Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia Hoja iliyoko mbele yetu ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa uhai na afya njema kwa siku ya leo kuweza kusimama kwenye Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja hii iliyoko mbele yetu. Ni hoja nzuri na nilikuwa nimejipanga vizuri sana kuweza kuchangia lakini kwa bahati nzuri hoja hii kwa kweli imenifilisi kwa kiasi kikubwa, lakini nitaendelea kutoa ushauri kwa sababu nilikuwa nimejipanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri wa Madini, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Katibu wa Wizara pamoja na timu yote kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya katika Wizara hii; hongera sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo yangu ni machache sana; kuipongeza na kuishauri Serikali kupitia hii Wizara ya Madini. Nianze kwanza kwa kuwapongeza wachimbaji wadogo ambao wanaendelea kuchangia pato la Taifa kwa kiwango kikubwa, kwa asilimia 40, kwa dhahabu yote ambayo inapatikana Nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wasemi wanasema unapotaka kumkamua ng’ombe ili akutolee maziwa mengi ni vyema ukamnenepesha. Kwa nini nasema hivyo; nizishukuru taasisi za kifedha kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo, lakini naomba iendelee kutoa zaidi na kupunguza masharti kwa wachimbaji wetu wadogo ili waweze kupata vifaa vya kisasa waweze kuzalisha dhahabu kwa wingi na kuweza kuzidi asilimia ambayo sasa hivi wanachangia, asilimia 40. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vichache sana kwa hawa wachimbaji wadogo ambavyo vinahitajika ni kama vile compressor, crusher, bombing, winch, digger, vilipuzi na vifaa vingine. Vifaa hivi wakiweza kukopeshwa wachimbaji wetu wadogo wakaondoka kwenye uchimbaji duni uliopo hivi sasa wa kutumia kushusha ama kupandisha mawe kutoka chini kwa kutumia roller ama kuingia ndani kwa kutumia mock wanaita ukweli uzalishaji utakuwa ni mkubwa na mapato yao yatakuwa makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naiomba Wizara izidi kuzishawishi taasisi za kibenki ziweze kupunguza masharti ili kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo waweze na wao kunufaika na mali hii iliyoko chini ambayo ni aina ya dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mchimbaji mdogo ninaomba Wizara hii iweze kuwasaidia wachimbaji wadogo, hususan wenye leseni kupitia GST waweze kuchimba maeneo ambayo yameshafanyiwa utafiti. Lakini pia GST ipunguze gharama zake za kuwafanyia utafiti hawa wachimbaji kutoka kwenye gharama ya shilingi 432,000 kwa mita na waweze kushusha angalau ifike hata shilingi 200,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakifanya hivyo watakuwa wamewasaidia sana hawa wachimbaji wadogo, pamoja na kwamba mnawakopesha wanakwenda kuchimba kwa kutumia ramli mafanikio hayatakuwepo. Lakini GST mkiwapunguzia hawa wachimbaji gharama za uchorongaji na mkaingia nao makubaliano, hata kama kwa malipo kidogo kidogo, watakuwa wanaifanya kazi kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, nadhani unanisikia, nakuomba ulichukue hili. Washauri sana GST waweze kupunguza gharama za utafiti za uchorongaji ili wananchi wetu waweze kunufaika na uchimbaji wao kuliko kutumia uchimbaji unaoitwa uchimbaji wa ramli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa madini unaliingizia Taifa fedha nyingi. Lakini pia uchimbaji unaendelea kwa kasi na tukumbuke kwamba tunapopata mapato tuhakikishe mazingira yetu na yenyewe tunayaweka kwenye hali nzuri. Tusiangalie ukusanyaji wa mapato tu wakati mazingira yetu yanaharibika. Wachimbaji wetu wadogo wanaharibu mazingira sana kwa kutumia miti ambayo wanaifunga kama vile matimba kuingia kwenye mashapo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishauri ili tuweze kupunguza uharibifu wa mazingira haya basi Wizara ichukue angalau wachimbaji wachache iwapeleke nchi mbalimbali kama vile China na South Africa kwenda kuona namna gani wenzetu hawatumii miti, wanatumia utaalamu gani ama vifaa gani vya kuweza kujenga yale mashapu kutoendelea na kutumia miti, watumie utaalamu huo wa kisasa. Tutakuwa tumeokoa uharibifu wa mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana hili suala la uharibifu wa mazingira, sisi wachimbaji wadogo kwa kweli ni waharibifu wakubwa kwa sababu inapotokea sehemu kunaitwa lashi, watu wanachimba na zinapokata zile dhahabu wanaondoka wanaliacha lile eneo likiwa lina hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe kama kuna uwezekano, wakati uchimbaji huo unaendelea, waendelee kupanda miti ili iweze kusaidia kutengeneza mazingira hata ikitokea wameondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikupongeze tena kwa mara nyingine pamoja na Wizara yako. Ninamuomba Mheshimiwa Rais kama ananiona, kama kuna uwezekano basi Wizara hii atengeneze kautaratibu kazuri ka kutoa tuzo kwa viongozi hawa wenye taasisi hii kama vile Waziri, Naibu Waziri, Makatibu wake na wote kwa ujumla, taasisi hii angalau basi ipate tuzo kwa sababu tukiangalia kutoka 2017 mpaka leo 2023 mapato kupitia madini yamepanda kwa kiwango cha hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Naunga mkono hoja. (Makofi)