Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante ili na mimi kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo ameendelea kuweka mikakati katika Wizara hii na kuhakikisha suala zima la mifugo katika nchi hii linakuwa endelevu na lenye tija. Nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na wafanyakazi wote wa Wizara kwa namna walivyoanza vizuri kufanya kazi. Pia nipongeze kwa ripoti nzuri hii ambayo imewasilishwa katika Bunge hili, iliyojaa mikakati na namna ya kwenda kumkomboa hasa mfugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu, wafugaji, hasa wafugaji wa asili, wanategemea mifugo kwa kila kitu. Wanategemea mifugo katika mahitaji ya kujisomesha na kwa ajili ya chakula; na kwa kila kitu mfugaji wa asili anategemea mifugo ili aweze kujikwamua kiuchumi. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba tunapoongelea mifugo maana yake tunaongelea uchumi, sasa ni uchumi upi tunao uzungumzia katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni kumekuwa na chanagamoto nyingi sana. Jambo ambalo linawakwaza wafugaji wasione suala zima la ufugaji kama linaleta tija na kuweza kujikwamua kiuchumi ni kwa sababu wafugaji wa nchi hii wamekuwa ni watu ambao ni wakukimbizana hapa na pale wakiwa ni watu waliosahaulika, kwa sababu wafugaji wanakuwa ni kama wakimbizi katika nchi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu kumekuwa na migogoro mingi sana baina ya wafugaji pamoja na hifadhi zetu. Lakini tunashukuru kwa sababu migogoro mingi kati ya wafugaji na wakulima sasa imepungua kwa asilimia kubwa. Hata hivyo haya yote yanatokana na sababu kwamba Serikali haijaweka mkazo katika kuhakikisha maeneo yote ya malisho katika halmashauri zetu yametengwa. Haya ninayasema kwa sababu mamlaka zetu hazijasimamia kuhakikisha kila halmashauri kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya malisho. Hii imesababisha migogoro kuendelea kila siku katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayasema haya kwa mifano hai. Tuna mifano ya wafugaji ambao wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara na mifugo yao ikiendelea kutaifishwa na kupigwa minada. Baada ya kutaifishwa na kupigwa minada wafugaji wanabaki wakiwa maskini, kitu ambacho kinasababisha wale wafugaji waone kwamba kazi ya ufugaji si kazi ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu sasa kwa Serikali, niombe sasa mamlaka husika wakasimamie maazimio ya mikutano ilifanyika baina ya wadau wa ufugaji pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye aliongoza ule mkutano uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya; kwamba kila Wilaya sasa iende ikatenge maeneo ya malisho ili kuondoa migogoro. Migogoro hii inasababisha mifugo mingine kukatwa, kujeruhiwa na kufa. Migogoro hii imesababisha hata wafugaji wengi kupoteza maisha na wengine kuwa walemavu. Kwa hiyo niombe sana mamlaka hizi zikasimamie ili walau wafugaji waone wana haki ya kufuga na kujipatia kipato katika familia zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, nipende kugusia suala zima la utambuzi, usajili na ufatiliaji. Tusiposimamia suala hili katika nchi yetu tuna uhakikia hata masoko ya nje hatutaenda kufanya vizuri. Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa kwamba utaratibu wa kuweka hereni katika mifugo ulisitishwa; lakini sasa, mkakati wa Serikali ni nini? Tunaendaje kutambua mifugo yetu? Tusipofanya hivi ni lazima sisi hatutaingia kwenye soko la ushindani na hatma yake hatutaweza kuingiza kipato katika nchi hii na masoko yetu hayatakubaliwa. Tukiweza kuwatambua wanyama wetu itatusaidia kuweka mkakati na kuwatambua, kwa mfano, suala la usalama kwa wanyama wale.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale wanyama kuna nchi zingine bila kuwa na hereni hawawezi kupokea mnyama, hawakubaliki kwa sababu hawatambuliki na hawana uthibitisho. Kwa hiyo niombe Serikali sasa ije na mpango ambao hautakuwa na maumivu kwa wafugaji ili suala hili la kuweka alama na kuwatambua wanyama wetu iende kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, pamoja na kuwa na mifugo mingi katika nchi yetu, lakini kama nchi tumeshindwa kupata faida kubwa kutokana na mifugo. Hii ni kwa sababu sisi hatujawekeza lakini tumekuwa na ushuru na utitiri mwingi wa tozo katika nchi yetu ambayo inafanya wafanyabiashara wengi wa nyama kushindwa kufanya biashara ya nyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano; ukiangalia tozo zilizopo katika nchi yetu na nchi jirani ya Kenya, Tanzania kuna tozo zaidi ya kumi lakini wenzetu wa Kenya wenyewe wana tozo tatu. Hii inasababisha na kurahisisha sasa hata mfanyabiashara wa nyama wa Tanzania kuona ugumu kufanya biashara Tanzania na kukimbia nchi za jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ghrama zetu pia ziko juu sana. Kwa mfano suala la kuchinja mbuzi; Tanzania tunachinja mbuzi kwa shilingi 6,500 lakini Kenya wao wanachinja kwa 150 ambayo ni sawa na shilingi 2,700 kwa bei ya Tanzania. Hili suala naomba Wizara iliangalie ili kurahisisha wale wafanyabiashara wanaosafirisha nyama waweze kufanya biashara hii zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile kuna tozo ambazo hata hazina umuhimu sana. Kwa mfano autonics certificate kuna hizi za meat crown ambazo zingeweza kufanywa kupitia zile tozo za uchinjaji ili kumrahisishia mfanya biashara aweze kufanya biashara bila kupata maumivu yoyote. Pia suala pia la usafirishaji limekuwa la gharama kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie namna Wizara inavyoweza kufanya ili kuweza kuinyanyua hii sekta ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwanza kuhusu minada. Minada yetu haimpi faida mfugaji, anayepata faida ni yule anayeuza nyama. Mfugaji anapokwenda mnadani kuuza nyama hawatumii kipimo chochote isipokuwa ni makubaliano tu, kwamba huyu ng’ombe anafaa kuuzwa laki tano au milioni; lakini yule anayeuza nyama lazima aweke kwenye kilo. Kwa hiyo moja kwa moja ukiangalia mfugaji hapati faida, anayepata faida ni yule anayeuza nyama. Sasa, niiombe Serikali iweke mizani katika minada yetu ili ng’ombe wapimwe kilo wakati wa mauzo, walau hata sasa na mfugaji anaweza akapata faida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni ombi, hasa katika Mkoa wetu wa Manyara. Kwamba, katika miaka miwili mitatu tumekumbwa sana na suala la ukame. Niiombe Serikali iwachimbie wafugaji mabwawa ya kutosha ili inapofika msimu ule wa ukame wanyama waweze kupata maji ya kutosha na waweze kuhimiri... (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)