Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii kuweza kuchangia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu wake. Niwapongeze kwa muda mfupi Mheshimiwa Waziri na mabadiliko ambayo tunayaona tukipitia Kamati yetu ambayo yanakwenda kutokea ndani ya Wizara ya Uvuvi. Vile vile nichukue nafasi hii nimshukuru na kumpongeza kwa kumwalika Waziri kutoka Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili limetupa moyo hususani kwa sisi tunaotoka Zanzibar. Mheshimiwa Waziri nimpongeze amekuwa Waziri wa mfano kwenye suala hili. Wanapoalikana kwenye vikao kama hivi, wanajenga umoja na kazi kuifanya iwe ya pamoja. Hata hivyo, kwa sababu Mheshimiwa Waziri amealikwa na yeye yupo ajifunze kupitia hili. Sio vibaya, sio kosa, sio dhambi kusema kwamba kuna baadhi ya Mawaziri ambao shughuli zetu zinaingiliana kuweza kuwaalika ndani ya Baraza la Wawakilishi. Huu kwa Mheshimiwa Waziri umekuwa mfano, naamini wengine watasoma kutoka kwake na Mawaziri wengine watasoma kutoka kwake. Hili liwe endelevu kwa wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii zaidi kuishauri Wizara, kwa muda huu mambo makubwa ambayo nimeyaona ni ya kushauri, kwa sababu Waziri kwa muda mfupi ambao amekabidhiwa Wizara, sisi tukiwa kama Wajumbe wa Kamati tumeanza kuona mabadiliko na mwelekeo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hakupewa Wizara hii kwa bahati mbaya. Tunatamani atimize kiu ya Watanzania kwenye Wizara hii. Wizara yake pia imebeba sera za vijana, kiu za vijana ni ajira, kuondokana na matatizo ya ajira. Wizara hii ina majibu tosha kwenye suala la ajira. Uvuvi ni ajira, ufugaji ni ajira tena tuchukue fursa hii na nimshauri Mheshimiwa Waziri, atumie fursa kubwa kuwaonesha vijana kuna nini ndani ya ufugaji na kuna nini ndani ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Watanzania hawaelewi thamani ya kufuga ni nini? Mtu yeyote ambaye ni mbaya anamtazama mfanyabiashara anaekwenda kufanya biashara, jioni anamfikiria kakusanya shilingi ngapi? Mtu mbaya ndipo anapoelekea au jambazi, lakini Tanzania hii hii tuna wafugaji asubuhi mpaka jioni anatembea na mabilioni ya fedha anaongozana nayo. Watanzania au vijana wa Tanzania hawafahamu kama almasi, lulu na ule ufugaji pia ni almasi lulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri achukue muda huu awaelimishe vijana wa Tanzania wafunguke. Mtu akisikia suala la ufugaji, akisikia suala la uvuvi anadhani kwamba, watu wa aina fulani au tabaka la aina fulani ndio wanaohusika na kuvua, lakini pia wanahusika na suala la ufugaji. Haipo hivyo, uvuvi ni utajiri, lulu inakaa baharini, sawa na mchimba madini anapokwenda kutafuta madini ya kuchimba. Lulu iko kwenye bahari, samaki ni lulu yetu Watanzania, ufugaji ni lulu yetu Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunazungumza madini, lakini na haya kwetu ni madini na yanaweza pia kuwavusha Watanzania. Tanzania kila siku tukiamka asubuhi vijana tatizo kubwa ni ajira, ajira, ajira. Tumejielekeza ili uonekane unafanya kazi na umeajiriwa ufanye kazi ofisini, Wanadhani kwamba ufugaji sio sehemu ya ajira. Ufugaji una majibu ya ajira kwa vijana. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, woneshe dira kwa vijana, umri wao unatosha kutufungulia njia Watanzania, umri wao unatosha kuwaonesha vijana wenzenu wa Tanzania ufugaji una fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mtanzania mfugaji anamiliki mifugo anakwambia mifugo 10,000, mimi Mzanzibari nashangaa hee! Ng’ombe 10,000 tena! Ng’ombe 10,000 mpigie mahesabu ana mamilioni mangapi ameyaweka nyumbani? Namaanisha nini? Namaanisha hata mfugaji anahitaji kupewa elimu. Anahitaji kuelimishwa ili mifugo yake iwe mafunzo kwa wengine. Maana kama atauza kwa faida na kuonesha faida yake kwa Watanzania vijana wengi watashawishika kuingia kwenye suala la mifugo, lakini vile vile watauona umuhimu wa kuvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumwambia Mheshimiwa Waziri, vijana kiu yao yote ndani ya Tanzania, yote tunayoyafanya tisa, kumi wanataka suala la ajira. Tuwaoneshe ajira ya Watanzania iko hapa. Kaka yangu Waziri ni msikivu, Naibu Waziri wake ni msikivu ndio maana wametumia mezi michache kuanza kuleta chachu ya mabadiliko ndani ya Wizara. Siri ni moja tu, kama wataendelea hivyo watatuvusha na watampa matumaini aliyewateua. Usikivu wa Waziri ndio unaomfanya Waziri aweze kuwavusha watu salama. Sikiliza maoni ya watu ingawa sio maoni yote unaweza kuyakubali, lakini kwa sehemu usikivu wa Waziri na akichukua ushauri wa Kamati atafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshauri Waziri, tutumie muda kwanza kuwaelimisha wafugaji wetu juu ya suala la chanjo. Mambo mengi ukiyaona Tanzania yanagoma tatizo lake ni Mtanzania kutopewa elimu. Ukimwelimisha vya kutosha, ukampa fursa akuulize maswali umjibu aridhike, Mtanzania hana shida. Hivi mfugaji gani utakaemwambia ng’ombe hawa, mbuzi hawa, kondoo wakichanjwa tunaboresha nyama yake tunapata soko kubwa la nje, Mtanzania gani atakataa? Mfugaji gani atakataa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililokuwepo tunajiaminisha kwenye mipango yetu. Tukishapanga maofisini tunatumia nguvu kwenda kutoa maamuzi. Hili kwetu halitatufikisha kokote. Muda Waziri anaotaka kutoa maamuzi hususani yatakayowahusu wavuvi na wafugaji awafuate kwanza, awashauri wakubaliane, wazungumze hatopata pingamizi sehemu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini kama mfugaji wa sasa tena Mungu kajalia leo wapo hapa wengi, wafugaji wa leo umwambie kwamba baada ya ng’ombe kumuuza milioni moja utamuuza milioni moja na laki tano maana nyama yake itakwenda nje ya Tanzania, hawezi kukataa. Anakataa kwa sababu mara nyingi tuna maamuzi ya kibabe. Unaamua, unapanga halafu unamtolea maamuzi, ng’ombe wake, halafu wewe ndio unamtolea maamuzi, sio sahihi. Tushirikishe kwenye maamuzi, Waziri apange naye, azungumze naye, waone nini wanafanya atakuwa hana tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimekuja hasa na mambo ya kushauri, nimshauri Waziri, Taasisi zake nyingi ziko katika maeneo ya kukodi, wanakodi majengo hususani hapa Dodoma. Mheshimiwa Waziri, alipe kipaumbele suala la kujenga Ofisi kubwa ambayo taasisi zake zote ataziweka hapo. Leo mfugaji anatoka Mara anamtaka mtu wa uvuvi, sijui sekta gani iko jengo gani, sijui sekta gani iko jengo gani, sio sahihi. Ajenge jengo la Ofisi Dodoma ndiyo tumekwishahamia, bado hawajaamini kama tumehamia? Ndio tumeshafika. Wajenge jengo ambalo litakusanya taasisi zao zote ili waweze kufanya kazi na kuleta ufanisi na tija ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia ndani ya bajeti hii ili Mheshimiwa Waziri, aende vizuri, mipango yake iende vizuri lazima awe na ofisi nzuri, lazima awe na sehemu ambayo wafanyakazi wanafanya kazi vizuri. Leo unaenda hata huko kwa mpangaji kuna masharti, siku nyingine anaamua tu kufunga ofisi yake, siku nyingine anaamua tu leo hatufanyi kazi. Kwa hiyo, masharti ya wapangaji ni mengi. Dodoma tumeshafika, ndiko Makao Makuu ya Nchi, tunataka Waziri ajenge na taasisi zake zote zilizoko ndani ya Wizara yake zifanye kazi ndani ya jengo hilo. Ajenge jengo moja kubwa lilete faida, lilete tija kwa Watanzania ili kazi ziweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la sensa kwa mifugo. Suala la sensa kwa mifugo lina faida yake, lakini kwa nini Waziri kuna baadhi ya mambo hapati ushirikiano? Ni pale pale ninaporudi, kwa sababu hawatoi ushirikiano kwa watu wa chini. Kwa usikivu wao nawaomba suala la sensa litaenda kutupatia majibu ya kuona ng’ombe wangapi wako Tanzania na wanamilikiwa na akina nani? Hata hii migogoro ya kila siku ya wafugaji na wakulima itaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitegemei mfugaji halisi wa Tanzania ataenda kuingiza ng’ombe ndani ya shamba ya la Mtanzania mwenzie. Tuwape elimu wafahamu kwamba sote rasilimali ya Tanzania ni ya kwetu, haya mambo mengine yanasababishwa na watu waliokuwepo ndani ya mipaka ya Tanzania. Hata hivyo, ile migogoro likija zogo la wafugaji utasikia fulani, fulani ni wafugaji, Hapana, wengine ni wahamiaji, majirani zetu. Waziri afanye sensa tujue kitongoji, kata ina wafugaji wangapi, wenye kata yao wapange hapa mtafuga, hapa mtalima. Tatizo litatokea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mfugaji wa leo kweli atakataa kuambiwa hapa fuga, hapa nywesha maji?

Mpelekee maji ng’ombe wake, mihangaiko anayohangaika kuna muda hata ng’ombe anashindwa kunywa maji, watengeneza mabwawa, wawaoneshe maeneo ya kufuga hawana shida. Hii nchi ya Tanzania iko salama, ina amani kwa sababu watu wa nchi ya Tanzania ni wasikivu, waelewa, ndio maana ukaona mpaka leo Tanzania ina amani. Usikivu wao tuutumie vizuri kwa kuleta maendeleo kwao. Kama tutawasimamia vizuri Waziri na Naibu Waziri wakishuka chini, Wizara ya Uvuvi itabadilika, uvuvi hautodharauliwa na vijana na watu wataung’ang’ania kama wanaenda kuchimba dhahabu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tauhida, kengele yako ilikuwa imelia.

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)