Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma na mwingi wa ukarimu kwa kupata fursa kusimama mbele ya Bunge hili Tukufu na kutoa mchango wangu katika hoja hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu naomba pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu ya kunipa nafasi kuhudumu kama Waziri wa Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba nimshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na pia naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa uwezo na umahiri mkubwa mnaoonyesha katika kuliendesha Bunge letu.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nimshukuru Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Comrade Mheshimiwa David Ernest Silinde kwa kunipa ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Pia napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii, bajeti ya protein, bajeti ambayo imepata wachangiaji wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa hoja zilizowasilishwa hapa na kuchangiwa kwa vyema sana na michango mizuri sana ya kina yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara yangu.

Mheshimiwa Spika, mifugo na uvuvi ni utajiri. Kupitia michango mingi iliyotolewa na Wabunge, takribani Wabunge 54 waliochangia kwa maneno ya kuzungumza Bungeni na wachache waliochangia kwa kuandika inathibitisha juu ya ukubwa na umuhimu wa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha katika michango hiyo imedhihirika wazi umuhimu wa kuimarisha Wizara kupitia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayoongoza Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Sekta ya Uvuvi pia imepanga kutekeleza vipaumbele vinavyoendana na kufungamanisha uchumi wa buluu kwa kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi zinasimamiwa ipasavyo ili kuwa na uvuvi na ukuzaji viumbemaji endelevu, maendeleo ya viwanda, ukuaji wa kipato cha mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa kwa ujumla kwenye maji baridi na maji chumvi na kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mifugo ni dhahiri kuwa masuala ya kuendeleza malisho, ajira kwa vijana, mauzo nje ya nchi, utafiti wa mifugo ikiwa ni pamoja na kuendeleza kosafu bora za mifugo ni ya umuhimu katika kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa na nyama, mayai na ngozi, kuendana na mnyororo wa thamani na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwatambua Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa hoja mbalimbali kuhusu Wizara ambapo jumla ya Wabunge 54 kama nilivyokwisha kusema wametoa michango yao. Kuna waliotoa maoni yao kwa kuzungumza hapa Bungeni na wengine kwa maandishi. Naomba sasa wote hao niwatambue kama ambavyo watakavyokuwa wamesomwa katika risala yangu.

Mheshimiwa Spika, michango ya Waheshimiwa Wabunge niliowataja katika risala ilikuwa ni mizuri sana na iliyosheheni busara, hekima na changamoto. Aidha siyo rahisii kujibu kwa kina na kutosheleza hoja zote za Waheshimiwa Wabunge kwa muda huu mfupi nilionao hapa katika membari hii. Ninaahidi kwamba hoja zote tutazijibu kwa maandishi na kuwapatia Waheshimiwa Wabunge wote.

Mheshimiwa Spika, ushauri na maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo umezingatiwa. Hata hivyo ningependa nitumie muda mfupi nilionao kujaribu kutoa ufafanuzi katika baadhi ya hoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ziko hoja mahususi kadhaa zilizozungumzwa hapa. Nikianza na upande wa mifugo. Katika upande wa mifugo iko hoja iliyozungumzwa juu ya hereni. Serikali ilianza kulitekeleza zoezi hili kupitia Wizara ya Mifugo na Uvivu na baada ya utekelezaji iligundulika kwamba yako makosa ambayo tuliyatekeleza kwa wakati ule. Na kwa hekima na busara za viongozi wetu wakaitaka wizara irejee, ifanye tathmini ijiridhishe kama ushirikishwaji umefanywa sawasawa; tuangalie juu ya bei, juu ya ubora wa bidhaa zile.

Mheshimiwa Spika, kazi hii sasa tumekwishakufika mwisho; kwa maana ya kwamba tumepata yale yote ambayo Serikali imeelekeza, kwa maana uongozi wetu umeelekeza maana maelekezo haya yalitolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Bunge hili Tukufu. Baada ya kutoa maelekezo yale Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilichukua hatua sawa na maelekezo yale. Na hapa, ingawa kule mbele nitaendelea pia, nataka nieleweshe, maana yupo mmoja katika wachangiaji, Mheshimiwa Luaga Mpina, amezungumza kuwa maelekezo yanayotolewa na viongozi wetu, akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu, na amemtaja haswa yeye mahususi, kwamba hayafanyiwi kazi. Kufanyiwa kazi kwa jambo hili la hereni, kwa maana ya tathmini na kujiridhisha juu ya bei na juu ya uwezo wa zile hereni zenyewe ni moja ya ushahidi wa kwamba viongozi wanapoelekeza hufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nitakuja hapa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, ya kwamba katika mkakati wetu wa utekelezaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, la kwanza kwenye kwenda kuitekeleza sheria hii kwenye bajeti hii tuligundua kwamba tuna jukumu la kuwashirikisha ipasavyo Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine wote. Ninawaombeni kwa heshima kubwa na taathima tukubaliane ya kwamba leo tupitishe bajeti hii kisha tuanze engagement kati ya Wizara na ninyi viongozi. N mawazo yenu yote tutayachukua kwenda kuboresha zoezi hili. Nataka niwahakikishie litakwenda kuwa zoezi zuri sana litakalokwenda kuinua uchumi wa wafugaji, uchumi wa Taifa letu na mchango chanya wa hili Taifa. Msiwe na wasiwasi wowote, sisi ni watu wasikivu na ni watu ambao tuko tayari kushirikiana nanyi Wabunge wetu ipasavyo kabisa.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine mahususi ambayo ningependa kuzungumza hapa ni hoja ya malisho. Nimesema katika bajeti ya kwamba tumetenga fedha za kuhakikisha mashamba yanayomilikiwa na Serikali ambayo yaliyojaa nchi nzima na kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni mapori, na Waheshimiwa Wabunge mmesema hapa. Nataka niwahakikishieni ya kwamba moja ya jukumu kubwa tutakalokwenda kufanya ni kuyafanya mashamba yale yawe ni mashamba ya uwekezaji na uzalishaji ili yaweze kuwa na tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, tunazo njia mbili kubwa za kufanya, njia ya kwanza ni kwa kutumia fedha zetu wenyewe ambazo tumeziweka katika bajeti na njia ya pili tutafungua milango ya uwekezaji. Nilishasema katika Bunge ikiwa wewe Mbunge, ikiwa unaye mwekezaji yeyote mlete Wizarani atuambie andiko lake, alete business plan yake, alete mpango wake sisi tuko tayari kutoa ushirikiano tuzalishe.

Mheshimiwa Spika, mathalani kule Ruvuma tumechagua ni eneo la uzalishaji wa mahindi aina ya mahindi ya njano (yellow corns). Kwa muda mrefu sasa mifugo kama vile wazalishaji wa kuku wamekuwa wakihangaika; inapofika kipindi cha kiangazi huwa wanapata tabu sana namna ya kupata mahindi. Mimi na wenzangu wizarani tumeshauriana na tumekubaliana mashamba ya upande wa kule tuliyonayo pale Hanga, Ngadinda na kwingineko, Songea kule tunakwenda kuzalisha yellow corns. Yellow corns hii itakwenda kwa ajili ya kutengeneza uhakika wa chakula cha kuku na mifugo mengine. Kwa hivyo niwahakikishieni jambo hili tunakwenda kulifanya; na kwa mara ya kwanza Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumetengeneza mpango wa kwamba sio kwa kutegemea mvua tena, tunakwenda kufanya mechanization tunakwenda kumwagilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunafikiria kwamba hata nyasi imwagiliwe, sio mahindi tu na mpunga hata nyasi tuzimwagilie, hayo ndio mawazo tuliyonayo. Mmoja katika ya Waheshimiwa Wabunge humu amesema kwamba kwanza tosheleza chakula cha ng’ombe wako hapa nyumbani.; ni ukweli tutatosheleza chakula cha hapa nyumbani. Lakini niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sitaki kusema maneno mengi; angalia leo hii chakula cha mifugo inayolishwa kule Asia kwa kiasi kikubwa sana ilikuwa inatoka Sudan na jirani zetu wa Kenya.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, kama hatutaweza kutumia tena fursa hii sisi Watanzania leo haitatokea tena wakati mwingine. Kila mmoja hapa anajua matatizo yanayowapata majirani zetu, hii kwetu sisi ni fursa. Wamekuja, mimi nimempokea hapa Waziri wa Kilimo wa kutoka Saudia nimekaa naye, walikuwa wanachukua nyasi kutoka Sudan, moto unaowaka kule sitaki kusema kwa nguvu sana hapa Bungeni. Hiyo kwetu ni fursa tutapata forex, tutapata fedha za kigeni tutatumia hiyo kama ni ajira ya watu wetu. Kwa hivyo ni ukweli kwamba ng’ombe wetu hapa nyumbani huwa wanahainga. Nilisema, kwamba tunataka tuone gari zinatoka sehemu moja zinakwenda sehemu nyingine zikiwa zimebeba nyasi. Kama vile ambavyo tunatoa mahidni kutoka sehemu moja kupeleka kwa wahitaji na ndivyo hivyo tunataka tufike katika hatua ya kuchukua nyasi kupeleka Kiteto, Simanjiro ili ile mifugo ya kule Lungido iweze kuokolewa. Ndugu zangu inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilikwenda Simanjiro na Comrade Ole-Sendeka, na nilikwenda Kiteto na rafiki yangu Comrade Olelekaita, niliwashuhudia ng’ombe wakati wa ukame mkali wakinyweshwa uji, yes, ndiyo, kwa ajili ya kutafuta survival. Na sisi binadamu tumekuwa tukijinusuru kwa kupelekeana mahindi ya nafuu. Nasema hivi tunakwenda sasa katika mechanization tutazalisha majani ya kutosha kama tunajihami tutawahami na mifugo yetu pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa jambo la vaccination hapa, kwa maana ya chanjo. Chanjo ni muhimu sana. Ili tuuze ng’ombe wetu vizuri chanjo na herein, kwa maana ya kuitambua mifugo yetu ni jambo la muhimu. Yuko ndugu yangu mmoja pale Mwanza anaitwa Chobo; alikuwa anauza nyama kule UAE; Chobo amekataliwa kuuza nyama Uarabuni hivi sasa, hauzi tena. Kiwanda kiko kizuri sana pale ni kwa sababu ya vitu hivi. Sisi tumedhamiria, kabla hatujakwenda huko nitakaa na Waheshimiwa Wabunge wote, kila mmoja anajua ana hoja yake, kwa nini anasema isiwe hereni, milango yangu iko wazi. Tutahakikisha tunakaa tunakubaliana, tutakwenda na campaigns za uhakika ambazo hazitatuletea taharuki ya namna yoyote.

Mheshimiwa Spika, nataka tutoke katika kuuza tani 12,000. Kwa nini sisi tuzalishe nyama tani 800,000 zinatutosheleza humu nyumbani, kwa nini hatuuzi tani 100,000 nje ya Taifa letu wakati uwezo wa kuuza na masoko yako makubwa sana? Ndugu zangu kupanga ni kuchagua, tunapata tupate forex, tupate ajira za watu wetu, tupate uchumi mkubwa. Yako mambo ni lazima tuyafanye ili kusudi tukubaliane hii mifugo yetu iweze kutunufaisha na inufaishe Taifa letu. Hii GDP inayochangiwa hivi sasa kwa asilimia nane ninawahakikishieni kama kuna nafasi nzuri na rahisi ya kuinua ni katika mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Mungu Mkubwa sana Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatutengenezea njia rahisi sana kwa diplomasia kubwa sana ya uchumi. Wanenepeshaji wa ng’ombe, wale wa mbuzi, wale wa kondoo na wengine tukae mkao wa utayari. Nataka niwahakikishieni hatutakwenda katika zoezi lolote baada ya bajeti hapa, tunatengeneza engagement plan na implementation plan ya uhakika. Waheshimiwa Wabunge wote msiwe na wasiwasi. Wale mliokuwa mnakusudia kuchukua shilingi yangu kwenye jambo hili naomba kabisa kwa uhakika wala msiwe na wasiwasi huo, manake tutakaa na mambo yatakuwa mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya tatu, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia kuhusiana na wakala, na hii inahusiana na miundombinu ya mifugo kila Mbunge anataka josho, kila Mheshimiwa Mbunge anataka rambo, kisima kirefu cha maji, kila Mbunge angependa awe na bwawa la mifugo na akitazama anaiona bajeti ya Waziri wa Mifugo imetengeza marambo manane tu kwa mwaka. Way forward mmeitoa ninyi wenyewe, mmesema hapa, na nimewasikieni, kuanzia kwenye kamati ya Bunge iliyowasilisha hapa na kuja kwa Mheshimiwa Mbunge mmoja mmoja mmesema hapa. Kwamba Wizara inasimamia miradi kutokea Dodoma. Bwawa linajengwa Kiteto kwa Mheshimiwa Olelekaita, bwawa linajengwa kule Simanjiro, bwawa linajengwa kule Longido, bwawa linajengwa kule Mkuranga ndani Mkurugenzi yuko pale Dodoma peke yake na engineer wayasimamie yale.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamesema, kwamba, hapa tunalo jambo la kufanya, na katika jambo la kufanya mnadhani ya kwamba tutengeneze wakala. Waheshimiwa Wabunge, wafugaji wenzangu nataka niwakumbusheleo hapa, kwa ufupi sana. Watu wa kilimo kupitia Tume ya Umwagiliaji wamepata fedha nyingi sana ninyi, nyote ni mashahidi na mmepitisha nyie wenyewe hapa. Zile schemes za umwagiliaji wakulima watakaokuwa wanatumia watakuwa wanachangia nadhani tunaelewana hapo. Sisi binadamu, nimetoa mifano ya RUWASA, yale maji tunayoyatumia sisi tunachangia. Ninafahamu, ndiyo maana mkasema tupate wakala. Ninawajua wafugaji, nimekaa nao miaka kadhaa sasa, wako tayari kuchangia lakini katika mambo ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, hoja hii inatosheleza kuwaambieni ya kwamba tunalichukua jambo hili ndani ya Serikali tunakwenda kulianzishia harakati zake. Tutali-fast track tukipata baraka Inshallah Ta’ala jambo litakuja litapita lita-solve matatizo ya watu wote hapa. Ninyi leo kazi yenu ni nyepesi sana tu, nakuombeni kwa heshima kubwa na taathima tena kwa mara nyingine nipitishieni muone mchakamchaka utakaopigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende katika uvuvi; limesemwa jambo kwa mapana na marefu sana hapa juu Lake Tanganyika. Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma, Rukwa; narudia tena; limesemwa jambo la Lake Tanganyika kufungwa. Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma, Katavi na Rukwa wamesema kwa mapana sana na wananchi wamewasikia, na mimi na wenzangu Serikalini tumewasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba itifaki hii ilisainiwa ipo ndani ya Serikali, ilikuwa na lengo jema; lakini itifaki hii haikutulazimisha sisi nchi wanachama ya kwamba namna ya utekelezaji wa ile itifaki ufanane, haikuwa hivyo. sisi hapa katika Ziwa Tanganyika tuna kitu kinaitwa kilimia; mmoja miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge amesema hapa. Kilimia, najua Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, Mheshimiwa Aida Khenani, Mheshimiwa Bindyaguze, na Waheshimiwa Wabunge wengine wanafahamu vizuri. Kilimia lile ziwa huwa linajifunga lenyewe automatically, hasa kipindi hiki cha baridi. Nimefurahi kwamba Waheshimiwa Wabunge kutoka mikoa hii mmewaleta wapiga kura, wavuvi wenyewe. Ndugu zangu hakuna sababu yoyote ya kupata taharuki.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge nataka niwahakikishieni, kama ambavyo tumewaandalia mkutano kesho; ninafahamu tuna mkutano na wakuu wa mikoa hiyo yote, Waheshimiwa Wabunge wote, wakuu wa wilaya zote, wakurugenzi wote, kwa kuwa hoja ni ushirikishwaji. Wabunge neno hili la ushirikishwaji tunakwenda kulikamilisha kesho pale St, Gasper, tunakaa tunajadili. Kwa hiyo hakuna hofu, wala hakuna mtu yoyote apate wasiwasi ya kwamba labda kuna jambo linalohusu kufungwa kwa ziwa. Niwahakikishieni, narudia tena, issue si ni kushirikisha? basi nataka niwaambie mimi kwa heshima kubwa na taadhima na wenzangu kule Serikalini, hakuna jambo tunaloliheshimu kama kuwaheshimu watu ninyi mliopigiwa kura na wananchi. Wanasema sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kilumbe na Waheshimiwa wote, Mheshimiwa Bidyanguze, Mheshimiwa Aida, Mheshimiwa Kavejuru, Mheshimiwa Sylivia, Mheshimiwa Ndalichako, Mheshimiwa Kandege, Mheshimiwa Kakoso na Waheshimiwa Wabunge wote niwaondoe hofu. Waambieni wana-Tanganyika wavuvi wa Ziwa Tanganyika waendelee na shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Daktari Samia Suluhu Hassan kama mnaona jambo kubwa Mheshimiwa Rais wakati wote amekuwa akilisisitiza kwetu sisi wasaidizi wake ni kutokuleta taharuki. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan Amejenga msingi imara wa zile “R” nne, kila mmoja anazijua hapa. Ikiwa yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua milango anakaa na kila mtu, anazungumza naye, anapata kufanya reconciliation hata; yale watu tuliodhani kuwa ni magumu kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan yamekuwa ni mepesi. Sasa mimi Abdallah Ulega ni nani nisijifunze? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hakika nataka niwaondoeni hofu juu ya jambo hili ndugu zangu. Tunazo njia nzuri sana za kuendea mambo, msiwe na wasiwasi na wavuvi msiwe na wasiwasi, wakati wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni wakati wa uzalishaji, ni wakati wa kukuza uchumi wetu na hakuna sababu nyingine ya kubabaika. Mifugo na uvuvi ni utajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia juu ya mamlaka ya uvuvi ninawaelewa, na Kamati ya Bunge imetuelekeza juu ya jambo hili. Niwakumbushe; katika Sera ya Uvuvi ya Mwaka 2016 jambo hili limetamkwa, na sisi Serikalini tumelichukua. Tumelichukua kwa sababu tumekuwa tukifanya kila mara operations. Ninyi wote hapa mmesema, kila Waziri anayeingia katika Wizara hii anafanya operation. Tunachoma nyavu, tunafanya vile lakini inaonekana inakosekana ile sustainability, uendelevu unakosekana.

Mheshimiwa Spika, sayansi ya uvuvi inataka tulinde maeneo ya mazalia na makulia ya samaki na ndiyo maana Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 43(f) ikatuelekeza Serikali wazi wazi, kwamba tuhakikishe tunalinda maeneo ya mazalia na makulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la mamlaka Mwenyezi Mungu akitujalia insha Allah litakwenda kuwa ni mwarobaini mzuri sana. Kwa hivyo kusudio hili tumeanza kuchukua maoni ya Waheshimiwa Wabunge na tutaendelea sisi, tutapitisha katika vikao vyetu vyote vya kiwadau, tutaona linalowezekana kufanyika. Hili unajua automatically linakwenda kuondoa hizo hofu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukishakuwa umelinda maeneo ya mazalia na makulia una uzalishaji mzuri, kuanzia baharini kule katika matumbawe kuja huku katika Maziwa na mpaka Nyumba ya Mungu, Hale mpaka Jipe, yote hayo yanaingia mle, hapa mambo mbona yatakuwa mazuri sana na uzalishaji utakuwa ni mzuri sana. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wasiwe na wasiwasi wavuvi wenzangu juu ya jambo hili, kwani tumelichukua na tutalipa uzito na tutaona kusudio hili linawezaje kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo mengi ya kusema, lakini haya ndiyo yaliyokuwa mazito. Mengine nitayajibu kwa maandishi. Nataka nimalizie nisichukue dakika zako nyingi. Kwa kuwa nimezungumza juu ya mundombinu ya mifugo na nia yetu kama Serikali, najua wako watu wangependa kuzungumzia minada, wengine wangependa kuzungumzia magomvi kati ya wakulima na wafugaji yaliyosababishwa na mambo ya maji ukosefu wa mabwawa, nafahamu. Najua pia wako watu wangependa kuzungumzia malisho, nimeyasema hapa naomba watuunge mkono ili tukapunguze kero hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua sayansi ya kuondoa hii migogoro ya wakulima na wafugaji, naiona ni nyepesi tushikamane, tutaiondoa, watu waishi kwa amani. Leo najua njia za mifugo huko Wilayani kote njia za mifugo zinajulikana. Kama zinajulikana kupita mle katika zile njia za mifugo kama tunafanikiwa kwenda kutengeneza chombo ambacho kitakuwa kikisimamia ile miundombinu ya mifugo na wafugaji ambao wako tayari tukaenda tukashirikiana nao vizuri, wakawa wanachangia vizuri, sasa ugomvi utatokea wapi? Kama mtu anatafuta maji? Maji si ndiyo haya hapa, kama mtu anatafuta malisho, malisho si ndiyo haya hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafahamu kwamba hata kaka yangu Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa Mstaafu wa zamani Mheshimiwa Innocent Kalogeris angetamani aishike tena leo shilingi kama alivyofanya mwaka jana, lakini asiwe na wasiwasi, mawazo hayo na fikra hizi zilizotolewa hapa zinatosheleza kabisa kujenga msimamo wa kwamba tunakwenda pazuri.

Mheshimiwa Spika, najua hata rafiki yangu Mgosi Wandima, Mheshimiwa Reuben, angetamani ashike shilingi kwa ajili ya mnada wake pale Handeni Mjini. Kaka suluhisho ni hili hapa, tushikamane hakuna hoja tena. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mwisho, naomba nimalizie kwa maneno yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumza hapa mtani wangu Mheshimiwa Luhaga Mpina juu ya hoja mbili; unajua nilikuwa sitaki kusema, lakini sasa ametaja majina ya wakubwa, nataka nimfafanulie baadhi ya mambo. Hoja ya kwanza kwa sababu amemtaja mpaka Rais ya Awamu ya Tano ile ya kuchoma moto vifaranga. Unajua hizi sheria zinatekelezwa halafu katika utekelezaji wa sheria yako mambo ya busara na hekima, namna ya kufanya vile vitu. Sheria inasema tu–destroy kwamba mtu kama amekosea akaingiza vifaranga unatakiwa ku–destroy, namna ya ile destruction, sheria haikusema uchome moto, uwachimbie katika shimo, uwafanyaje sheria haikusema hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ugomvi wa pale ulikuwa ni nini? Ni kwa nini vifaranga vichomwe mbele ya macho ya watu? Namshukuru amezungumzia juu ya animal welfare (haki ya wanyama), angalia mgongano wa mambo hapo, aliyekosea ni nani? Aliyekosea ni mwingizaji wa vifaranga au vilivyokosea ni vile vifaranga? Sasa kwa nini uvichome moto mbele za watu? Simple, kwa hivyo hapa issue inawezekana vinachomwa moto kila siku huko, yawezekana kabisa, lakini kwa nini unavichoma moto mbele za watu? Hii ndiyo hoja.

Mheshimiwa Spika, binadamu wameumbwa siyo mnyama, siyo hayawani, binadamu siyo hayawani, viumbe vile vina haki yake na namshukuru amezungumza vizuri wakati alipokuwa akitetea ng’ombe ambao ni kweli Kanuni ile tumeisaini ya kuilinda haki za Wanyama. Sasa haki za wanyama ni pamoja na kutokuwachoma hadharani. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pilli la samaki. Anataka mimi niseme, unajua Mpina mimi nakuheshimu sasa siwezi kusema kila kitu wewe ulikuwa bosi wangu pale Wizarani. Sasa mimi niseme ukweli, mimi ni muungwana, msema ukweli ni mpenzi wa Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo na yeye anajua tumekaa vizuri sana, mimi na yeye pale wakati niko katika winding up pale Wizarani kwa namna ambavyo namheshimu, kwanza jana nilimpigia simu Mheshimiwa Mashimba Ndaki, kumuuliza bwana, kesho tunakwenda katika hoja, nimeliona jina lako, vipi Mzee unataka kuchangia? Akaniambia Mheshimiwa Waziri, sina haja ya kuchangia bwana. Akaniambia kwamba yeye atachangia kwenye kilimo, nikamwambia bwana mimi nakutakia kila la kheri kwa sababu nilitaka nijue anataka kuchangia kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa leo nikiwa na watendaji pale Wizarani, Mheshimiwa Luhaga Mpina, nilimpigia simu niseme ukweli na msema ukweli mpenzi wa Mungu na namfurahia amewataja watendaji wengi wa Wizara ambao na mimi nilikuwa nao pale Wizarani. Sasa hivi kama saa moja tu iliyopita, nikamuuliza bwana mzee nimeona jina lako unataka kuchangia, una jambo lolote nikusaidie? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, akaniambia, hapana bwana. Mimi ni kweli naenda kuchangia, nikamuuliza kuna kheri shehe? Akaniambia ipo kheri kubwa sana wala usiwe na wasiwasi. Sasa simkatalii yeye kuchangia hapa Bungeni kwa kuwa ni haki yake, lakini nataka nimkumbushe ananiambia kwa nini sisemi juu ya rula ilivyotumika pale kantini? Sasa Mheshimiwa Mpina wakati mwingine tunakaa kimya, maana kukaa kimya nako ni busara. Samaki yule akishapikwa anapoteza shepu, anapoteza size, sayansi ya samaki haielekei huko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, samaki yule aliyempima hapa Bosi wangu wa zamani Mheshimiwa Mpina, alikaangwa, kapita katika nyuzi joto nyingi sana. Kwa hivyo ameshapoteza ile hali yake, yaani ile physical appearance yake imepotea kabisa, huwezi kupata uhalisia. Sasa alitaka mimi wakati ule nikiwa Naibu nimwambie Mzee unakosea hapo. Katika hali ya kawaida na nadhani kwa kuwa sikumwambia hivyo wakati ule sikupishana naye, sikugombana naye, ndiyo maana mimi Abdallah Ulega hadi hii leo nipo katika podium hapa kama Waziri. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, mantiki yake ni nini? Mantiki yake ni kwamba, kama ningeligombana nae wakati ule ningeliambiwa mimi ni mkosefu, sina adabu, ni mjeuri, unagombana na bosi wako, labda saa hizi nisingekuwa mahali hapa. Itoshe kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge kwa heshima kubwa na taadhima nawashukuruni sana, ameondoka mke wangu Mama Tulia hapa na furaha kubwa sana kwa sababu amesikia michango mizuri ya pongezi, matumaini, shukurani na kunitakia kheri katika kutekeleza jukumu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaahidi kwamba kazi imeanza. Mtafurahi yaani show show vijana wa mjini wanasema, naombeni uungaji mkono wenu hata wale kama nilivyokwishasema waliokuwa wanafikiria kushika shilingi vinginevyo iwe nje ya hoja hizi, lakini naomba waniamini, ninaye Naibu Waziri mzuri sana, comrade Silinde. Mheshimiwa Silinde alikuwa akiniheshimu sana toka tukiwa wote Manaibu Waziri hapa sana. Leo hata mimi najua nilipoteuliwa na yeye kuwa Naibu wangu nilijiuliza hee! Hii nchi kweli inaona. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, niruhusu nimalizie hizi dakika zangu mbili niwaambie Waheshimiwa Wabunge kidogo; katika Naibu Mawaziri sisi wakati ule nikiwa Naibu Waziri, tuna utamaduni wetu, kila mahali mnapokuwa wawili, watatu anapatikana kiongozi. Sasa tukakaa Manaibu Waziri tukaulizana nani anakuwa Mwenyekiti wetu? Mheshimiwa Silinde akanyoosha mkono wa kwanza, wote tukiwa Manaibu, akasema ahaa jamani hilo nalo la kuulizana, Mwenyekiti hapa si Abdallah Ulega bwana Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Hiyo nawaonyesha namna ambavyo toka huko nyuma tumekuwa tukishirikiana na kuheshimiana sana. Kwa hivyo, nawapa matumaini, ninaye Profesa Riziki Shemdoe, wote wanamfahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huyu jamaa Profesa Riziki Shemdoe, ni Mgosi Wandima, kule kwa Lushoto kuna kitu kinaitwa Muku, wanajua Wasambaa hapa. Muku wanakula watu wa kazi, akila hiyo hachoki kufanya kazi, ndiyo huyu jamaa. Kwa hiyo saa nane ya usiku nikimpigia simu anaitika simu yangu, nikimwandikia meseji yuko hewani. Nataka niwahakikishie, sasa kuna maneno hapa naogopa kuyasema, nikiyasema itakuwa hatari, lakini kwa mchanganyiko huu jinsi ulivyo mzuri ni kama ile timu iliyoingia nusu fainali juzi hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, basi, kwa kuwa naomba nisishikiwe shilingi, niseme tu kwamba ni kama zile timu mbili ambazo zimefanya vizuri sana hapa juzi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.