Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza katika siku hii ya leo. Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, pia kwa sababu mimi ni mwanamichezo napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza Simba na Yanga kwa ushindi walioupata weekend hii katika michezo yao ya robo fainali na tunawaombea katika mechi zijazo waweze kushinda ili kusudi Taifa letu liweze kuingia katika hatua ya nusu fainali ambayo itakuwa rekodi kwa Taifa letu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaomba nijielekeze kwenye hoja. Mimi nina mambo kama matatu hivi. Kwanza, kumekuwa na jitihada kubwa sana za kuhamasisha upandaji wa miti, ni jambo jema na jambo zuri lakini lazima ifike wakati tujiulize je, kupanda huku kunaendana na utunzaji? Kweli tumeweka malengo ya kupanda nadhani miti 1,000,000 kwa kila Halmashauri, tunapanda vizuri sawa lakini je, miti mingapi inapona? Kwa hiyo pamoja na kupanda tujielekeze pia katika utunzaji wa miti hii ili tusije tu tukawa na takwimu za kwamba tumepanda miti kadhaa lakini miti ambayo inaendelea kuishi na kuwepo kwa nia ya kutunza mazingira inakuwa ni michache. Kwa hiyo, nguvu zielekezwe kwenye kupanda lakini pia na kwenye kutunza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ninalopenda kuchangia ni kwa namna gani kama Taifa tumejipanga kunufaika na Mifuko ya Umoja wa Mataifa ambayo ina jukumu la kusaidia nchi maskini kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru na napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais katika mkutano wa mazingira kule Scotland – Glasgow, alikuwa jasiri na aliyaeleza mataifa makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa yana mchango mkubwa katika kuharibu mazingira na kuchangia madhara haya ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuahidi kuchangia ile mifuko takribani Dola Bilioni Mia Moja ambayo fedha hizi zitasaidia nchi maskini ambazo kimsingi hazichangii sana mabadiliko ya tabianchi, hazichangii sana kuharibika kwa mazingira, sasa hizi nchi kubwa zinao wajibu wa kuzi–support hizi nchi ndogo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais alikuwa jasiri na aliyaambia Mataifa makubwa kwamba pamoja na ahadi zenu ifike wakati muweze kuheshimu ahadi zenu na kutoa hizi fedha. Sasa kama Taifa tumejipangaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza Wizara na Serikali walikuja na huo mwongozo pamoja na kanuni za udhibiti na usimamizi wa biashara ya carbon au hiyo tunaiita hewa ya ukaa. Mifuko hii iko mingi na katika Mkutano wa mwaka jana maarufu kama COP27 kumeanzishwa Mfuko unaitwa Loss and Damage Fund. Mfuko huu malengo yake ni kusaidia katika kutibu majanga mbalimbali ambayo nchi hizi maskini zinapata kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu na hoja yangu kwa Mheshimiwa Waziri na kwa Serikali kwa ujumla, tumejipangaje katika kuhakikisha kwamba tunanufaika na fedha hizo na tunaweza kukabiliana na majanga yanapotokea. Kwa mfano, jambo la muhimu la kwanza sana inatakiwa lazima uwe na orodha ya majanga yanayotokea katika Taifa lako ili mfuko ule utakapoanza kutekelezwa basi walau unapoenda kuwasilisha yale maombi tayari unakuwa na ile orodha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, pamoja na Kanuni hizi, natumia nafasi hii kuwapongeza sana Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania walifadhili Halmashauri ya Mji wa Mafinga tukaenda kujifunza kule Wilaya ya Tanganyika kwa Mheshimiwa Kakoso. Wenzetu wamepiga hatua sana. Nimeona Serikali Mheshimiwa Jafo amesema kufikia 2024 Januari, hakutakuwa na matumizi ya mkaa kwa Taasisi za Umma na Binafsi ambazo zinahudumia watu kuanzia mia moja. Je, kama Taifa tumejipangaje katika kutumia nishati mbadala?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Mafinga tunavyo viwanda vya mkaa ambao unatokana na mabaki yanayotokana na uzalishaji wa mazao ya misitu. Sasa yale mabaki ni kwamba tungeweza kuyachoma kwa kuyachoma maana yake tungeendelea kuharibu mazingira, sasa viwanda kama hivi vilikuwa vitatu,viwili vimeshafungwa, kimoja kinaendelea lakini hata hiki kimoja mkaa kinauza nje ya nchi kwa sababu hapa nchini hawawezi kuuza kwa sababu bei inakuwa ni kubwa kutokana na mazingira yale ya uwekezaji siyo rafiki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alipiga marufuku matumizi ya kamba hizi za nylon, kwamba ili tuweze kufufua zao la mkonge, tuweze kutengeneza ajira lakini kwa ajili hiyo ya kulinda mazingira tupige marufuku uingizaji wa kamba za plastic lakini kamba bado pia zinaingia. Je, tunajipangeje katika haya yote, kwa mfano kuhakikisha kwamba hawa watu wanaozalisha nishati mbadala kama nilivyosema viwanda hivi vya Mafinga, tunaviwekea mazingira gani ili vizalishe ule mkaa ambao kama mtu hana uwezo wa kugharamia gesi basi aweze kuwa na ule mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, watu wa Mufindi, Iringa na Njombe tumepanda miti kwa wingi, niliposoma kanuni sijui kama nimeelewa vizuri na kwa kuwa inawezekana hata mimi Mwakilishi naweza nikawa sijaelewa vizuri, nilikuwa naiomba Wizara iwe na mpango mkakati maalum, waje watuletee elimu na kutuwezesha kufahamu je, hata hii miti ya kupanda nayo tunanufaika katika hii biashara ya hewa ya ukaa?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nashukuru kwa kunipa nafasi na Mungu atubariki wote na awabariki Simba na Yanga katika mechi zijazo. Ahsante sana. (Makofi)