Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuamsha asubuhi hii ya leo tukaweza kuja kujadili bajeti hii muhimu kwa nchi na kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia napenda kupongeza Wizara zote mbili ambazo zinahusika na mambo mawili haya ya Muungano na Mazingira. Nikiendelea, kwanza napenda kuwapongeza wananchi wa Tanzania kwamba, keshokutwa tu tunatimiza miaka 59 ya Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano ambao umeleta sura na nuru ya Taifa letu katika dunia nzima. Ni Muungano wa kupigiwa mfano, tunatakiwa sisi tuliourithi kutoka kwa waliouasisi kuundeleza na kuutunza kwa vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali na vikao mbalimbali vya kutatua changamoto mbalimbali za Muungano zinazojitokeza, napenda kuipongeza Serikali kwa jitihada hizo inazozichukua siku hadi siku. Pia napenda kukubaliana na maoni ya Kamati kwamba mgawanyo wa ajira na uwiano wa watumishi katika sekta za Muungano ufanyiwe kazi na uwe uwiano ule uliopangwa ili kuhakikisha pande zote mbili za Muungano zinanufaika na utumishi huo na ajira hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea, najikita kwenye upande wa mazingira. Napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha nchi yetu inatunza mazingira, tunadhibiti mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla na shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira. Napenda nichangie mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi, naipongeza Serikali kwa kuwekeza miradi ya mazingira mbalimbali kwa upande wa pande zote mbili za Muungano, na upande wa kwetu Zanzibar tumepata miradi ya kujenga tuta, ukuta, kuhifadhi maji chumvi yasiingie. Pia, tumepata mradi wa majiko ambayo yanatumia nishati mbadala ili kuepusha ukataji wa miti na kuni. Vile vile mradi ambao utasaidia wananchi wa Pwani wasipasue mawe ili kujengea kwa kupewa boti kama mbadala wa biashara zao na kujiingizia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto bado ziko, hasa kwa upande wa visiwa. Visiwa vyetu vinaliwa na maji ya bahari na kuna hatari ya kupoteza uhalisia wa visiwa hivi. Tanzania ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo sasa ni Tanzania na ndani ya Tanzania kuna visiwa ambavyo vinahitajika duniani. Tudhibiti visiwa hivi visichukuliwe na bahari na baadaye vikapotea kabisa kwenye ramani ya dunia. Tanzania ni bara na visiwa vyake na hasa maeneo ya pwani. Maeneo kama ya Nungwi, Kizimkazi, Makunduchi, Mkoani, haya tayari maji yanapanda juu na yameshaathiri makazi ya wananchi na huduma mbalimbali za kijamii. Ni vyema sasa tukawekeza zaidi kuhifadhi visiwa hivi kwa sababu maji ya bahari yana nguvu kubwa yanapoingia kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea naomba nichangie kuhusu hapo hapo kwenye mazingira. Ukataji wa miti bado umekuwa mkubwa. Ukataji wa miti hauendani na uwekezaji wa miti. Tufanye tathmini ya kutosha, uwekezaji wetu wa miti unaendana na uhalisia wa miti iliyoota? Kwa sababu, tunawekeza fedha nyingi katika kupanda miti, lakini hatuna uhakika wa kutosha kwamba miti ile yote iliyopandwa inakua na inastawi. Tukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam tu, mkaa unaotumika kwa mwezi ni tani ngapi? Kila tani kwa wastani ni miti mingapi? Miti mingapi kwa wastani ni hekta ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutazame hapo, tani zinazotumika kwa mwezi na miti inayokatwa kwa mwezi; kwa maana mti tunajua unatoa kiasi gani, kilo ngapi, halafu tuone sasa tani zilizokatwa miti ni hekta ngapi? Je, na upandaji wa miti unawiana na ukataji ule wa miti? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea, Tanzania tuna ardhi ya kutosha, tuna misitu, tuna eneo kubwa, lakini kuna fedha nyingi zimewekezwa kwenye mambo ya hewa ya ukaa. Kwenye hewa ya ukaa bado Tanzania hatujasaini, lakini kuna nchi ambao ni majirani zetu wa Afrika ikiwemo Kenya, Burundi, inatarajia kusaini; Gabon, Mozambique, Malawi, wameshasaini mkataba ambapo katika mkataba huo kuna ajira zitapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ajira zitakazopatikana kwa ajili ya uwekezaji kwenye hewa ya ukaa na fedha nyingi zitapatikana kwenye hewa ya ukaa. Kama ajira milioni 30 zinategemea kupatikana ifikapo mwaka 2030, lakini pia inatarajiwa kupata fedha kwa kupitia biashara karibu Shilingi trilioni 14, sisi tumekwama wapi? Au kuna masharti magumu ambayo hayaendani na mila na desturi zetu? Kama hakuna masharti ya namna hiyo, basi tunapaswa na sisi kujiunga na kusaini, ili tuweze kufaidika na hizi fedha na uwekezaji wa ajira mkubwa ambao unapatikana kwenye hewa hii ya ukaa ambayo tayari nchi jirani zetu wameshajiunga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka kuishauri Serikali, ni kwenye utunzaji wa mazingira…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)