Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru lakini nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai. Pia, niishukuru familia yangu kwa kunivumilia kuwa peke yao na mimi nikichapika na kazi huku za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote humu ndani ni viongozi. Familia zinatutegemea, taifa linatutegemea lakini vizazi vijavyo vinatutegemea sana. Kwa kadri tutakavyofanya vizuri sasa hivi, ndivyo tutakavyoweka mazingira mazuri ya vizazi vinavyokuja. Inashangaza katika level hii ya uongozi, sisi kwa maana ya Wabunge kufikiria katika level ya kifamilia kwa kweli tutakuwa hatuitendei haki nchi hii. Tunatakiwa kufikiria katika level ya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kuiwezesha nchi hii kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia na mimi hili jambo lilozungumziwa na wabunge wengi hapa la uuzwaji wa Tanga Cement. Kwa sababu gani? Lina masilahi ya nchi. Tunatamani kabisa kwamba Wabunge wote tukae hapa tukiwa na mtizamo huo kwamba hili jambo tukiliendea Kimasihala tutapata doa kubwa sana kwa kizazi kinachokuja kwa kuliingiza taifa hili katika janga. Tunayo kila sababu ya kufanya analysis ya kutosha kabisa na kufanya maamuzi ya kufanya jambo hili lakini pia Sheria zinatakiwa zifuatwe lakini pia wataalam waachwe huru wafanye kazi zao kitaalamu ili kusudi tuweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo dhana miongoni mwetu kusema kwamba linalofanyika sasa hivi la kuuzwa kwa Tanga cement kwamba ni jambo baya. Hata hivyo, nataka nikwambie kwamba ubaya au uzuri wa jambo hili tunaweza tukauangalia au tukaliona katika muktadha wa misukumo isiyopungua minne. Jambo hili liko katika misukumo minne kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, msukumo wa kwanza, nii msukumo wa muuzaji. Muuzaji amekuwa na changamoto ya uendeshaji wa Kampuni hii kwa takribani miaka minne au mitano tangu Mwaka 2016. Hivi sasa amekuwa akipata hasara hali ambayo iliyofikia mpaka sasa hivi tunavyokwambieni ni takribani miezi minne watu hawajalipwa mishahara yao. Jambo hili kwa namna yoyote ile hakuna mfanyabiashara ambae anaweza kulivumilia. Kwa sababu athari zake ni kubwa. Athari zake ni kwamba: -
(i) Serikali inakosa kupata kodi yake kwa maana ya corporate tax;
(ii) Kuna watu wamewekeza pale ambao walikuwa na matumaini ya kupata faida kwa maana ya dividends, hawapati kampuni inashindwa kuwalipa.
(iii) Pia huyu anahusiana na watu wengine kwa maana wanunuzi kwake lakini kwa anaowauzia (suppliers na customers).
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali kama hiyo lazima kuna mazingira ambayo yanapelekea mahusiano yale yakawa sio mazuri. Tunasema kuna jeopardize uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna msukumo mwingine, huu ni msukumo wa mnunuzi. Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la kasi sana la bidhaa hii ya cement. Tanzania imezalisha kiasi kikubwa sana cha cement mpaka kufikia mwaka 2022, kulikuwa na uzalishaji wa takribani tani zipatazo milioni 7.5. Pia, kumetokea ongezeko la soko la nje ambalo Tanzania kupitia viwanda vyake hivi vimelipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ongezeko kubwa kiasi cha kwamba mpaka kufikia mwaka 2022, Tanzania iliweza kuuza nje kiasi cha dola milioni 147.6. Hata hivyo, pamoja kuuza nje hivyo, pia tuliweza kununua kutoka nchi za nje cement hiyo hiyo kwa thamani ya dola milioni 137.2. Sasa ukiangalia hapo kwa mtazamo huo unaweza ukakuta kabisa kwa mfanyabiashara yeyote yule mwenye jicho hawezi kuiachia hiyo fursa. Huo ni msukumo ambao mfanyabiashara unamsukuma aamue kuinunua hiyo kampuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika kuna msukumo wa Serikali. Serikali inatarajia kupata pesa kwa mtindo wa kodi kama nilivyowahi kusema hapo. Serikali inatagemea sana kuimarika kwa bidhaa hii ya Cement kwa ajili ya kuweza kukidhi haja ya mahitaji ya miradi yake ya kimkakati kama vile Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere lakini na mabwawa mengine ya umwagiliaji, Mradi wa Fly over, Mradi wa Reli na miradi mingine ambayo inatarajia kabisa kwamba kama atanunua kupitia soko hili la ndani kwa vyovyote vile watakuwa wamenunua kwa bei ya chini kabisa na hivyo kufanya miradi hii kuwa viable na kuleta tija mwishoni mwa safari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtazamo mwingine tena, huu ni mtazamo wa walaji. Walaji wanategemea kabisa kwamba bidhaa hii iwe ni ya bei ya chini lakini iwe ni bidhaa ya uhakika, kusiwe na bei za kubadilika badilika. Katika mazingira hayo kama nilivyojaribu kusema huko mwanzo unaona kabisa kwamba mazingira haya yote unapelekea uuzwaji wa Tanga cement kuwa hakuna njia lazima Tanga Cement iuzwe. Hii ina- justify kwamba Tanga cement iko katika mazingira ya kwamba lazima iuzwe kwa ajili ya masilahi mapana ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kinachotokea sasa hivi kumekuwa na madai ya hapa na pale kama nilivyosema watu wamekuwa wakidai kwamba jambo hili si zuri, ni masuala ya kufirika tu. Unavyozungumzia cartel kwamba Twiga Cement Ikinunua Tanga cement itasababisha cartel hilo ni jambo la kufikirika. Kwa sababu hakuna mazingira yoyote yale ya kibiashara kwamba yanaonesha cartel inaweza ikajitokeza. Kwa sababu gani? Kwa sababu cartel inakuja baada ya kuwa na stiff competition yaani ushindani uliokuwa mkubwa sana miongoni mwa makampuni yaliyoko kwenye participation ya biashara hiyo. Kiasi cha kutishiwa kuona kwamba kuendelea kuvutana inasababisha wao kuwa na cost ya production kuwa kubwa. Sasa kwa namna moja wanalazimika kwamba basi wapange bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira hayo hayapo hapa kwetu kwa sababu gani? Hapa kwetu sio tu bidhaa ya cement lakini bidhaa yoyote ile hakuna bidhaa ambayo ina meet competitive market. Masoko yetu yaliyoko hapa hapa nchini yana viashiria tu vya kuonesha kwamba kuna competition lakini is not competitive market na hivyo suala zima la kusema kwamba kuna cartel hili ni suala la kufikirika na tusiingie katika mtego huu. Tuiache Twiga cement ainunue Tanga Cement kwa sababu kutakuwa na tija kubwa, production itakuwa kubwa lakini pia atakuwa na ushindani na makampuni mengine ya nje.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA:…kutakuwa na uwezo wa kuwa na creativity katika kampuni lakini pia …
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mchungahela, kiti kikizungumza inabidi usubiri. Naomba upokee taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Timotheo Mnzava.
TAARIFA
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, sidhani kama kuna mtu ana shida ya nani kumnunua nani. Nataka nimpe tu taarifa kwamba kwenye kuangalia hili hatuangalii stiff competition peke yake, namna ya ku-measure iko nyingi. Hali ya soko, share markets, capacity ya viwanda kuzalisha na sababu nyingine. Ukisoma Major analysis and report ya FCC ukurasa wa 34, wenyewe wanakili kwamba hawa waki-major wakafika asilimia 42 na point ya share ya market, hiyo ndio changamoto iliyopo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, unapokea taarifa?
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa kwa muktadha kwamba market share sio inayosababisha cartel kwa kadili nilivyojaribu kuzungumza hapa. Kwa sababu sikuwa na muda tu, kama ningekuwa na muda ningeweza kumpa fact zote zinazosababisha cartel na miongoni mwake ni competition ya market na sio kuwa na wingi wa share. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi Dangote ana share takribani kwa mfano 20 percent lakini anaweza aka-inject capital kubwa pale kiasi cha yeye akawa na uwezo sasa wa kuwa na share asilimia 60 utamfukuza sokoni? (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, na muda wako umekwisha, hitimisha hoja yako. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nashukuru kwamba ninachotaka kuhitimisha ni kwamba tuynatakiwa tuwe makini kwamba Serikali yenyewe iwe makini katika utendaji wake kwa sababu shida iliyoko hapa siyo wafanyabiashara walioko sokoni shida inaweza ikapatikana kwa watendaji wa Serikali katika kutimiza majukumu yake; na kutokutimiza majukumu kwa Serikali isitupiwe kwamba hawa wafanyabiashara wanafanya kosa la jinai ambalo sisi nafikiri tunaweza pia tukaliona kwamba siyo kosa isipokuwa huu ni udhaifu wa upande mwingine. Mimi ninaomba tuwe serious biashara tunahitaji biashara kubwa wafanyabiashara wakubwa wakubwa ambao wataiondoa nchi hii hapa tulipo na kuwa katika viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.