Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa heshima na mimi kuchangia Wizara ya Mifugo. Kwanza naishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi, namshukuru Mheshimiwa Ulega, bajeti yake kwakweli ameisoma kwa uchungu sana, na ameonesha kwamba ni kijana ambaye amedhamiria kufanya kazi kubwa, nakushukuru sana. Na mimi nadhani Mama Samia hatua anayoenda nayo kuna watu anawaona moyo wao unataka nini. Nadhani alikuona moyo wako unataka kuimarisha na kuwakomboa wafugaji kwenye mateso waliyonayo sasa hivi na watu wa uvuvi, nadhani unafanya kazi vizuri. Kwa maana hiyo moja kwa moja naunga mkono hoja yako kabla sijaendelea, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kufanya kazi kubwa ya kuwaamini Mawaziri wake. Mimi nadhani katika uongozi huu kama Waziri hata perform huyo atakuwa na shida yake binafsi. Mheshimiwa Rais anawaamini sana, anawapa ninyi mumpelekee mawazo. Kwa hiyo Mheshimiwa Ulega mpelekee mawazo ya wafugaji; kwamba kama tuna kopa kwa ajili ya mambo mengi hakuna eneo la kukopea kama kukopa kwa ajili ya kuimarisha mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Rais anaweza kukopa popote, kwa sababu ukichukua wafugaji wote, mali zote za wafugaji ng’ombe, mbuzi na kila kitu ulichotaja hapa ni trioni 25, na ukichukua samaki peke yake ni trioni 846. Sasa, trioni zote hizo manashindwaje kukopa kuimarisha, tuna shida gani ya kukopa ili kuimarisha trioni za fedha? Sasa unapewa milioni 200 ndugu yangu, sijui bilioni mbili, sijui bilioni tatu inatosha wapi? Haitoshi. Kama nchi inaweza kukopa ikope kwa ajili ya kuimarisha ufugaji na uvuvi. Mimi nadhani hilo ni jambo zuri sana la kufanya katika nchi yetu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda mbali nataka nizungumze jambo moja tu. Mheshimiwa Waziri umesema habari ya kupeleka mizani kwenye minada; na umezungumza kwa uchungu sana nimeiona moyoni mwako. Nataka nikupe tahadhari, tena tahadhari kubwa. Usipokuwa makini ukipeleka hiyo mizani bila kuwapa elimu wafugaji utakuta minada iko mitupu, na hasa minada ya vijijini. Mauzo ya ng’ombe hayategemei mizani peke yake. Nataka nikupe mfano; mimi nikiwa na maksai kumi inawezekana maksai sita ndizo zenye uwezo wa kununua milioni moja, maksai nyingine zote zinakuwa chini ya milioni moja, labda inakuwa laki nane au laki saba. Mimi nikikutana na mfugaji anayenunua ng’ombe yule mnunuzi namuuzia maksai kumi zote kwa milioni moja, zile zingine zote zinabebwa na maksai sita. Kwa hiyo ukienda kwa mizani inawezekana mtu asiuze ng’ombe zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, achunge sana hili neno; kama anakwenda huko afanye utafiti kwanza kabla hajapeleka mizani vinginevyo atakwenda kuua minada; watu watauzia majumbani hakuna mtu atakayepeleka ng’ombe mnadani. Lazima twende tuwaelimisha wafugaji juu ya hasara anayoweza kuipata kutokana na hili jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri amezungumzia habari ya mashamba darasa. Mashamba darasa maana yake ni kwamba uwe na maafisa ugani wa kutosha. Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeseme 2025 tuwe na afisa ugani kwa kila kijiji. Tuna vijiji 12,319, unao? Unao wa mashamba darasa? Asilimia 35 ya maafisa ugani ndio walioko vijijini sasa hivi; unao hao wa mashamba darasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani imesema tupeleke majosho kwa kila kijiji. Tuna vijiji 12,319. Kwenye jimbo langu katika vijiji 35 ambavyo vina wafugaji wa kutosha ni vijiji 10 tu ndivyo vina majosho, na majosho yenyewe mnaenda kufanya nyie watu wa Wizara. Siku hizi mna mtindo mnapeleka milioni 22 mnaenda kuchimba majosho. Unachimba josho la milioni 22 halina kisima, halina kibanio halafu unaliacha hapo, halafu fedha yenyewe inatoka Wizarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemuona hapo Mheshimiwa Waziri, aende akafumue huo mtindo. kwa nini fedha ya kijijini ikae Wizarani? Walaji gani wanakaa Wizarani na fedha haiji kiasi kwamba josho linajengwa kwa miaka miwili hadi miaka mitatu?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kata ya Salama kuna josho limebomoka, naomba aende alitengeneze. Kwenye Kijiji cha Salakwa hamna josho, kwenye Kijiji cha Maliwanda hamna josho, vijiji takriban 20 havina josho. Nitamletea aweze kuangalia kwamba kwanini inafanyika hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuzungumze mashamba ya NARCO; sasa najiuliza, NARCO ni biashara au ni nini? Mashamba ya Serikali ya NARCO na mashamba mengine ya Serikali mliyonayo ni ya biashara au ni ya watu? Ni ya watu au ni ya Serikali au? Mimi sielewi sasa Kwa sababu kama mna ng’ombe, mashamba yenye kutunza ng’ombe milioni 42 leo mnatunza ng’ombe 19,000. Sasa mimi nashindwa kuelewa haya mashamba ni ya nani? Kila mtu shamba lake, kila meneja shamba lake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, kama anaweza kama anaitendea haki hii Wizara aanzishe mamlaka ya wafugaji. Mimi nashindwa kuelewa, hivi leo nchi yetu inashindwa kuwa na mamlaka ya Samaki na ng’ombe ilhali tuna Mamlaka ya TAWA, tuna TARURA, tuna RUWASA na tuna TFS. Mna mali ya kutosha kutoka kwa wafugaji lakini mnashindwa kuweka mamlaka, kwa sababu gani? Sijawahi kuona nchi ina mamilioni ya fedha kwenye maeneo kama hii…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Chumi uko salama hapo? (Kicheko)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, niko salama kama ambavyo Singo yuko salama.

NAIBU SPIKA: Nashukuru, nashukuru. (Kicheko)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipunguza sauti sawa. Kwa hiyo naomba nchi yetu itengeneze mamlaka ya wafugaji ili iwalinde wafugaji, wafugaji wanashida. Waheshimiwa Wabunge wa CCM na wale wa NEC mliomo humu ndani, katika eneo ambalo hatujafanya vizuri Tanzania ni la wafugaji. Wafugaji hatuwafanyii vizuri, hatuwatendei vizuri kabisa. Tunaomba hii Wizara mama aitendee vizuri, tunamuomba sana Mheshimiwa Rais na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa. Mimi nimekuja na kitabu hapa, ninacho hapa. Katika eneo la wafugaji hatujafanya vizuri; tuna ilani hapa hatujafanya vizuri katika eneo la wafugaji. Tuwalinde wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuja hapa na lile suala la herein; sasa katika ilani inasema hivi, tuwatambue wafugaji wenyewe, mifugo yao na wafugaji yenyewe. Sisi hereni tunawekea ng’ombe tu mfugaji hatujui tunamwekea nini, au na yeye tuna mwekea hereni? Sasa unawezaje kumwekea herein, is not sustainability. Unawekaje hereni kwenye mfugo, uweke leo kesho usijue unaweka nini? Ndama anazaliwa leo hakuna hereni. Tunaanzisha vitu ambavyo havina maana. Hata kama tungeuza hereni kwa bei nafuu lakini where is sustainability? Iko wapi sasa? Leo mtu anazalisha ng’ombe unampa hereni moja kesho kutwa anauwezo gani wa kuangalia?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa taarifa, ni wapi taarifa. Haya Mheshimiwa Tabasam.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Anazungumzia suala la heleni hawa ng’ombe wako madume na majike, sasa heleni wanatakiwa wavikwe. Je, watavishwa madume peke yake au na majike? Kwa sababu wakivishwa majike…

NAIBU SPIKA: Ahsante, Mheshimiwa Getere.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: …akivishwa dume inakuwa ni hatari kama atavaa heleni.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa heleni sio mbaya, ni mzuri kwa maeneo yaliyoandaliwa, ni mzuri kwenye ranchi ni mzuri kwa maeneo yaliyoandaliwa siyo vijijini. Mtu hana simu hana nini eti unamlazimisha kununua heleni halafu anaiona ng’ombe wake…

MBUNGE FULANI: Taarifa, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa mnamchukulia muda wake, endelea Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili jambo la hereni nalo tuliwekee utaratibu mzuri ili tuweze kwenda nalo.

Mheshimiwa Waziri umezungumza habari ya mikopo ya wafugaji; ni kweli benki ya NMB inakopesha wafugaji kwa asilimia tisa, ni kweli, lakini masharti ya kupata mkopo eh! kazi ipo; kupata mkopo kazi ipo. Ni kweli benki ya NMB inafanya kazi nzuri, hata kwenye jimbo langu inafanya kzi nzuri sana ya kukopesha mikopo lakini nani anawasimamia wafugaji wapate mikopo. Kwanza unapewa masharti uwe na clearance, uwe sijui na vitu gani. Unatumia kama laki tano laki sita halafu unaomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)