Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kufungua dimba katika uchangiaji wa bajeti ya Ofisi ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kimsingi ndiye Waziri kwenye Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya na kazi hii anaifanya. Nimewahi kusoma maandiko matakatifu kutoka kwenye vitabu vyetu vitukufu kwamba Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Wasalaam alifundishwa biashara na Bi Hadija ambaye ndiye alikuwa mke wake. Huyu ndiye aliyemfundisha bihashara pamoja na Utume wake lakini biashara hiyo alifundishwa na mwanamke.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna Bibi mmoja anaitwa Elizabeth ambaye ni Mama yake Yohana mbatizaji ndiye aliyegundua kwamba Bi. Mariamu, Mama yake Yesu ana ujauzito. Kwa hiyo utagundua kwamba mwanamke kwa nafasi hii ambayo tumemkabidhi Rais majukumu haya hatukumkabidhi kwa bahati mbaya ni kiumbe ambaye amebarikiwa kutoka kwa uumbaji wa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, theories mbalimbali, wanazuoni wengi wanatanabaisha kwamba kitovu cha matumizi sahihi ya rasilimali ni rasilimali watu. Rasilimali watu katika nchi yetu tumeikasimisha katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inafanyika kazi nzuri sana na tunawapongeza sana. Sera zote za Utumishi wa Umma, Sheria lakini miongozo mbalimbali yote inasimamiwa na Ofisi hii ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika haya mambo yaweze kufanyika na kukamilika ni lazima kuhakikisha kwamba wakati wote haki za watumishi zinasimamiwa ipasavyo na hili Mheshimiwa Rais ameonyesha kwa vitendo haswa baada ya kuwapandisha madaraja watumishi wote kwa wakati, lakini kulipa malimbikizo yote ya pesa ambazo watumishi wa umma walikuwa wanadai. Hali kadhalika amebadilisha kada ya utumishi na hili amelifanya kwa kutoa Muongozo wa kupandisha madaraja kwa watumishi wapya ambao wapande madaraja kwa miaka minne na wale watumishi wa muda mrefu kwa miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatakiwa ifanye kazi katika maeneo kadhaa ambayo ningeomba kutoa ushauri. Eneo la kwanza ni maadili, katika idara zote zinazosimamia maadili ya utumishi wa umma ni vizuri sana zikazingatia misingi ya utumishi wa umma. Hapa nitatoa mfano kwamba, sisi tunapokea Ripoti ya CAG ambayo Bunge linaipokea na linajadili. Ningependa kuona na Sekretarieti hii ya Maadili ya Viongozi wa Umma na yenyewe ianze kufanya hivyo kupitia ile Tume ya Utumishi kwamba Tume ya Utumishi inaleta ripoti ndani ya Bunge, lakini kwa bahati mbaya sana ripoti ile hatuijadili.

Mheshimiwa Naibu Spika kwa hiyo ningependa kushauri kwamba ifike mahali sasa angalau na Tume ile ya Utumishi ikileta ripoti ndani ya Bunge, tuifanyie mjadala ili tuweze kuona ufanisi uko kwa kiwango gani katika maeneo yote ya utumishi wa umma? Tunaweza tukagundua upungufu katika utendaji, lakini pia kuangalia haki za watumishi na msawazo wa ujumla wa utumishi katika nyanja mbalimbali za utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna mfumo ule wa Upimaji Utendaji Kazi kwa Watumishi (OPRAS) mfumo ule una changamoto. Sasa ni vizuri wakaja na mfumo bora zaidi ambao utakuwa unapima quantity na quality. Tunaweza tukasema ubora lakini pia na wingi wa kazi ambazo mtumishi mmoja anafanya na hapa tuwashirikishe vizuri watu wa e– government. Hii mifumo tunaizungumza tu, lakini ukienda kwenye uhalisia huoni namna inavyofanya kazi na ndiyo maana wakati mwingine inazua maswali mengi hata kutoka kupoteza imani hasa linapokuja suala la ajira. Kwa hiyo niombe sana kwamba tutumie e–government kuhakikisha kwamba tunaboresha mifumo iweze kusomana vizuri, tuwe na kanzidata ambayo inaweza ikajua mfanyakazi mmoja anafanya kazi kwa kiasi na mwingine anafanya kazi kwa kiasi gani. Pia na usambazaji mzima wa hao watumishi katika halmashauri zetu, katika idara na katika mashirika kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo lingine ambalo ningetaka nishauri na hili ni jambo ambalo kwa kweli kama Taifa inabidi tuliangalie kwa umakini mkubwa sana, suala zima la ajira. Nitatoa tu mfano katika kada moja ya elimu, kama kuna mahali tumekosea ni pale tulipoua Tume ya Mipango. Tume ile ya Mipango ndiyo ilikuwa inaweza kupanga mipango yetu ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Tumeiunganisha Tume ya Mipango kwenye Wizara ya Fedha, sasa hivi ufanisi wake huuoni na huko mbele ya safari tutakwenda kukumbana na tatizo ambalo ndiyo hili naomba niliseme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye kada moja tu ya elimu; tunavyo Vyuo 35 vya Elimu hivi ni katika ngazi hii ya diploma na certificate ambavyo ni vya Serikali. Kila chuo kinadahili wanafunzi 400 kwa mwaka, kwa maana kwa vyuo 35, tunapata wanafunzi 14,000 wanadahiliwa kwenye ualimu kwa mwaka mmoja. Ukichukua na wanafunzi walioko kwenye vyuo binafsi vya elimu viko 23, hivi vinachukua wastani wa wanafunzi 11,000, ukichanganya unapata ni wanafunzi wastani wa 25,000 wanadahiliwa kila mwaka. Kwa hiyo kwa vyuo hivi vinavyochukua wanafunzi kwa miaka mitatu maana yake una wanafunzi 75,000 wanadahili sasa hivi wako kwenye vyuo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Vyuo Vikuu UDOM, St Augustine pamoja na University of Dar es Salaam, DUCE na vinginevyo vina wanafunzi, mpaka sasa hivi ninavyozungumza hapa 56,183. Jumla yake ni wanafunzi 131,183 hawa wanadahiliwa, wanaandaliwa kwa ajili ya soko la elimu. Soko lenyewe halipo, ajira zilizotoka ni 21,000 elimu na afya ambazo ni wastani wa kwenye elimu ni 12,000, hawa wanafunzi tutawapeleka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri, hapa sasa ndiyo tunakuja kwenye Tume ya Mipango lakini pia eneo la utawala bora. Kuna umuhimu gani kuendelea kuzalisha walimu kama kwenye soko hatuwahitaji? Ifikie mahali tupunguze utitiri vya vyuo hivi vinavyotoa kada za elimu kama hatuna nafasi ya kweza kuajiri ili watoto wetu wasome masomo ambayo watakapokwenda kwenye soko wanaweza wakayafanyia kazi na ualimu kwasababu ni ambalo ni mahususi maana yake akishasoma hawezi akafanya kazi nje ya eneo hilo. Kwa hiyo niombe sana jambo hili tulifanyie kazi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, inakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)