Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia na mimi nichukue nafasi hii nikushukuru kwanza wewe Mwenyekiti kwa nafasi hii ambayo umenipa, pia nichukue nafasi hii nimpongeze Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa hotuba nzuri aliyoitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wewe ni rafiki yangu, umekuja Kigoma mara nyingi sana, Kigoma unaifahamu, hasa eneo la uvuvi. Kwenye eneo la Mifugo kwa kweli hujafanya vizuri. Wewe umekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi lakini umekuja kwenye Jimbo langu hasa kushughulikia kwenye eneo la uvuvi. Kwenye hilo naomba nikushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri naomba nizungumzie mambo mawili, kwanza kwenye eneo la mifugo. Eneo la mifugo Mheshimiwa Waziri ninakupongeza Waziri aliyekutangulia alikuja Wilaya ya Uvinza kutoa eneo kwenye Ranchi ya Taifa ili liweze kutumika kwa ajili ya wafugaji. Hilo ni jambo jema sana. Ni baada ya mimi kuja kuomba Bungeni hapa na Wizarani, Waziri aone namna ya kutenga eneo ambalo litasababisha wananchi wale ambao ng’ombe zao zinazagaa katika vijiji vyote 61 waweze kupeleka ng’ombe huko. Hili jambo nashukuru lakini Mheshimiwa Waziri utekelezaji kwa maana ya kuhamisha wale ng’ombe kwenye vijiji 61 haujafanyika.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja Kigoma kwenye ziara, alipoandamana na Naibu Waziri wako huyo Mheshimiwa Silinde ambapo naye ndiyo aliteuliwa kuingia kwenye Wizara hiyo akiwa Kigoma, nilimwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba naomba Naibu Waziri aje aweze kutatua huu mgogoro ahamishe kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa na Wilaya waweze kuweka mikakati mizuri ya kuondoa hizo ng’ombe katika vijiji hivyo ili wananchi wabaki salama wale wanaojishughulisha na kilimo, kwa sababu kilimo ndiyo uti wa mgongo lakini kilimo ndiyo kinachosaidia wananchi wetu wadogowadogo kwa ajili ya kujikimu na maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wale ng’ombe wanapoendelea kubakia kwenye vijiji, maana yake kwa kweli habari ya kilimo haipo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri unaona jinsi ambavyo unapingana na Wizara ya Kilimo. Sasa hili nakuomba, lakini ng’ombe wale wamezagaa kwenye misitu ya TFS kwa hiyo unapingana pia na Serikali kwa upande huo mwingine. Itakapohamishwa hiyo mifugo maana yake kule itabidi uweke miundombinu kwa ajili ya majosho ambapo kule vijijini hakuna josho hata moja. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri hilo ni la kwanza, naomba sana kwenye eneo hilo nadhani baada ya Bunge hili la bajeti nakuomba ama wewe ama Naibu Waziri aje kule Jimboni ili tuweze kufanya mikakati ya namna ambavyo tunaweza tukahamisha hiyo mifugo kupeleka kwenye eneo lililo rasmi, naamini Serikali itapata mapato kulikoni ambavyo ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine Mheshimiwa Waziri ni kwenye eneo hili ambalo limezungumzwa na Wabunge wenzangu kwenye eneo la samaki. Mheshimiwa Kilumbe ameongea vizuri sana, Mheshimiwa Aida amezungumza vizuri sana. Kwa kweli kwenye eneo hili Wabunge wa Mikoa mitatu ya Kigoma, Katavi, Sumbawanga, ndio ambao tuko kwenye ukanda wa hilo Ziwa Tanganyika, Mheshimiwa Waziri nataka nikuambie kwamba ziwa Tanganyika ndiyo chanzo kikuu cha mapato katika Mikoa hii mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hata hizi Halmashauri zetu zipo kwa sababu ya uvuvi, hakuna namna nyingine. Nataka nikuambie, nimekwenda kufanya ziara kwenye Kata mbili, Sigunga na Mgambo nilichokiambulia ni hiki. Kata ya Sigunga waliniambia Mheshimiwa Mbunge tunaomba kama Ziwa linakwenda kufungwa tuandalie makaburi, hatuna kazi nyingine ya kufanya, kazi yetu ni hapo ziwani. Sasa hebu niambie hiyo kauli ni nzuri kwa wananchi ambao ni wapiga kura? Nikasema siwezi kuwaandalia makaburi lakini Serikali lazima iwe makini namna ya kutekeleza hili jambo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kule kwenye Kata waliniambia kama Ziwa linakwenda kufungwa niwatafutie kazi nyingine ya kufanya.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nashon kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Askofu Gwajima.

TAARIFA

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa anayezungumza kwamba Ziwa Tanganyika linategemewa na nchi nne, sehemu kubwa ya Ziwa hili ipo Congo na mtaalam Waziri anafahamu kwamba samaki huwa wanahamahama katika kuzunguka zunguka. Ukifunga kwetu huku kule Congo wanaendelea kuvua. Utakuwa umefanya uamuzi wa kijinga wa kuisaidia nchi nyingine kile ambacho ungekipata wewe, kinatumiwa na nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zingine zote zitaendelea kuvua halafu wewe utaacha kuvua, wale watapata wewe utakuwa maskini. Kwa hiyo namjulisha mzungumzaji kwamba ni uamuzi usio wa kisayansi. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nashon taarifa unaipokea?

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo iko sahihi lakini nadhani haelewi ni kwamba hili Ziwa linafungwa kwa maana ya nchi zote hizo zinazozunguka eneo la Ziwa, lakini mimi nazungumzia upande wangu kwamba wananchi wa Kata ya Buhingu wanasema niwatafutie kazi nyingne ya kufanya, maana yake ni kwamba kazi yao wao ni hiyo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza kutokana na kwamba jambo hili halikuwa na ushirikishwaji, Wabunge wenyewe hatukuwa tumelijua, pamoja na kwamba wananchi wetu kule Majimboni walikuwa wanajua kwamba Wabunge tumeshazungumza hili huku Bungeni au tumekwisha zungumza na Waziri jambo hili, hatukuwa tumezungumza na Waziri jambo hili, nasi kama wananchi ambavyo walikuwa hawalijui nasi pia Wabunge tulikuwa hatulijui. Kwa hiyo, jambo ambalo linatakiwa hapa ni kuona namna ya kutushirikisha Wabunge, wadau wa uvuvi na wananchi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna haja ya kufanya siri ya jambo hili, Ziwa ni la wananchi na Ziwa ni la Serikali na wananchi lazima watii sheria za nchi Serikali ambazo zipo ni jambo la kawaida lakini lazima kuwe na ushirikishwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza ipo timu kubwa ya wavuvi ambao wako hapa Dodoma, wamekuja kukutana na Waziri na leo baadhi yao wataingia humu Bungeni wakati Waziri atakuwa ana-wind up watakuwa wanamsikia. Kwa hiyo, naomba jambo hili….

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Serikali ilichukulie kwa umakini sana na Wabunge hoja yetu siyo kukataa Serikali isifunge Ziwa, lakini hoja yetu ni kushirikishwa.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Ahsante, naunga mkono hoja.