndiyo nilikuwa nahitaji hii, nimeipokea. Ni ukweli na ndiyo maana saa nyingine hata mnasema kwamba aah! kuna chuki kati ya Wabunge hivyo inakuwaje kama ukienda sehemu zingine uko utakuta kuna kituo cha afya cha ghorofa halafu kwako cha mabati ya kienyeji, utampendaje hapo? Kwa hiyo kwenye ajira hizi ajira ya afya hivyo hivyo; sehemu kama Gairo tuna upungufu wa watu karibia 200 na kitu, lakini ukiangalia hawaji. Safari hii kwa kweli tunao, na kama vipi tuje tuazimie humu Wabunge, tuazimia hapa watu wafukuzwe kazi na Spika naye kama hataki naye tunamuazimia sisi si ndio tuliomchagua? Ndiyo maana yake. Sasa sisi hapa bosi wetu ni Spika na Rais, kwa hiyo kama tunaye humu watu wanatufanyia vituko huko majimboni tuna kazi ya kulalamikalalamika humu tunajifichaficha, haiwezekani kitu kama hicho. Tuje tuazimie tu Spika alete hapa, TAMISEMI pale huyu, huyu, huyu hatakiwi sisi ndio tunasimamia Serikali na Spika naye akituletea siasa zake tunamwambia naye kaa pembeni na wewe tunakuazimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwenye vituo vya afya na walimu tunaomba kabisa wafanyakazi hao tuwapate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA kwa kweli inafanya kazi nzuri sana lazima tuseme ukweli. Hata Mkurugenzi wa TARURA huyu CEO wao ni mtu mzuri sana, lazima tuseme ukweli, pale wanapofanya watu ukweli huwa tunasema vitu vya ukweli. Mama Rais wetu ametupa ile mia mia za barabara, kweli tunaona zinafanya kazi, lakini bado hazitoshi na sijaona watu wanatafuta hata ile vyanzo huko Serikalini hawatafuti vyanzo. TARURA lazima itafute vyanzo siyo lazima iwe mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna service levy, hivyo ukiichukua service levy ile ni kodi ya nini? Hujui! Unaambiwa kodi ya huduma, ukiangalia mfanyabiashara analipa yeye; kuzoa uchafu, zimamoto, sijui nini, kila kitu analipa halafu kuna service levy, halafu service levy wanakwenda wanajenga majumba, majumba tu eti kitega uchumi, kitega uchumi kipi? Hapa Dodoma wamejengajenga magorofa yale, sasa hivi wanalala panya na watu wawili, watatu, kitega uchumi, kwa nini wasichukue hizi hela za service levy basi angalau iwe na maana ziende TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ndiyo ukweli. Hii service levy Waheshimiwa Wabunge wazifanyie uchunguzi, haya mashirika yote yanayohusika na TAMISEMI angalia hata yale majengo waliyojenga kwa mfano haya ya Shirika la LAPF, si wamejenga majengo, majengo kama ile Millennium Tower na mengine, mwende mkaangalie kama wamerudisha robo ya pesa ya gharama iliyotumika, mimi najiuzulu Bunge hapa. Kila siku baada ya miaka fulani wanatoa bilioni nne au tano ukarabati, wakati hata bilioni mbili halijaleta yaani kuna pesa, Mheshimiwa Waziri, Dada yetu uwe makini. Halafu kuna vitu vingine...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa unga mkono hoja, kengele ya pili imegonga.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya kwanza.
MWENYEKITI: Haya tunaendelea na uchangiaji hii ni kengele ya pili kiti ndivyo kinavyoelekeza Mheshimiwa Shabiby.
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Spika, haya ahsante. Naunga mkono hoja.