Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Vwawa kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa na wananchi wa nchi hii na pia Baraza la Mawaziri na viongozi wengine wote ambao wamepewa dhamana ya kuiongoza nchi hii, nawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba niupongeze Uongozi wa Bunge, nikitambua kabisa kwamba kazi kubwa tuliyonayo ya Bunge hili ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Kama kazi yetu ni kuisimamia Serikali na kuishauri, maana yake kama mambo yatakuwa hayaendi vizuri, basi Bunge hili haliwezi kukwepa wajibu kwamba hatujafanya kazi yetu vizuri ya kuisimamia na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, napenda nichukue nafasi hii kuwashukuruni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa kwamba sasa tumepata viongozi wazuri wanaoweza kuikokota na kuisukuma nchi yetu ikafika kuwa nchi ya kipato cha kati. Kwa muda mrefu tulikuwa tunatafuta viongozi, tulikuwa tunatafuta Rais ambaye ana maono ya mbali, sasa Mungu ametupa uwezo, tumebahatika tumepata Rais mwenye maono ya mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni tajiri sana kwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba, ambayo imejaa karibu kila kona. Tuna madini ya kila namna, tuna misitu, tuna mlima mrefu kuliko milima yote katika Afrika na wa pili duniani kwa urefu, tuna mbuga nyingi za wanyama, mito, maziwa, bahari na zaidi ya hapo tuna watu zaidi ya milioni 53. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni competitive advantage ambayo tunayo. Kwa maana hiyo, tuna vitu vingi vinavyoweza kuiwezesha nchi yetu kuendelea na kufika kuwa nchi ya kipato cha kati. Sasa tatizo kwa muda mrefu limekuwa ni nini? Tatizo kubwa ni tatizo la uongozi na hili ndio limekuwa likitusumbua sana. Sasa wakati huu tumepata viongozi, nadhani tutaweza kwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha kwa kuleta Mpango huu na kueleza dira na kuonekana mambo ambayo tunaweza kuyafanya. Mpango huu umezingatia dira ya Taifa na pia umezingatia Hotuba ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba nichangie katika eneo la kilimo. Katika Mpango huu kilimo bado hakijapewa nafasi nzuri sana na hakijapewa mkazo kama ambavyo kingekuwa kimepewa. Sisi kule Wanavwawa ni wakulima, wananchi wa Vwawa wanalima sana, tunalima kahawa kwa wingi, mahindi, tunalima mazao mengi na tunaamini kabisa kama Serikali itatuwekea misingi mizuri, ikatupatia pembejeo kwa wakati, tuna uwezo wa kuzalisha chakula kwa kingi ambacho kinaweza kikatumika sehemu nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe wazo kwamba tusiseme mazao ya biashara, sasa kila zao ni zao la biashara, hata mahindi ni zao la biashara, hata maharage ni zao la biashara. Kwa hiyo, mazao yote yanayoweza kulimwa yapewe uzito unaostahili ili tuweze kuzalisha chakula kingi, tuweze kuzalisha kwa ajili ya kuuza sehemu zinginezo. Kwa hiyo, kilimo ni muhimu sana tukakipa uzito unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, ambayo ningependa nichangie, tumezungumzia viwanda, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa ni Serikali ya viwanda. Hata hivyo, viwanda ambavyo tumesema, nimesoma kwenye huu Mpango hatujaainisha, tunataka viwanda vingapi na viwe wapi? Hilo hatujalisema, lakini pia tulikuwa na viwanda vingi sana ambavyo vilijengwa katika nchi hii, nini kilitokea viwanda hivyo vyote vikafa? Tulikuwa na mikakati mingi ambayo tuliweka juu ya viwanda, tumejifunza nini katika mipango yote tuliyokuwa nayo katika kujenga viwanda vilivyopita? Sasa haya yanatakiwa yawe ni msingi mzuri wa kutuwezesha kuweka mikakati mizuri ya kuweza kujenga viwanda tunavyovihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ili tuweze kwenda sambamba kufika kwenye hiyo nchi ya viwanda, tunahitaji viwezesha, vitu vitakavyotuwezesha kufika huko, tunahitaji umeme, barabara na vitu vingine vingi. Sasa naomba nichangie kwenye suala la umeme; umeme wa REA umesambazwa nchi nzima katika vijiji vingi sana. Katika Jimbo langu kule watu wengi wamepata, lakini vijiji vingi bado havina umeme. Kuna Vijiji kama Nanyara, Nswiga, Irabii umeme unapita juu kwa miaka mingi, unawaruka wananchi unakwenda wapi, wananchi wale wanahitaji wapate ule umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema kwamba umeme ni muhimu sana na Mheshimiwa Waziri wa Nishati ameona kule kuna joto ardhi, kule kuna chanzo kizuri sana cha kuweza kuzalisha umeme. Naomba mkazo uwepo katika kuanzisha na kutumia nishati hii inayotokana na joto ardhi ambayo inaweza ikatusaidia sana kutukwamua katika suala hili la umeme ambalo ni muhimu sana katika kuipeleka nchi kuwa nchi ya kipato cha kati.
Suala lingine ambalo ningependa kuchangia, ili tuweze kuwa nchi ya kipato cha kati, tunahitaji wataalam wetu, tunahitaji watu wawe na ujuzi wa kuweza kufanya kazi na kuweza kutekeleza majukumu yetu. Sasa hivi vyuo vyetu tulivyonavyo na mfumo wa elimu tulionao, hauwaandai vijana kuweza kupata ujuzi unaohitajika sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tunayo kazi kubwa ambayo napenda nishauri, Wizara ya Elimu tutafakari kwa undani mitaala tuliyonayo inatuandaa, inawaandaa vijana wetu kwenda kuwa nchi ya kipato cha kati? Sasa hivi mkazo utatiliwa kwenye Vyuo vya Elimu ya Juu. Naomba nishauri, lazima tuwe na vyuo vingi vinavyotoa elimu ya kati tertiary institutions ambazo zitatoa wataalam watakaoweza kushiriki kufanya kazi katika viwanda tunavyovihitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye upande wa elimu, ningependa mitaala ile wakati inaandaliwa, iandaliwe vizuri, iwe ni demand driven rather than supply driven, halafu wapatiwe sehemu za kwenda kufanya field ili waweze kuiva na kukomaa hilo litatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka naomba nishauri mambo mengine yafuatayo:-
Kwanza, ili tuweze kufika na kutekeleza mpango huu ambao ni mzuri, nashauri, lazima tuweke nguvu sana katika ukusanyaji wa mapato, bila kukusanya mapato huu Mpango utakuwa hautekelezeki. Sasa hivi lazima tuweke mkakati wa kutosha wa kuhakikisha kwamba nchi inajitegemea kimapato kuliko kutegemea wafadhili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tubadilike kifikra ili watu watambue kwamba wajibu wa maendeleo ya nchi hii ni sisi wenyewe ndiyo tutakaoleta maendeleo, ni wananchi wa nchi hii ndiyo watakaoleta maendeleo na si mtu mwingine.
La tatu, naomba kushauri, tumekuwa tukiimba kila wakati kwamba huko vijijini wananchi wanahitaji huduma za fedha, bila kupeleka huduma za fedha, bila kuanzisha hizi micro-institutions za kuweza kuwa-support wakulima, ku-support watu mbalimbali huko vijijini, ku-support vikundi mbalimbali, hatuwezi kuleta maendeleo ya kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri tuimarishe huduma za fedha mpaka vijijini ili wananchi wetu waweze kupata mikopo mbalimbali na kugharamia vitu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni vipaumbele, tunahitaji tuwe na vipaumbele vichache, ambavyo vitagharamiwa na Serikali. Viwanda naamini vitagharamiwa vitakuwa vinaendeshwa na watu binafsi siyo Serikali tena. Sitegemei kuona Serikali inaweka mkono mkubwa wa kuendesha viwanda wakati uwezo wetu ni mdogo, labda viwanda vile ambavyo ni strategic, lakini viwanda vitaendeshwa na private sector. Katika maeneo ya elimu, kilimo, uvuvi na ufugaji, afya na maji, miundombinu, barabara, viwanja vya ndege, umeme; hivyo Serikali lazima iwekeze vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba nishauri tumezungumzia sana kwamba tunahitaji viongozi ili waweze kuisukuma nchi hii. Hata hivyo, katika nchi hii hatuna utaratibu wa kuandaa viongozi, wala wa kuwafundisha, wala kuwaelekeza namna ya kutekeleza majukumu yao.
Sasa umefika wakati tuwe na mfumo mzuri wa kutambua viongozi wazuri na kuwaendeleza na kutambua vipaji vyao ili wakabidhiwe kufuatana na uwezo walionao. Hilo litatusaidia kuwa na viongozi wanaoweza kujenga, wazalendo wenye uwezo wa kuleta maendeleo ya kweli katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana na pia naomba Serikali izingatie mawazo yetu. (Makofi)