Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika bajeti hii muhimu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Nianze kwanza, maana nisije nikasahau kuunga mkono hoja na kuwatia shime sana ndugu zangu hawa wawili Mheshimiwa Waziri ambaye ni mpya kwenye Wizara hiyo kwa maana ya kwamba ameaminiwa hivi karibuni na Mheshimiwa Rais kuongoza Wizara hiyo na Naibu Waziri pamoja na Watendaji wote wa Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri afahamu kwamba wakati bajeti yake inasomwa hapa huko Mkoani Kigoma na hasa kwa wadau wote wa Ziwa Tanganyika, kuna taharuki kubwa sana ya suala la taarifa ya ufungaji wa Ziwa Tanganyika, kwamba Serikali za Nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika zimekaa kukubaliana kufunga Ziwa kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe 15 ya mwezi huu ili kuruhusu samaki waendelee kukua na kuweza kuvunwa wakiwa katika hali ya ukubwa na ubora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka niseme kwamba jambo hili ni jema na niliye simama hapa kama mwakilishi wa wananchi sikusudii kulipinga, isipokuwa nakusudia kuweka maneno ambayo nafikiri Serikali ikiyachukua yatakuwa ya faida zaidi katika mpango wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nataka Serikali ielewe kwamba duniani zipo Serikali za aina nyingi, kuna Serikali za Kijeshi ambapo Baraza la Kijeshi ndiyo mmiliki wa Serikali hiyo. Zipo Serikali za Kifalme ambapo Mfalme na ukoo wake hata akifa huyu anarithi mwingine, zipo Serikali za Kisiasa kama ya kwetu ambapo Vyama vya Siasa vinakwenda kwenye uchaguzi, wananchi wanapiga kura, wanaunda Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana yangu ya kusema hivyo? Uendeshaji wa Serikali hizi hauwezi kuwa sawasawa, Serikali ya Kijeshi haina sababu ya kupata ridhaa ya wananchi, itafanya mambo yake yote kwa kuzingatia mitazamo yake. Hivyo hivyo Serikali ya Kifalme, lakini Serikali ya kisiasa inafanya mambo yake kuamua na kutekeleza kwa kuzingatia maoni ya wananchi na Serikali ya Kisiasa inakuwa na wamiliki wawili mmiliki wa kwanza ni chama kilichopewa ridhaa ya kuunda Serikali na mmiliki wa pili ni wananchi waliopiga kura za kuchagua Serikali ile. Kwa hiyo mipango yetu yote lazima iwe na ridhaa ya wananchi, tusikae Wizara na Wizara, Nchi na Nchi, Serikali na Serikali tukaamua mambo kwa niaba ya wananchi na kuwapelekea wananchi tu, wafuate hayo tuliyoamua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kufunga Ziwa ni suala jema, lakini halina ushirikishwaji wa wananchi na kama halina ushirikishwaji wa wananchi hapo linapata ubatili. Kwa maana hiyo ningependa kusema kama mwakilishi wa wananchi kwamba hebu turudi tushirikishe wananchi. Hata hivyo, dhana ya kufunga Ziwa ni ya kufikirika haina tafiti za kutosha, Mheshimiwa Waziri anakumbuka Ziwa Tanganyika kwa takribani miaka zaidi ya ishirini halijafanyiwa stock assessment, ni hivi karibuni wamefanya na hawajapata majibu ya stock assessment ya utafiti huo. Kwa hiyo dhana ya kufunga ni ya kufikirika tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tuliongea kwa maongezi ya kawaida kwamba hili ziwa lifungwe lazima kuwe na mambo ya msingi ya kutangulia. Wananchi waandaliwe wawe na ufugaji wa samaki sasa linalonisikitisha ni jambo moja wanataka kufunga Ziwa Tanganyika, lakini vizimba vya ufugaji wa samaki wamepeleka Lake Victoria. Ziwa Tanganyika hawakupeleka kizimba hata kimoja, lakini Ziwa Victoria wamepeleka vizimba 290 kwa taarifa nilizonazo. Hivi vizimba vingekuwa Ziwa Tanganyika na vinafanya kazi, leo tungesema fungeni maana wananchi wana alternative nyingine ya kupata kitoweo cha samaki, badala yake wamepeleka huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nataka niliseme, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na CCM iwe makini sana, tunaweza tukaja kutengeneza tabaka kwenye nchi yetu. Leo, hii Kigoma na Mikoa mingine resources zinazopelekwa za nchi ni kidogo sana. Hata hivyo, kuna maeneo vitu vinapelekwa vingi, nitatoa mfano sina nia mbaya. Nia yetu ni kujirekebisha ili twende pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapozungumza unapeleka vizimba, unapeleka mikopo mikubwa ya wavuvi Lake Victoria, lakini Lake Tanganyika hupeleki, unavutia maendeleo upande mmoja. Hata hivyo, huo upande unaovutia maendeleo, ndiyo ambao umejengwa daraja la bilioni 700 ambazo hazijawahi kuingia mkoa wowote. Huo Mkoa ambao umepeleka hivyo, ndiyo kuna meli tisa, Lake Tanganyika kuna meli tatu na kati ya meli tatu na kati ya hizo hakuna meli hata moja ambayo inafanya kazi. Huo mkoa unaopeleka hivyo vizimba ndiyo mkoa ambao reli ya SGR inajengwa imepelekwa huko kabla ya huku ambako kuna resources kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka niseme kama tunataka kujenga umoja wa Taifa, ni lazima tuhakikishe hizi rasilimali za nchi tunagawana haka kakeki ka Taifa. Sasa huko kwenye maendeleo ndiyo wanakopeleka maendeleo zaidi, kule ambako kumelala wanaacha, watatengeneza utabaka siku moja tutakulana nyama wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo ninachokusudia kusema kwenye Bunge hili, Mheshimiwa Waziri… (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe, kuna taarifa.
TAARIFA
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumpa taarifa kaka yangu, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam Mstaafu kwamba Daraja la Busisi ambalo limejengwa Mkoani Mwanza halitumiwi na watu wa Mwanza peke yake. Kwa siku kuna magari tisa yanakwenda Kigoma kutokea Mwanza yanapita kwenye daraja lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kilumbe, pokea taarifa na muda umekwisha, malizia.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unisaidie kunilindia muda. Hii taarifa siipokei kwa sababu imeendana tofauti na mchango wangu. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa, naomba umalizie mchango wako muda wako umeisha, malizia muda wako.
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nataka niliseme kwa ujumla kwamba, sisi na wananchi wetu wa Ziwa Tanganyika tunataka Serikali ifanye jambo hili kwa utulivu, hatulikatai maana tulifunga misitu ili miti iweze kukua na kufunga Ziwa tunakubaliana lakini tushirikishane vizuri zaidi katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)