Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia nafasi kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Nina hoja kadhaa, kama nne hivi, lakini nitaenda kuzichangia kwa kadiri nitakavyoweza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa lolote lile ili liweze kuendelea lazima liwe na usimamizi madhubuti wa rasilimali watu kuhakikisha kwamba wanatenda kazi kwa ufanisi ili kuweza kuleta tija. Hata Waziri wakati anawasilisha hapa ameonesha bayana kwamba, tukiwa na rasilimali watu za kutosha basi uchumi wa nchi yetu utasonga kwenda kwenye uchumi wa kati. Tumekuwa kama Taifa kwa kweli, tukishuhudia wimbi kubwa la upungufu wa rasilimali watu. Maana tusipokuwa na rasilimali watu wa kutosha wenye uwezo, wenye weledi na waadilifu, tutaendelea kushuhudia utolewaji hafifu wa huduma za kijamii, ubadhirifu wa fedha za umma na mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ndiyo wana mamlaka yote ya kutoa vibali na kuhakikisha kwamba Watanzania wenye sifa wanaajiriwa, ili kuwepo na ufanisi kwenye taasisi zetu. Nitaenda kuainisha upungufu uliopo hasa kwenye sekta ya afya, sekta ya elimu na Serikali kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa rasilimali watu kwenye sekta ya afya ni mkubwa sana. Watanzania sasa hivi tupo milioni 61,700,000 na kitu kwa mujibu wa sensa ambayo imepita. Tuna upungufu wa zaidi ya wafanyakazi 82,000 kwenye sekta ya afya. Nilikuwa napitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, page 134. Inasema: “Kuongezeka kwa watumishi wa sekta ya afya kutoka 86,000 mwaka 2015 kufikia 100,000 mwaka 2020”, ambapo tumeongeza watumishi 18,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani kwa miaka mitano, kama Taifa, na upungufu tulionao kabisa mmeona it is a statement kuweka kwenye Ilani ya Uchaguzi kwamba mmeweza kuajiri watu 18,000! Kwa maana nyingine, tangu tupate Uhuru mnaandika mmeajiri watu 100,000 kwenye sekta ya afya. Kweli! Tuko milioni 61, if you take the ratio hapo, ina maana mtumishi wa afya bila kujali category aliyonayo, anatakiwa kuhudumia Watanzania 600,000. Are we serious? Halafu tutegemee tuwe na Watanzania ambao watahudumiwa wawe na afya njema, wafanye kazi ya utendaji kwenye uchumi wa nchi na kuweza kuchechemua uchumi wa nchi yetu? You are not serious. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naona kwa sababu hata Wizara zikija hapa zinasema, kuweza kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, wanakuwa wamewekwa kwenye comfort zone. Sasa ukiwekewa kwamba uajiri watu 18,000, au 20,000 au 30,000 kwa miaka mitano, tayari wamekuwa kwenye comfort zone. Ndiyo maana hata wakiomba vibali vya kuajiri uta-relax tu, Ukiangalia ilani yenyewe imekupa idadi ndogo ya watu. Hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye sekta ya elimu, ndiyo kabisa. Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2021/2022, mpaka 2025/2026 umesema kabisa kwenye sekta ya elimu, shule za msingi…

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumpa Taarifa mwongeaji. Kwanza nampongeza kwa kuisoma Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Tumegundua kwamba anaisoma na anaielewa vizuri. Nimwambie tu, tulishaajiri 7,000, na sasa hivi tumetangaza 21. Kwa hiyo, tumeshaipita ilani na tunaendelea kuajiri. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Matiko, taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Nicheke kidogo. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokuwa naapa hapa, napewa Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama nyenzo kuhakikisha Serikali iliyopo madarakani na chama ambacho kimepewa madaraka na wananchi wanatekeleza na kuleta maendeleo kwa Watanzania. Sasa dada yangu Munde uwe unasoma kwa kina, unachukua na figure nyingine unalinganisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia upungufu wa wafanyakazi kwenye sekta ya afya na elimu, ni zaidi ya 223,000. Mnazungumzia kuajiri 7,000, umeajiri 20,000, kweli! Tutachukua miaka mingapi kuweza kuajiri hao wote wakati watu wanakua? Yaani leo miaka 62 ya Uhuru, mme- document hapa, watu 100,000. Ungetakiwa tu ukae chini. Ngoja niendelee. (Makofi/Makofi)

MBUNGE FULANI: Ehe.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema kwa elimu, shule ya msingi, ratio ni mwalimu mmoja wanafunzi 50; Mpango wa Tatu wa Maendeleo. Kwa sekondari ratio ni mwalimu mmoja afundishe wanafunzi walau 20. Ukiangalia jinsi wanavyotoa ajira hizi, na ambapo nashukuru kwenye elimu sasa hivi, maana nimepitia hapa, ile miaka mitano hamkuajiri kabisa kwenye sekta ya elimu. Sasa hivi walau wametangaza 21,200 na 13 kwenye elimu, lakini bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia upungufu tulionao kwenye sekta ya elimu ambao ni 223,000, ukiangalia na uwiano, ina maana unazungumzia shule ya msingi, on average ni kwamba mwalimu mmoja kwa wanafunzi 120, na kuna nyingine mpaka 200 au 300. Maana unakuta shule ina wanafunzi 1,000 au 2,000 lakini walimu watatu au wanne. Sasa ukiangalia hiyo ratio ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 400. Tutafika kweli! Yaani leo tutegemee wanafunzi wa shule za umma wafaulu kama za binafsi! We will be joking. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani leo utegemee mwanafunzi wa shule ya umma afaulu! Anapewa mtihani wa kujipima sawa na anaopewa Nicole wangu? Never on earth. Hatuwatendei haki Watanzania hawa. Tujitoe, tuajiri kama Taifa, kama ambavyo tunatoa matrilioni kujenga barabara na mambo mengine, tuwekeze kwenye rasilimali watu. Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo iko nyuma, inaenda sijui sayansi ipi ya kutothamini rasilimali watu? (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, muda wangu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Matiko ukae. Taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nadhani Mheshimiwa Mbunge anaposimama angepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ambazo zimejionesha katika kushughulikia tatizo la rasilimali watu nchini. Ninachotaka kumwambia ni kwamba, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ni utekelezaji wa miaka mitano, hapa tulipofika ni kama tunaelekea tu nusu ya safari. Hata hivyo, ameona juhudi nyingine tofauti tofauti za kuhakikisha kwamba, tatizo la rasilimali watu nchini linatatuliwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kufanya tafiti na kuangalia uwiano mzima wa watumishi tulionao ili waweze kutoa…. (Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Hebu, upande huu kaeni kimya. Upande huu kaeni kimya.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Kwa hiyo, mnakataa maamuzi ya Kiti!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Kwa hiyo, unakataa maamuzi ya Kiti Mheshimiwa Ester Bulaya! Nikusomee Kanuni ya kupinga maamuzi ya Kiti?

Kaa kimya, kaa kimya. Usilete mambo ya kujua humu ndani, kwanza huna unachokijua.

MHE. ESTER A. BULAYA: (Hapa hakutumia kipaza sauti)

NAIBU SPIKA: Wala usinijibu mimi. Nikikusomea kanuni hapa utatoka na hutarudi tena mpaka miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri endelea.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana commitment ya Serikali yetu kuhakikisha inatatua tatizo la watumishi, imeanzisha mfumo wa Human Resource Assessment, ili kujua ukubwa wa tatizo na kupitia ajira na mikakati mingine tuweze kutatua tatizo hilo. Kwa hiyo, Serikali haijakaa kimya, imefanya juhudi kubwa na itaendelea kutekeleza mipango mbalimbali kutatua tatizo hilo.

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Matiko.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei taarifa yake. Hapa tupo Wabunge tunaishauri Serikali. Mchukue mawazo yetu myafanyie kazi, mweze kuboresha hapo mlipo, maana mnajikongoja, muende kwa kasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Raslimali watu ndio kitu muhimu cha kuchechemua uchumi wa nchi. Mtajenga miundombinu; na hapa kwenye Ripoti ya CAG ameainisha kwamba, amepitia akaona kwenye Halmashauri 16 kuna vituo vya afya, kuna zahanati zimekamilika za Shilingi bilioni 4.93 zimeshindwa kufanya kazi kwa sababu ya upungufu wa Watumishi wa Umma hawapo. Then tuna-advise mnasimama kupoteza muda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, mwaka wa fedha 2021/2022…

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mwenyekiti wa Kamati inayohusika, taarifa.

TAARIFA

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe Taarifa Mheshimiwa mchangiaji kwamba, ni kweli kuna upungufu wa watumishi wa sekta ya afya na elimu, lakini upungufu umeonekana kutokana na kuongezeka kwa ujenzi wa shule za msingi, ujenzi wa vituo vya afya na ujenzi wa zahanati. Ujenzi wa vituo hivi umekwenda kuonesha upungufu wa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasi kama Bunge, ukipitia Taarifa ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, naye Mbunge akiwa mmojawapo, tulipitisha maagizo ya kuiomba Serikali iongeze wafanyakazi na Serikali imetekeleza na hayo yanafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa Taarifa hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Matiko.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunafurahi sana majengo kujengwa, lakini inaonesha mlikuwa hamna mpango. Kwa sababu, ukijenga majengo ni lazima yaende sambamba na kuajiri rasilimali watu. Hatuwezi kujenga majengo tunaacha popo wanakaa, halafu tunakaa tuna-relax hapa wakati hela za umma zinatumika bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuwe na value for money. Mathalani mwaka 2021/2022 tu tuliidhinisha bajeti ya kuajiri watumishi 10,800 kwenye Serikali Kuu. Vibali viliombwa vya watumishi 20,000, lakini vikaidhinishwa 7,000 tu, na bajeti tumepitisha hapa kwa watumishi wote. Kwa hiyo, unaona hawatoi uzito kwenye kuhakikisha kuna rasilimali watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nihame hapo, maana naona viti havitulii.

MBUNGE FULANI: Endelea!

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ukaimishaji wa watumishi wa umma kinyume cha sheria na kanuni ambazo zinasema usizidi miezi sita. Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG, kuna watumishi 258; kwenye taasisi 40 tu walizopitia, wanakaimishwa nafasi kati ya muda wa miezi sita mpaka 108. Yaani unamkaimisha mtu kwa miezi 108, you are saying about nine years, hujamwona kama ana sifa ili umthibitishe awe mfanyakazi kamili, na kama hana sifa umweke pembeni mteue mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi mimi ukinikaimisha kwa miaka tisa, kwanza nakuwa hata siwezi kufanya kazi kwa ufanisi, kwa sababu, sina mamlaka kamili, umenikaimisha tu. Kwanza pia, unanipa majukumu mengi, nina kanafasi kangu kengine huku, na huku umenikaimisha. Miaka tisa unamkaimisha mtu, miaka tisa! Hii siyo sawa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)