Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye imempendeza ameturuzuku uhai kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kwenye Wizara hii ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu na ni muhimu sana kipekee kwa sisi watu wa Ukanda wa Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali, tulikuwa na kilio cha muda mrefu cha kutokuwa na mnada wa uhakika pale kwenye border yetu ya Horohoro. Mnada ule umekamilika, tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na kukamilika kwa mnada ule na wananchi wale kufurahia jambo lile, lakini mnada ule umekuwa kero kwa sababu tangu kukamilika kwa mradi ule mwanzoni mwa mwaka huu mpaka leo mnada ule haujafunguliwa. Mheshimiwa Ulega, hili unaliweza, nakuomba sana. Tukimaliza tu Wizara yako, assignment ya kwanza nakuomba ndugu yangu twende tukafungue mnada ule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkandarasi yule anakataa kukabidhi kwa sababu anatudai karibu milioni 100. Hizi tuna uwezo nazo, twendeni tukafungue mnada ule. Tunapoteza fursa ya mapato kwa sababu hali ya upande wa pili kwa wenzetu Kenya ni mbaya kwenye minada yao. Kwa hiyo, tukifungua mnada ule tumepiga bao. Twende tukafanye jambo hili kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tuliomba majosho kumi tukapata mawili, si haba, tunaishukuru Serikali tulipata jumla ya milioni 46 tukapeleka Kibewani na kule Mkota. Tunaomba yale yaliyobakia mtufikirie.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile pale Duga tuna josho ambalo tulilijenga tangu mwaka 1972; limechakaa. Nakuomba sana josho lile ni muhimu lifanyiwe kazi kwa haraka hususan kwa hili ambalo mmelifanya jambo kubwa la kuleta mnada mkubwa pale Horohoro. Tunaiomba sana Serikali iangalie eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali na sisi ni wanufaika kwenye maeneo yale ya kupata boti. Pale Zingibari ndugu zangu wamepata maboti, ndugu zangu wa Mwaboza wamepata boti na tunaye mvuvi mmoja mwingine binafsi na yeye amepata boti; tunashukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mmekuwa mkitusaidia kutoa mbegu kwa wakulima wetu wa mwani, tunashukuru sana. Lakini tunahitaji kuongeza jitihada. Mwani unazalishwa kwa wingi lakini uongezaji wa thamani ni mtihani. Tunaomba sana Serikali mliangalie eneo hili; kuongeza thamani ya mwani wetu ili wananchi wale waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu, Mheshimiwa Ulega, mlituahidi kwamba mtatujengea kituo cha kutotoa vifaranga. Ahadi hii kama umeisahau vile; nakuomba ikumbuke ahadi hii. Tunashukuru mnatuletea Mradi wa Bahari Mali kwa kushirikiana na wenzetu wa IUCN ambapo vikundi vyetu vitatu vitakuwa sehemu ya mradi ule; tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba – ndugu yangu Waziri unajua, ukipeleka jambo zuri kama hili kwa watu wenye uhitaji ambao ni wengi, jambo lile badala ya kuwa neema linageuka kuwa kero. Ninawasihi sana, sambamba na mradi huu, Serikali angalieni maarifa mengine ya kuongeza ukubwa wa mradi huu ili wananchi wetu wa Ukanda wa Pwani waweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nimeisikia bajeti yako, eneo moja limenisikitisha; tumeingiza lita milioni 11.6 za maziwa zenye thamani ya bilioni 22. Hizi ni fedha ambazo tungeweza kuwasaidia wananchi wetu tukazalisha maziwa kwa wingi ndani ya nchi tukaokoa fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesafirisha maziwa kwenda nje lita 278,000. Kwa hiyo, ukiangalia uwiano tumeingiza zaidi kuliko tulivyouza nje. Tuliangalie vizuri eneo hili, hatuna sababu ya kuagiza maziwa nje, tuna uwezo wa kuzalisha maziwa ndani ya nchi yetu tukajitosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia makusanyo ya Wizara, na Kamati imefanya kazi nzuri, imetuonesha; hali hairidhishi. Tulikusudia kukusanya bilioni 80, tumekusanya bilioni 30; only 37 percent; hii haiwezi kuwa sawa. Tuongeze maarifa zaidi tukusanye zaidi, tuna uwezo wa kufanya hivyo. Na hasa kwenye sekta ya uvuvi, tulikusudia kukusanya bilioni 40, tumekusanya bilioni 13; only 33 percent.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage amesema pale; kwenye eneo hili la uvuvi na ufugaji wa samaki hatupaswi kuwa na kiwango hiki. Yaani mchango wa sekta ya uvuvi kuwa asilimia moja haiwezi kuwa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sekta ambayo ulimwenguni uingizaji wake ni mkubwa sana, hatujafanya vizuri, tuongeze bidii kwenye eneo la ufugaji wa samaki ili tuondoe umaskini kwa wananchi wetu, tujihakikishie usalama wa chakula na lishe katika nchi yetu. Sekta hii ina uwezo wa kututoa. Hatuwezi kusifiwa kuwa nchi ya maziwa makuu, hatuwezi kusifiwa kwamba ni nchi yenye ukanda mkubwa wa bahari lakini ufugaji wa samaki haueleweki; hii haiwezi kuwa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu, Mheshimiwa Ulega na timu yako uliyonayo sasa, najua tukiamua kuweka mkazo kwenye eneo la ufugaji wa samaki tunaweza kupiga bao. Na hiki kigugumizi cha ufugaji wa samaki kwenye Ukanda wa Pwani kinatoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ulega, wewe mtu wa pwani, unajua umaskini wetu watu wa pwani wakati tuna rasilimali ya bahari. Twendeni tukafanye kazi ya kuwaondolea wananchi umaskini kupitia ufugaji wa samaki kwenye eneo la ukanda wa bahari.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru; ahsante. (Makofi)