Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja hii ambayo iko mezani na kwa kuanza ningependa nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha kwamba sekta hii ya Uwekezaji Viwanda na Bashara inaleta tija katika Taifa letu, lakini kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo Wizara inafanya, lakini pia niwapongeze watendaji wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo inafanyika schini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kipekee kwa sababu, wasilisho la Mheshimiwa Waziri limeonesha namna ambavyo Mheshimiwa Rais amefungua fursa za ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Waziri imetuambia kuanzia Julai, 2022 mpaka mwezi huu Machi, 2023 takribani ajira 81,8200 zimezalishwa katika sekta za miradi ya kimkakati na uwekezaji kwa kweli ni jambo ambalo linatia faraja sana kwa sababu wote tunafahamu changamoto ya ajira kwa vijana wetu. Kwa hiyo, kipekee sana nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo tumeahidi ajira kwa vijana ifikapo 2025 inatekelezwa kwa kasi na kwa weledi mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kujikita kuchangia kuhusiana na programu za ubunifu ambazo Mheshimiwa Waziri ameziongea kwanza niipongeze Wizara kwa hatua ambazo inafanya katika kuhakikisha kuwa ajira kwa vijana zinapatikana na Mheshimiwa Waziri ameeleza hapa namna ambavyo Wizara inawekeza katika programu za ubunifu za vijana ikiwemo kuatamia wabunifu vijana. Ameeleza hapa katika mwaka wa fedha uliopita waliwatmia vijana wabunifu 27 na kufikia Machi mwaka huu wamewatamia vijana watano.

Mheshimiwa Spika, ameeleza hapa, kwamba katika mwaka wa fedha uliopita waliatamia vijana wabunifu 27 na kufikia Machi mwaka huu wameatamia vijana watano. Niipongeze Wizara, lakini nimshauri Mheshimiwa Waziri, jitihada hizi hazijitoshelezi kulingana na maendeleo ya teknolojia ambayo tunayo, lakini vilevile kutokana na fursa ambazo vijana wanazihitaji programu hizi bado ni ndogo sana. Na sio kwamba, tunailaumu Wizara kwamba, haifanyi kwa kadiri ya ambavyo inatakiwa kufanya, mimi naamini Wizara hii ilitakiwa kufanya zaidi ya haya ambayo yanafanywa.

Mheshimiwa Spika, programu za ubunifu katika Taifa hili zinafanywa na kila Wizara, lakini hatuna uratibu ambao unaonesha ni programu ngapi zinafanya biashara na ambazo zimekuwa stahimilivu kwenye soko la biashara; na hii ndiyo Wizara ambayo ina jukumu la masuala yote ya kibiashara. Kwa hiyo mimi nilitegemea pamoja na kwamba Wizara inatuonesha program ambazo wao wanazifanya, walitakiwa kutuonesha uratibu wanaoufanya kwenye programu za ubunifu katika Wizara zote, na watuoneshe ni programu ngapi za vijana zinafanya biashara na zimechangia ajira kwa kiasi gani, ndiyo kazi ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunapoendelea mbele, mimi nafahamu kwa mfano COSTECH ambayo iko chini ya Wizara ya Elimu wameingia mkataba na CRDB hapa juzi kwa ajili ya kuwawezesha vijana kwenye programu za ubunifu. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pia inafanya programu hizo, Wizara ya Kilimo na Wizara nyingi sana, lakini Wizara hii itusaidie kufanya uratibu ili tuweze kujua programu gani za ubunifu zinastahimili kwenye soko la ajira na soko la kibiashara.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu sana kwa sababu, hapa tumesema ajira ambazo zinaratibiwa, ndizo hizi ambazo zimeripotiwa. Ajira hizi ambazo wanazalisha vija awenyewe ni muhimu sana kwa sababu tunakoelekea kila siku tunasema teknolojia ndiyo ambayo inaajiri vijana wengi zaidi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atusaidie ili tuhakikishe kwamba vijana hawa ambao wanaweka jitihada kubwa sana katika programu zao za ubunifu Serikali inawa-support na wanaratibiwe vizuri. Pale ambapo uratibu ukifanyika changamoto zikitokea ni rahisi sana kwa Wizara husika kuelekeza sekta inayohusika kuwasaidia vijana hawa ili wasiweze kudondoka katika soko la kibiashara.

Mheshimiwa Spika, naomba niongee kidogo pia kuhusiana na suala ambalo limezungumziwa hapa awali. Sisi kama Taifa wote tunafahamu, kwamba shughuli zote zinazohusisha utawala wa Taifa letu lazima ziongozwe na Katiba, Sheria, taratibu na kanuni ambazo tumejiwekea sisi wenyewe. Ibara ya 97 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalipa Bunge hili jukumu la kutunga sheria, lakini Katiba hiyohiyo inaipa Mahakama jukumu la kusimamia haki; na Kikatiba ndio taasisi ya mwisho ambayo inasimamia haki katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliane; katika kutekeleza miongozo na shughuli ambazo zinaleta tija ya maendeleo katika Taifa letu ni busara na weledi mkubwa kwamba, taratibu na kanuni ambazo tumejiwekea sisi wenyewe na sheria ambazo Bunge hili limezitunga ni lazima zizingatiwe. Sheria yetu ya Ushindani inasema wazi kabisa; nasema hivi kwa sababu, tukicheza tusifuate wenyewe sheria ambazo tumejiwekea tutakuwa hatuendi katika mwenendo ambao ni sahihi; sheria ya ushindani inasema wazi kabisa kwamba kwenye makubaliano yoyote ambayo yanachagiza kuathiri soko ama yanachagiza kuathiri soko kwa maana ya ushindani, makubaliano yote ambayo yanajikita kwenye kuharibu ushindani ni makubaliano ambayo hayakubaliki kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sheria ambayo tulitunga sisi wenyewe ya ushindani, kifungu cha nane kifungu pia cha 5 kinatuambia wazi namna ya makubaliano ambayo yanakubalika katika soko letu la ushindani. Kifungu hicho kinasema kwamba makubaliano ambayo yanakubalika ni yale ambayo, moja, yanakuwa makubaliano ambayo hayazidi utawala wa soko kwa asilimia 35, lakini makubaliano haya ambayo sheria inatambua ni yale makubaliano ambayo yanalinda walaji dhidi ya soko la ushindani.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa issue ni kufuata sheria na taratibu. Hakuna mwekezaji yeyote anayekatazwa kununua hisa za kampuni yoyote, issue kubwa ni kwamba taratibu ambazo tumejiwekea ni lazima zifuatwe.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu sababu ya sheria kuweka taratibu hizi, moja, ni lazima tudhibiti soko dhidi ya ushindani, lakini pili, lazima tuhakikishe walaji wanapata bidhaa kwenye soko, na tatu, bidhaa lazima ziwe stahimilivu kwenye soko. Sasa tusipohakikisha kwamba taratibu hizi zinafuatwa inakuwa ni jambo ambalo kwa kweli linaleta maswali mengi sana. Lakini mategemeo yetu yalikuwa ni kwamba, taasisi ambazo tumezikasimu madaraka haya ya kusimamia taratibu hizi zinafanya mambo hayo kwa weledi mkubwa sana, ili kuepuka hii tafaruku ambayo tunayo sasahivi.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme yafuatayo; wakati hii Kampuni ya Scancem inataka kununua hizi shares za AfriSam Mauritius ni jambo ambalo ni la heri, lakini mgogoro umeanzia kwenye kujiridhisha kama hawa wawili wakiwekwa kwa pamoja wanazidi utawala wa soko kwa asilimia 35. FCC wenyewe wamefanya tafiti na wana data za kuonesha kuwa hizi kampuni mbili zikiungana kwa pamoja zitasababisha utawala wa soko kwa zaidi ya asilimia 35.

Mheshimiwa Spika, na ningependa nitoe mfano; kigezo kikubwa ambacho Mahakama imetuongoza tukifuate ni kigezo cha utawala wa soko, kwamba ni nani anayeuza zaidi.

Ukiangalia takwimu za FCC ukiunganisha hizi kampuni mbili, Twiga Cement na Tanga Cement, kwa pamoja zitauza asilimia 52 katika soko. Lakini pia takwimu zinatuonesha, kwamba katika uuzaji, katika kanda tano kubwa, kanda nne zitatawaliwa na hizi kampuni mbili. Kwa mfano, Kaskazini watauza kwa asilimia 92, Kanda ya Ziwa asilimia 77, Pwani asilimia 60. Kanda ya Kati asilimia 49 ni Kanda ya Kusini tu pekee ambayo imeachwa kwa sababu, soko lake liko dominated na Dangote.

Mheshimiwa Spika, sasa kama sisi wenyewe, sheria tunazitunga wenyewe, takwimu tunafanya wenyewe na tunazo sisi wenyewe, ni kwa nini tunakwenda kinyume na taratibu ambazo sisi wenyewe tumejiwekea?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hapa hakuna mtu anayekatazwa kununua hisa, tunachoshauri, taratibu zifuatwe. Kama Scancem hisa zake zinaonekana zimezidi…

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, kuna Taarifa kutoka kwa mtoa hoja.

TAARIFA

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nampongeza mchangiaji anavyochangia. Naomba tu kumpa taarifa kwenye eneo la kwamba, kanda nyingi zitakuwa zinahudumiwa na kampuni hizi mbili.

Mheshimiwa Spika, uuzaji wa saruji kwenye nchi hii hauuzwi kikanda. Ukienda Kagera utakutana na Dangote, ukienda Tanga utakutana na Dangote, ukienda Mtwara utakutana na Dangote. Kwa hiyo, Tanzania nzima inauziwa saruji na kampuni zote 14. Kwa hiyo, hiyo hoja ya mwanzo ya analysis tutaijibu badaye, lakini nilitaka tu kumpa hiyo, soko la Tanzania halijagawanywa kikanda. Ahsante sana.

SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, siipokei kwa sababu Mheshimiwa Waziri hajanielewa. Hii sio ripoti yangu mimi, ni ripoti ya Tume ya Ushindani inayoeleza mauzo kwenye kila kanda; na ndiyo ripoti iliyotumika kuamua kama Scancem wanapewa hisa za Tanga Cement ama hapewi. Kwa hiyo, mimi nilichofanya hapa ni kudurufu kile ambacho FCC wenyewe wamesema. Na hii ripoti inaeleza tu kama hawa wawili watauzaje kwenye soko. Ndio kila kampuni inauza, lakini inategemea na percent ya kila kampuni kwenye kanda husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha, muda wangu umeisha. Tunachoshauri ni kwamba, taratibu zifuatwe, kama twiga anataka kununua wahakikishe manunuzi hayazidi ile threshold ambayo tumejiwekea, asilimia 35 mpaka 40 kwa vigezo maalum. Kwa sababu wao wenyewe, tunatambua, hata vigezo ambavyo amepewa na FCC vya kununua baadhi yake anavipinga. Sasa na sisi kama Watanzania lazima tuwe tuna maswali. Mama amefungua fursa, wawekezaji ni wengi, Serikali iweke mchakato vizuri, wawekezaji wengi wapo, mchakato uwe wa wazi, usilete maswali ili tuhakikishe kwamba, rasilimali za Watanzania zinalindwa na taratibu na sheria ambazo tumezitunga sisi wenyewe zinafuatwa, ahsante. (Makofi)