Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ambayo tunategemea ukuaji wake na mchango wake ni mkubwa sana kwenye maendeleo ya nchi yetu hii na kwenye Pato la Taifa. Nakupongeza Mheshimiwa Waziri na wataalam wako wote Wizarani; mnafanya kazi kubwa na nzuri na kila mwananchi wa Tanzania anaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Madini imeendelea kukua miaka hadi miaka. Kwenye uchangiaji wa Pato la Taifa pia imeendelea kufanya vizuri na ukuaji wake kila mtu anauona. Tunawapongeza sana kwa hili na kwa kweli tuna imani kwamba ile mipango ya kufikia zaidi ya asilimia kumi na itaweza kufika kwa wakati na pato lake kwa Taifa litakuwa linaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapowapongeza hawa lazima pia tuwapongeze wachimbaji wadogo, wachimbaji wetu wadogo nao pia wameendelea kufanya vizuri. Wameweza kuendelea kuongeza uzalishaji na kuweza kuchangia kwenye pato la Taifa. Katika madini yote ambayo yanapatikana, asilimia 40 yanapatikana kutoka kwa wachimbaji wadogo; lazima tuwapongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wadogo hawa ambao wanachangia zaidi ya asilimia 40, maisha yao ambayo wanaishi hayaakisi kile ambacho wao wanakizalisha. Na hayaakisi hivi kwa sababu ya kodi nyingi na ada mbalimbali ambazo wao wanatozwa. Leo hii baada ya Wizara na mfumo mzima wa uchimbaji kuwa vizuri, sasa taasisi nyingine zote za kimapato zinaangalia uchimbaji huu mdogomdogo kama vyanzo vyao vya kutafuta mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumza kodi ambazo zinamkabili mchimbaji mdogo ni nyingi sana kiasi kwamba inasababisha mchimbaji huyu anazalisha kwa nguvu kubwa sana lakini tija kwake yeye binafsi inakuwa ndogo sana. Niombe kama Serikali muweze kukaa muone namna bora zaidi za kumpunguzia kodi mchimbaji huyu mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi hizi pia ziweze kukaa ziwe na utaratibu mzuri zaidi wa kumuwezesha badala ya kuwa wao kazi yao ni kuzuia. Leo mchimbaji mdogo anapoanza kufanya kazi yake zinakuja taasisi nyingine, badala ya kumsaidia, kumshauri vizuri, wao kazi yao wanakuja pale kumuwekea vikwazo ambavyo vinasababisha mchimbaji huyu ashindwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anakuja kudai jambo dogo tu anakwambia sasa hapa tunasimamisha uzalishaji wako mpaka ulipe hii kodi au ulipe hii ada. Na hiyo inakwenda kwenye ngazi kuanzia ya TRA wenyewe, hizi taasisi zinazozunguka mpaka kwenye ngazi ya kijiji. Leo mpaka mtendaji wa kijiji anafika pale anakwambia kwamba hujalipa service levy au ada hii hapa ndogo, uzalishaji usimame mpaka ulipe. Namna hii hatutaweza kumkomboa mchimbaji mdogo, lazima hizi sheria pia ziweze kubadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo upande wa STAMICO. Wamefanya kazi nzuri, tunawapongeza sana. Kutoka kuwa shirika mfu ambalo lilikuwa linataka kufutwa mpaka ilifikia hatua wanashindwa kulipa mishahara yao. Lakini sasa hivi wameweza kupiga hatua kubwa sana na wameweza kuzalisha faida ya zaidi ya bilioni 70 kwa mwaka; hii ni hatua kubwa sana. Tuwapongeze na tuwape moyo, wanaweza wakafanya mambo makubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri, Serikali iliangalie sana Shirika la STAMICO, linaweza likafanya miradi mikubwa na ya kimkakati na uzalishaji ukaongezeka na uchangiaji kwenye pato la Taifa ukawa mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyozungumza habari ya STAMICO, tuangalie sheria ya uanzishaji wake. Tunaweza tukaibadilisha sheria ya uanzishaji wa STAMICO na yenyewe ikawa wasimamizi badala ya Serikali kwenye ule uchimbaji wa madini mwingine wowote ambao Serikali inaingia, badala ya kuanzisha kampuni ndogondogo za kila siku, yenyewe sasa ikasimama badala ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikwenda ikulu pale kushuhudia makubaliano na kusaini mikataba lakini kulikuwa na makampuni mbalimbali ambayo yameanzishwa na Serikali ambayo yameingia ubia na hayo makampuni ya nje kwa ajili ya uzalishaji. Sasa badala ya kuanzisha makampuni madogo madogo mengi kila tunapotaka kuanza uchimbaji sasa tuipe jukumu hili STAMICO ili waweze kuifanya kazi hiyo. Nina imani STAMICO wanaweza wakafanya kazi hiyo vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia kwenye STAMICO hapa namna ambavyo wameendelea kwenda na ubunifu na sasa wamekuja na mkaa rafiki. Ni teknolojia ambayo wameanza nayo na ni nzuri, na ikiendelea hivi itasaidia sana mkaa huu kwenda kuwa mbadala wa ile mikaa ambayo inatumiwa ya miti na kuhakikisha kwamba mazingira yetu yanaendelea kuwa safi na salama kwa muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mkaa rafiki ambao unazalishwa na STAMICO, hii teknolojia ambayo wao wameifanya, mimi nishauri kwamba badala ya kuendelea nayo wao waiuze kwa Taasisi nyingine kama SIDO au VETA ili wao sasa waje waipeleke kwenye jamii huku chini na baadaye uzalishaji wake uweze kufanyika huko. Badala ya wao kuibuni na wao pia waendelee kuweza kuzalisha na kuuza huko mtaani. Wao wabakie na mambo makubwa makubwa kama ambayo wanaendelea nayo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakiendelea na mambo makubwa haya ambayo sisi tunayasema ili kuweza kuifanya STAMICO ikue kwa uwanda mpana zaidi. Leo mfano tunazungumza makaa ya mawe, haya makaa ya mawe ndiyo ambayo leo yanazalisha umeme. Je, sisi kutumia STAMICO tunaisadia vipi hii nchi yetu STAMICO iweze kuzalisha umeme mkubwa zaidi uweze kuingia kwenye Gridi yetu ya Taifa ili uweze kutusaidia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwamba sasa badala ya STAMICO kwenda kuzalisha hii miradi mingine midogo midogo, ijiwekeze kwenda kwenye kuzalisha umeme uwe mkubwa zaidi, tutoke sasa hivi tunataka tuzalishe kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere megawati elfu mbili na, twende kupitia makaa ya mawe chini ya STAMICO tufikirie miaka 10, 20 mbele uzalishaji wa umeme uweze kufikia megawati 10,000 mpaka 15,000 kupitia makaa ya mawe. Jambo ambalo linawezekana, ni kuwawezesha tu STAMICO waweze kufanya kazi hiyo vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa STAMICO wakati Mheshimiwa Rais anapokea Ripoti ya CAG tuliona alisema kuna baadhi ya mashirika na taasisi nyingine yamekuwa hayana faida kwa sasa hivi. Tutolee mfano NDC; NDC imekuwa inasimamia Mradi ule wa Liganga pamoja na Mchuchuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu imekuwa ni stori ya miaka nenda rudi, niombe sana kuishauri Serikali iweze kubadilisha sheria ili ule Mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma uweze kutoka kule ulipokuwepo kwa maana ya Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya NDC uweze kuja sasa Wizara ya Madini na isimamiwe na STAMICO ili sasa uchimbaji uweze kufanyika na baadaye iweze kuleta tija kubwa sana kwenye nchi yetu hii. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeisaidia STAMICO na itakuwa ina miradi mikubwa na sisi tutakuwa tumeweza kwenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya GST, GST pamoja na kazi nzuri ambazo wanaendelea kufanya bado wanapata bajeti ndogo na mazingira yao ya kazi siyo mazuri. Tukiweza kuwekeza vizuri kwenye utafiti maana yake wachimbaji wetu hawa wadogo wadogo na wa kati wataweza kufanya kazi zao kwa kujua nini ambacho wanakifanya, nini ambacho watakipata chini badala ya sasa hivi tunafanya uchimbaji wa kupiga ramli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwawezeshe hawa GST waweze kufanya kazi yao vizuri zaidi, wawe na vifaa vya kutosha. Leo wameagiza mitambo ya kuchoronga mitano na mingine inakuja, ni mwanzo mzuri lakini tuweze kwenda mbali zaidi na taarifa zao za GST ziweze kuwafikia wachimbaji wadogo hawa, ndiyo itakuwa ukombozi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza hapa kwenye mapato haya ambayo yamepatikana ya uchimbaji asilimia 40 yamezalishwa na wachimbaji wadogo lakini wachimbaji wadogo hawa hatujaweza kuwawezesha vizuri kuhakikisha kwamba uchimbaji wao utakuwa na tija na kuweza kuwasaidia.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kasaka, malizia mchango wako.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)