Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Madini. Namshukuru Waziri wa Madini, Naibu Waziri, Katibu na Viongozi wote wa Wizara ya Madini, wanafanya vizuri sana kwenye Wizara hii, wameitoa mbali na sasa hivi inakua ilipotoka asilimia 4.7 mpaka hiyo asilimia Tisa sasa inaenda ni jambo la kupongeza sana. Ahsanteni sana kwa kuifanya Wizara ionekane ni Wizara ya maana sana kwa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa haya ma-“b” anayoweza kuweka kwenye Wizara ya Madini tumeona mikataba ya ma–“bi” na ma–“bi” inaongezeka maana yake yote ni maono yake katika nchi hii ya kuona madini yetu yatumike vizuri kutoka ardhini yaingie kwa wananchi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri ambayo anafanya Mheshimiwa Waziri Dotto, kusema kweli wachimbaji wadogo amewatoa mbali sana hawakuwa hapo, ametoa maeneo mengi sana amesaidia migodi mingi sana kwenye mazingira lakini nimuombe Mheshimiwa Dotto atazame maeneo kama matatu ya wachimbaji wadogo, wakiwemo wachimbaji wadogo wa Jimbo langu wanaitwa Nyabuzume na Nyaburundu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni PL hizi leseni kubwa za utafiti zinachukuliwa na wachimbaji wakubwa wanakaa nazo miaka, hata kama hawachimbi wachimbaji wadogo wanazunguka hapo pembeni hakuna kupewa, wanakaa nazo miaka mingi, utafiti miaka mia, kwa hiyo nadhani hilo nalo uliangalie ili wachimbaji wadogo wanaozunguka migodi mikubwa au maeneo ya wachimbaji wakubwa waachie maeneo mengine kwa wachimbaji wadogo, hilo ni jambo kubwa sana kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni PML hizi nazo ni leseni ndogo zinazokatwa wachimbaji wadogo, nao wamekuwa kama mafisadi na wenyewe. Wengine ana PML tano, 10, 40, 50 zinakaa kwa muda mrefu wenzao wanazunguka humu ndani hamna kitu, hata wale wengine viongozi wao nao wana ma-PL ya kutosha, hilo nalo uende ulitazame viongozi wachimbaji wadogo wapewe maeneo yanayotosha kwa ajili ya uchimbaji

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ni mitaji. Wamezungumza Wabunge wengi hapa, nikamsikiliza mwingine anasema twende tukamwambie Mheshimiwa Mwigulu Wizara ya Fedha itupe fedha, hizo ni ndoto! Kuomba Wizara ya Fedha ikupe mikopo ya wachimbaji wadogo hizo ni ndoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dotto nikuombe, mimi najiuliza hivi watu wa mbolea wanafanyaje amezungumza hapa Mheshimiwa Nyongo hapa, tunakopesha tunaleta mbolea tunagawa kwa wakulima tunaipa ruzuku mbolea maana yake hiyo ruzuku inaenda kutusaidia kwenye maeneo yetu inaleta chakula humu ndani. Sasa kwa nini hatutoi ruzuku kwa wachimbaji wadogo, ambao ndiyo wanaleta fedha kwenye nchi hii, wachimbaji wadogo ndio wanaoleta fedha hatuwapi ruzuku kwa nini sasa? Na hii kazi inatakiwa kufanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa dotto nikuambie kitu kioja nenda NMB benki, nenda CRDB benki nenda Benki ya Exim, nenda benki zote unazoona zinafaa uweke nao mkatabawa kukopesha wachimbaji wadogo. Mchimbaji mdogo asiende benki mwenyewe, umpeleke wewe ufanye kitengo humu kwenye Wizara yako, uende uongee nao wako tayari kuwakopesha wachimbaji lakini ukisubiri Wizara ya Fedha ikupe fedha na miradi mikubwa tuliyonayo ya mikakati hizo ndoto, hizo ndoto kama jina lako ni ndoto tu! nendeni CRDB, NMB kaa nao panga nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kwa mfano, wanapoenda wachimbaji wadogo wanaambiwa kwamba vifaa unavyotaka ni Milioni 100, Milioni 100 wanataka asilimia 20, asilimia 20 hapa unazungumza milioni 200 au milioni 50 wanapata wapi hiyo Milioni 50? Unawaambia ulete nyumba, ulete kila kitu watapata wapi hizo nyumba zinatoka wapi? Hawakopeshwi! Kwa hiyo, wewe chukua hicho kitengo chukua wachimbaji wadogo walete maandiko yao, proposal zao uzione, nenda kwenye mabenki ongea nao, mabenki wawakopeshe ninyi mtakuwa ni dhamana ya hawa wachimbaji wadogo, kwa hiyo naomba hili nalo ulichukue uweze kuliweka sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo lipo Mheshimiwa Dotto nakushukuru sana kwanza kwa kufungulia wale watu wa Kinyambwiga, wachimbaji wadogo wanapokuwa na migogoro mnawafungia kwa muda mrefu sana, mimi huwa najiuliza maswali mengi sana hivi ulishaona Wabunge tunaoshindwa kwenye uchaguzi? Ulishamuona Mbunge mzuri aliyeshindwa kwenye uchaguzi? Unajua anawakimbia hata watu hataki kuwaona, sasa kama kazi yako wewe inayokupa chakula au inayokuweka uwe na heshima ukishindwa unasononeka, kwa nini umfungie mchimbaji mdogo miezi sita, mwaka, anakula wapi? Kuna mamantilie wako hapo, kuna watu wa maji wanapeleka, kuna watu wa maziwa wanapeleka mnafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa madini unakua kwa asilimia 9.7 mpaka asilimia 10 inaenda, kama uchumi unakua na wachimbaji wadogo wanakuwa maskini maana yake nini? Maana yake haufunganishwi sasa na uchumi wa wachimbaji wadogo. Nikumombe Mheshimiwa Doto kwamba wachimbaji wadogo sasa umewapeleka mahali pazuri, uwasimamie wakue. Kadri uchumi wa madini unavyokua na wenyewe wakue sasa waweze kuendelea kwenye shughuli za kuleta maendeleo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna vitu vingi vya kujiuliza hapa wachimbaji wadogo wakipata madini mahali mkubwa naye anakata leseni anakaa nayo wanawakimbiza mnaenda kuwafungia, yaani wao wamekuwa kama vibarua, wakipata hapa madini wanahama wakipata madini wanahama hivi haitokei siku moja wakapata madini mkawapa? Mkasema sasa tunawapa eneo hili lote, kwa hiyo sisi wachimbaji wadogo tukiwa tunapata madini maeneo mengine mnawagawia watu wengine wakubwa sisi tunakuwa kama vibarua tu. Ninakuomba kwenye hilo nalo ulitazame vizuri ili wachimbaji wadogo hawa wapate mitaji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili suala la vifaa, kama ni mabenki basi kama ni Wizara ya Madini kwa nini isikope sasa, kopeni hivyo vifaa vya wachimbaji wadogo halafu ninyi muwape kwa sababu ninyi ndiyo mnawajua, kwa nini muwambie benki ziwape na hazina dhamana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri kwamba ninyi kopeni hivyo vifaa vitafuteni, kwa mfano watu sasa wanataka kupima kufanya utafiti wa kutosha kujua hapa kuna madini wasihamehame, madini kama vifaa vile vya utafiti mita moja ni rola 130 ukifanya utafiti. Kwa hiyo unapotoboa matundu matatu ni dola kama 390, sasa dola kama 300 maana yake ni kwa hela ya kitanzania mchimbaji mdogo hawezi kufanya utafiti. Kwanini kama walivyosema STAMICO, GST msiwape fedha wakawasaidia wachimbaji wadogo kuwapimia maeneo ambayo wanajua kwamba kuna dhahabu, hapa sasa wamekuwa wanatoboa hapa wanahama wanatoboa hapa wanahama sasa nchi nzima itakuwa matobo tu! Tutafute vifaa vya kutosha vya kuonesha kwamba hapa jamani kuna dhahabu muweze kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dotto ninakuomba baada ya bajeti yako kupitishwa hapa naomba uende Nyabuzume Jimbo la Bunda uende Nyaburundu Jimbo la Bunda, uwasaidie wale wachimbaji wadogo wapate mikopo kuna dhahabu pale mabilioni na mabilioni ya matani ya dhahabu iko pale tuwasaidie wapate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)