Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi niweze kuchangia katika hii Wizara ya Madini. Nitaungana na wenzangu tu kumshukuru Ndugu yetu Waziri Biteko pamoja na Naibu Waziri. Kusema kweli kazi yao inaonekana na hasa pale ambapo wameweza kujitahidi kuhakikisha kwamba ndani ya muda mfupi wachimbaji wadogo wanaweza kuchangia kwa 40%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli katika nani yangu nitajikita tu kwa hawa wachimbaji wadogo maana ninawaona wako majirani zangu pale wa Buhemba naona ni namna gani wanahangaika. Wako majirani zangu wa Sirorisimba lakini hata kule kwa Kinyigoti. Tunaona kwamba ni kwa kiasi gani ambavyo wanapambana sana wanajitahidi lakini wanakumbana na vikwazo vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Wizara imejitahidi sana kuwasaidia lakini tunadhani inahitaji ifanye zaidi ya hapo. Uzuri wa wachimbaji wadogo kwanza uzuri wao ni kwamba wana multiplier effects. Yaani mchimbaji mdogo akipata, yaani utaona amejenga nyumba, akipata ameendelea kufanya biashara nyingine yaani ile fedha anayoipta anarudi ku- reinvest. Kwa hiyo, hii inasaidia sana katika kwanza mzunguko wa fedha lakini na kukuza uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tofauti na wale wawekezaji ambao wanatoka nje wakubwa tunawahitaji lakini wao ni kwamba zaidi ya ile kodi ambayo tunabahatisha tunapata, hata CSR yenyewe wanatoa kwa mbinde sana. Kwa hiyo, tuna kila aina ya sababu na nikuombe Mheshimiwa Doto, umefanya kazi nzuri na kazi kubwa, nawewe kama kiongozi wa Wizara hii mojawapo ya kazi kubwa ya kiongozi ni kufanya mambo yafanyike. Sasa kati ya jambo moja ambalo unahitaji ulifanye hebu jipe malengo ndani ya miaka miwili, mitatu hawa wachimbaji wadogo sasa watoke 40% waende 60%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hilo ni jambo ambalo najua leo ukiamua Mheshimiwa Waziri Doto ni jambo linalowezekana sana. Wachimbaji wadogo hawa yako baadhi ya changamoto ambazo wanapambana nazo. Moja yaani yeye kwanza wao ndiyo wavumbuzi wa madini hasa ya dhahabu. Anachokifanya huwezi kuamini, mchimbaji mdogo anahangaika huko porini anakuja anakutana na mwamba, wa pili anakuja, mwingine anakuja mwisho wanakuwa wengi pale. Anatokea tu mtu wa kawaida anaenda pale na GPS anachukua coordinates akitoka pale anaenda kwenye portal tayari analipa shilingi 50,000 lile eneo linakuwa ni la kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake wale wachimbaji wadogo waliokuwa wanachimba pale wote wanaondolewa, lile eneo unapewa wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli yaani tunawapa adha kubwa. Kwa hiyo, ombi langu Mheshimiwa Waziri ambalo linawezekana, hebu yeyote yule wachimbaji wadogo wakishaanza pale, kwanza wanatambulika mpaka kwenye vijji vile wanavyofanya kazi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inapotokea tukitaka kuwasaidia inapotokea kwamba kuna mtu ameenda pale ameingiza kwenye GPS amepata coordinates na amechukua lile eneo, kabla hamjampa, hebu tuangalie nani alianza, ni wale wachimbaji wadogo au ni yeye. Kama ni wachimbaji wadogo ndiyo walianza, hebu tuwasaidie wale wachimbaji wadogo ndiyo waendelee kuchimba pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo tutawasaidia sana maana shida kubwa ambayo wanaipata ni kwamba wao yaani wakishatafuta, wakipata wanaondolewa hapo. Wakienda mahali pengine wakitafuta wakipata, wanaondolewa hapo. Sasa kusema kweli hii haiwasaidii sana katika kuwa kuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizao lao la pili ambalo wanakumbana nalo ni namna ya kupata ile miamba. Yaani wao wanakuwa tu ni kama waganga wa kienyeji. Anaenda anahangaika hapa miezi sita hajapata kitu anahama. Anaenda mahali pengine anahangaika hajapata kitu anahama. Mwisho anakuja kubahatisha kamchirizi kamwamba kidogo basi ndipo anapata hapo fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nini kifanyike katika kuwasaidia? Natambua kwamba ndugu zetu wa STAMICO ndiyo caretaker wa hawa wachimbaji wadogo. Lakini ukiangalia leo majukumu waliyonayo STAMICO wanamajukumu mengi. Wana majukumu makubwa na kusema kweli wanafanya kazi nzuri sasa tukisema tena wao waendelee kuwa ma-caretaker wa hawa wachimbaji wadogo hiyo nafasi hawana kwa sababu wakifanya huku ni bure lakini sasa unaachaje uzalishaji wako halafu utumie muda mwingi kwa ajili ya kuwasaidia hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaweza kufanya vitu viwili; moja, aidha tukatafuta chombo kingine kama labda GST wakawa wanafanya hiyo kazi ya kuwatafutia miamba. Maana unakuta yeye mchimbaji mdogo yule leo anachimba hapa, akikosa anaenda mahali pengine. Lakini kumbe ingekuwa mfano leo ukija kama pale Buhemba watafiti wakaja pale kama ni GST au chombo, taasisi yoyote ile ikawaonyesha kwamba mwamba ni huu maana yake ni kwamba wangeweza kufanya kazi kubwa sana kuliko ambavyo wanahangaika hivi sasa. Kwa hiyo, kama ombi langu tuone namna ya kuwasaidia wale wachimbaji wadogo katika kutambua ile miamba halafu wao waendelee kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza yaani mchimbaji mdogo hata akipata mwamba tu wa sentimita 50 yaani huo tu umetosha kumtajirisha. Kwa sababu wanatumia muda mwingi kufanya kazi ya kubahatisha na ndiyo maana wanaendelea kupoteza na unakuta siku hizi wanakuja watu sijui tuwaite matapeli au ndiyo hivyo tena, wanakuja kwamba na vimashine vya kudanganya na anapitapita hivi nadhani ni metal detector, kakishasema hapa anaambiwa chimba hapa. Anaenda mita 30 hamna kitu, anaenda pengine hamna kitu, kwa hiyo hali hii nadhani haiwasaidii sana wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri kama utauchukua huo ushauri wa kuhakikisha kwamba tuna chombo ambacho kazi yake ni kuwatafuta yaani leo nikisema pale Sirorisimba uchimbaji wa pale unakuja unawatafutia.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mathayo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mchangiaji kwamba ili waweze kufanikiwa hawa wachimbaji wetu wadogo, GST pamoja na STAMICO wapunguze gharama za utafiti. Mfano, mita moja sasa hivi wana-charge shilingi 432,000. Kwa kufanya utafiti wa mita 60 ni sawa na shilingi 29,000,000. Mchimbaji mdogo atazipata wapi? Kwa hiyo wapunguze hizo gharama ili wananchi wetu waweze kufanikiwa.

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Mathayo taarifa unaipokea?

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa mimi naipokea kwa mikono miwili, kwamba inavyoonekana hawa watu wengi iwe GST iwe STAMICO na wengineo nadhani gharama wamechukua zile gharama za zamani zile ambazo wazungu walikuwa wanazileta huku kwetu hizo ndizo wamekuja wame-copy na ku-paste. Kwa hiyo, unakuta leo unapomzungumzia mchimbaji mdogo kwamba atumie utafiti hataweza ndiyo maana wanahangaika hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo leo sasa kwa kadiri tunavyoenda.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mathayo malizia muda wako umeisha.

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nasema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)