Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini naomba pia ikikupendeza au ikupendeze, endapo nitakukwaza kwa muda wako basi univumilie kidogo ili tuweze kusaidia mchango kwenye otuba hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja, na pia nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu ndiye nguzo anayehakikisha kwamba Muungano wetu huu unaendelea kubaki kuwa Muungano; lakini ni kiongozi anayeongoza kwa upenzi, kwa masilizano, kwa mashirikiano wala haongozi kwa bakora. Kwa hiyo mimi naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini vile vile naomba nimpongeze na Rais wa Zanzibar kwa sababu watu wawili hawa ndio wanaotengeneza kitu kinachoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bila ya hawa na bila ya kufuata misingi ya Katiba, Sheria na Kanuni zetu maana yake hakuna kitu kinachoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na wasaidizi wake wote, bila ya kuwasahu wenzetu waliopewa dhamana ya kusimamia Wizara inayohusu mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa leo niende kwenye namba lakini sitaingia kwenye namba, leo nitaingia kwenye foundation ya Muungano. Wenzetu hawa wamepewa chombo kikubwa sana, wamepewa chombo ambacho ndicho kinachoshikamanisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bila Dira kukihenga henga chombo hiki sisi sote hapa hatuna sababu ya kuwepo. Kwa sababu tunakuwekwa hapa kwa kuwaenzi wazee wetu walipoamua, na wazee wetu waliamua kuunda kitu kinachoitwa Tanzania si kwa sababu ya Sheria, si kwa sababu ya Kanuni ila ni kwa sababu ya mapenzi waliyokuwa nayo kwa kitu kinaitwa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba ninukuu kidogo na ikupendeze. Kwenye katiba yetu hii kwenye eneo la kwanza kabisa la utangulizi, halafu mengine yatafuata; naomba ninukuu kwa heshima. Anasema hivi, Misingi ya Katiba; Na kwa kuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa haikuzungumzwa katiba wala sheria, naomba nirudie, imesema misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Wasomi wamekuja baadaye wakatutengenezea mambo yote haya lakini kubwa ni uhuru na imani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maana yake ni nini? Naomba niwaombe ndugu zetu hasa waliopewa dhamana ya kuunda au kusimamia Wizara inayohusu mambo ya Muungano, kwamba wako wazee wetu waliounganisha pamoja na mama yangu amesema pale kwamba tumeunganisha mchanga sasa tunaunganisha damu. Sasa naomba niseme hivi iko misingi ya kuunganisha zaidi imetajwa katika Katiba yetu, lakini kuna Vyombo viwili ambavyo vimetajwa katika Katiba hii ambavyo wasomi wetu wametuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye ukurasa wa 88 wa Katiba hii au kwenye Kifungu cha 102 kwenye Sura ya Nne inazungumza kitu kinachoitwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Maana yake Sura yote ya Nne inazungumza uwepo wa Zanzibar na Serikali yake. Vile vile, kwa maana hiyo hiyo kuna kitu kinaitwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kuna kitu kinaitwa Makamu wa Rais, kuna kitu Kinaitwa Waziri Mkuu, lakini kuna hiki kitu kinaitwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivi ndivyo vifaa vilivyoundwa kwa mujibu wa Katiba hii ili kuifanya Katiba yetu na nchi yetu iwe moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ombi langu ni hili, sababu ya kunukuu hii inaonekana au wengine wasomi wanaamini kwamba Katiba ndio Tanzania. Naomba tu niwambie Tanzania ni mapenzi ya damu. Tuliwahi kusema huko nyuma kwamba tumeungana kwa sababu ya mapenzi, ningewaomba wenzetu hasa wanaosimamia hili, waelewe kwamba wapo walioamua kwa makusudi ili kuifanya Tanzania ibaki kuwa Tanzania. Kwa hiyo ombi langu sana kwao, waendelee kuheshimu makubaliano tuliyokubaliana, wameyataja wenzetu wengi hapa. Kuna mambo ya ajira, kuna mambo ya mazingira, kuna mambo mengi tu. Naomba waendelee kuheshimu kwa sababu dhamana hii waliyopewa waelewe kwamba ina kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwakumbushe wenzangu kwamba tumetoka mbali. Mara baada ya Muungano wa mwaka 1964 kulikuwa na kitu kinaitwa mutiny, sijui kama mliwahi kukumbuka vijana wenzangu, hii kwa Kiswahili ni uasi lakini kwa sababu kuna kitu kinaitwa Jamhuri, naomba niwakumbushe wenzangu kwamba uwepo wa Zanzibar ndio ulisababisha Muungano ukawepo kwa sababu jeshi lililoko upande wa Zanzibar lilikuja kuchukua nafasi huku ili kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kuwa salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuelewe kwamba, kwanza kila upande wa Muungano kwa maana ya Zanzibar na Bara wote ni maeneo yaliyo sawa kwa mujibu wa Katiba hii. Hata hivyo, kwa maana hiyo hiyo ningeomba kwamba hata Wabunge walioko humu nashukuru hata katiba imesema, Wabunge wote waliotoka kwenye majimbo, waliotoka kwenye maeneo mbalimbali wote ni Wabunge walio sawa, hakuna aliye bora wala hakuna aliye na daraja la pili. Kwa hiyo, ningeomba sana wenzetu wa Muungano waendelee kutekeleza dhima yao ya kuhakikisha kwamba Muungano unaendelea kudumu kwa sababu sasa si matashi tena, sasa ni damu. Hatuna nafasi ya kurudi nyuma tunayo nafasi ya kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kuendelea. Kuna hoja wameizungumza wenzangu hapa, kwamba hoja ya jambo la mazingira. Amesema Profesa pale na amesema dada yangu pale kwamba tumeweka bajeti asilimia ndogo kwa ajili ya kupambana na mazingira. Wanasema kutenda kosa sio kosa, lakini kosa ni kurudia kosa. Ningeomba sana na hili namwomba Mheshimiwa Waziri alitafakari sana kwa sababu kuishi ni haki yetu kwa mujibu wa Katiba, lakini kutengeneza matatizo ambayo yatatufanya sote tuondoke ni kinyume cha Katiba, kwa sababu Katiba inatutaka tuishi, imetupa mamlaka ya haki ya kuishi. Kwa hiyo, ningeomba wenzetu wa Wizara kwamba bajeti inayokuja wahakikishe kwamba kwa asilimia kubwa lazima tutengeneze mazingira ya ku-survive sisi kama Tanzania. Tunapoendelea kutegemea wafadhili hata kama kwa sababu wamefanya commitment. Commitment ni jambo lingine, lakini commitment inatakiwa ianze na sisi kama watanzania. Kwa sababu hatuwezi kusubiri mwenzetu ajengewe ukuta kwa sababu athari inamuathiri Nungwi kule eti mpaka mfadhili aje, lazima tuanze sisi wenyewe, tusisubiri wafadhili waje eti ndio tuanze kujenga ukuta wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Tanga pale kunaliwa na Bahari, eti tumsubiri mfadhili aje atufanye kazi ya kutujengea ukuta kwa sababu sisi hatuna nafasi hiyo. Naomba sana kwamba tuzingatie bajeti yetu kwa maana lazima iwe na priority ya mambo yetu ya athari za mazingira kwa sababu ni wajibu wetu na ni haki yetu kuishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, pamoja na kwamba muda umeisha ningeomba sana kwamba suala la mazingira ni suala la kufa na kupona…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Dakika moja.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
NAIBU SPIKA: Endelea dakika moja.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Naomba sana kwa sababu ya muda ningeomba sana wenzetu wa Wizara inayohusu mambo ya Mazingira, mazingira ni suala la kufa na kupona sio la kumsubiri mfadhili eti atuonee huruma au aji-commit leo, atoe mwaka 2025, huo ni wajibu wetu sisi kama Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)