Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi mchana huu nitoe mchango wangu kwenye mada iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoendelea kuuheshimisha Mkoa wa Lindi. Leo hii Mkoa wa Lindi tunataka kujengewa kituo kikubwa pale cha bandari ya uvuvi, lakini vilevile tuna kile kiwanda chetu cha LNG, kuna chuo kikubwa pale kinataka kujengwa na ndugu zetu wa Nishati. Kwa hiyo, kwa vyote hivi niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuutupia jicho Mkoa wetu wa Lindi ili na wenyewe uinuke kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu anasema usiposhukuru kwa kidogo basi huwezi kushukuru kwa kikubwa, na vilevile usipomshukuru mwanadamu mwenzio basi hata Mungu huwezi kumshukuru. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha mwaka uliopita 2022/2023 kujenga lambo pale kwenye Kata yetu ya Kimambi. Pamoja na kwamba lile lambo halijakidhi viwango kulingana na wingi wa mifugo waliopo kwenye Mkoa ule wa Lindi, nishukuru kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu turejee kwenye historia kwa nini ng’ombe wako Mkoa wa Lindi leo. Miaka ya 2012 kwenda 2014 baada ya kule Ihefu kuonekana kwamba wale wafugaji wanaharibu ekolojia, wakaja viongozi kutoka Serikalini kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara wakiomba nafasi lakini Mkoa wa Mtwara wakakataa, sisi Mkoa wa Lindi tukakubali, na Mkoa wa Lindi Wilaya ya Liwale ndiyo ilikubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Liwale tulitenga maeneo matatu kwenye Kata za Kimambi, Lilombe na Mlembwe kwenye Kijiji cha Ndapata. Lakini masharti yalikuwa kwamba kabla hao ng’ombe hawajaja miundombinu itangulie. Mpaka leo naongea hapa ndiyo lambo la kwanza limejengwa mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuliambiwa kwamba tutaletewa malambo na majosho kabla hawa ng’ombe hawajakanyaga kwenye ardhi ya Mkoa wa Lindi. Lakini leo tunazungumzia 2023 tuna lambo moja tu kwenye Kata ya Kimambi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale ukianzia Nangurukuru mpaka Liwale kote kumejaa wafugaji. Kwa mfano kama Wilaya ya Kilwa kuna Vijiji vya Zinga, Nangurukuru, Njinjo, Kipindimbi mpaka unafika Kimambi, kote kumejaa wafugaji. Lakini uone urefu wa kutoka Nangurukuru mpaka Liwale, kilometa 230, kuna lambo moja tu kwenye Kata ya Kimambi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiongea na wataalam wa ufugaji kule wanakwambia mahitaji yetu kwenye Wilaya ile ya Liwale tunahitaji kuwa na malambo matatu kwenye Kata ya Kimambi, lambo moja kwenye Kata ya Lilombe na lambo moja kwenye kata ya Ndapata. Kwa ujumla wake tunahitaji malambo saba ili tuweze kunufaika na watu wale wa Liwale nao wajione kama walikubali mifugo na wananufaika na mifugo hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa majosho hatuna josho hata moja. Ukiwauliza wataalamu wanakwambia tunahitaji majosho matatu, angalau kwenye kila kata tupate josho moja moja, kwenye zile kata ambazo zimekuwa zikipokea wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu angalia umbali uliopo kutoka Kimambi kwenda Ndapata, ni zaidi ya kilometa 222. Kutoka Lilombe kwenda Kimambi ni kilometa 111, hawa wafugaji wanatembeaje kufuata hili bwawa lililopo kule Kimambi? Uone umuhimu wa kuhitaji malambo kwenye ile wilaya yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa tumepokea mifugo tuna jambo lingine la minada. Tunao mnada mmoja lakini mpaka sasa hivi bado una kizungumzkuti cha bei. Tayari wafugaji wameanza kulalamika kwamba ng’ombe mmoja pale gharama yake sasa hivi imefikia 14,000. Kwa taarifa nilizozipata wanasema kodi ya pato pale ni 2,000; kuna kodi ya muuzaji ambayo ni 5,500; kodi ya mnunuzi ni 7,500. Ukipiga hesabu hapo unapata shilingi 14,500, bado wafugaji wanaendelea kulalamika na wananchi wanaendelea kulalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye hili; huo mwongozo wa bei kama uko uniform kwa minada yote nchi nzima basi tuuone, uwe wazi na wananchi wale waweze kuupata nao waendelee kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetokea mara nyingi sana mgongano kati ya wafugaji na wakulima. Mgongano ambao unatokana na kugombea maji kwa sababu mkulima anahitaji maji na mfugaji anahitaji maji. Lakini naomba kupata ufafanuzi mahusiano yaliyopo kati ya wafugaji na wanyamapori?

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nilizonazo ni kwamba maeneo yale ambayo tembo walikuwa wanaishi ndiko sasa hivi ng’ombe wanaishi huko. Matokeo yake sasa sisi wakulima tunaendelea kuhangaika na hawa wanaoitwa wanyamapori. Lakini hivi juzi baada ya neema kubwa kutangazwa TANAPA, Pori letu la Akiba la Selous likagawiwa likapatiwa eneo la TANAPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nikwambie kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji kwenye Vijiji vya Ndapata na Kimambi, leo yamechukuliwa na TANAPA. Matokeo yake wale wafugaji wamehama kutoka TANAPA wameachia lile eneo TANAPA wanakuja maeneo ya wakulima. Kwa hiyo, mgogoro wa wakulima na wafugaji unaendelea kushamiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana palitokea mauaji, mwaka huu pametokea kujeruhiana…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kuchauka, muda umekwisha.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tusimamie jambo hili tuone kwamba wakulima na wafugaji wanakaa kwa salama na amani. Baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)