Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. TAUHIDA C. GALLOS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuweza kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia. Kwanza kabisa nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuipeleka Tanzania mbele na kuifanya Tanzania isonge mbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo machache tu, nina mambo matatu ambayo kwa leo ningependa kuyazungumza. Kwanza kabisa nianze na suala la Kiwanda cha Viuadudu kilichokuwepo Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa zaidi nikushauri Mheshimiwa Waziri kwenye kiwanda hiki. Jambo la kwanza, kwa namna ambavyo tumeenda kukitembelea kama Kamati, tungetamani sana kuona unapata muda na kukutana na mawaziri wenzio, aidha Waziri wa Afya au Waziri wa TAMISEMI. Kile kiwanda ili kiweze kufanya vizuri, ili kiwanda kiweze Kwenda kwanza tuanze na soko letu wenyewe la ndani. Kwenye suala hili la Kiwanda cha Viuadudu tungeanza kupata kwanza soko tungetengeneza sisi wenyewe tukaacha kununua dawa kutoka kwa wafanyabiashara wa kawaida ambao wanatuletea. Tafsiri yake Mheshimiwa Waziri si nzuri; na kwa nini si nzuri, kile kiwanda ni cha kwetu. Tunanunua dawa kutoka kwa watu wengine wa nje. Imani tunayoijenga tunawaza kwamba hasa kinachotusumbua pale ni ten percent.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuanze na masoko yetu ya ndani. Kama mtakaa na Mheshimiwa Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu mkaweka mikakati dawa zile mtazitoa vipi ile fedha itazunguka ndani na itatupa faida. Kiwanda kitaleta faida dawa zitakuwa zinafanyiwa kazi ndani ya Tanzania, lakini isitoshe pia itakuwa inafanya kukuza kiwanda chetu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninataka kushauri, Mheshimiwa Waziri na hili leo ndilo limenifanya nisisimame kwenye Wizara hii. Wakati tuko kwenye ziara ya Kamati tulipita TIRDO, kama sikosei pale panaitwa TIRDO, Dar es salaam; tuliwakuta vijana ambao wanafanya kazi moja nzuri sana. Hao leo ndio wamenihamasisha kusimama hapa kuchangia. Mpaka ukafika wakati najiuliza, hawa vijana ni Watanzania? Wako hapa hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri hajawahi kuwaona au hajawahi kubahatika kwenda kuwaona namshawishi aende akawaone. Hivi leo kijana wa Mtanzania ana uwezo wa kufanya vitu vikubwa, anau wezo wa kufanya mambo makubwa lakini anakosa nguvu ya kifedha. Kuna muda lazima tuoneshe njia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika pale kijana wa Kitanzania anatengeneza kifaa cha umeme, ananiambia leo mimi kama niko Dodoma nyumbani kwangu taa watoto wameziwasha mpaka saa tatu asubuhi nina uwezo wa kuiambia kupitia simu naomba taa uzime na taa zikazima. Hawa vijana wako Tanzania Mheshimiwa Waziri hatuoni thamani yake? hatuoni wanacho kifanya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwenye hili dada yangu ataniwia radhi kidogo niseme. Hebu tuangalie kwa namna ya kipekee; tunamuuliza kijana wa Kitanzania umeshindwa wapi umekwama wapi anasema fedha, lakini vifaa vile vile ambavyo tumeoneshwa pale anasema kwamba kama atapata mtaji mzuri hata upatikanaji wake bei yake itakuwa chini. Ana uwezo wa ku- control umeme wa ndani ya nyumba, kifaa hicho kijana wa Kitanzania anaweza kutengeneza. Mheshimiwa Waziri tuondoshe wenzio tulipo kila kitu tunategemea kutoka nje kila kitu tunategemea kutoka kwa nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuondoshwe kwenye akili ya kutawaliwa, Watanzania tuhamishwe kwenye akili za kutawaliwa, tuwape vipaumbele vijana. Ni mara nyingi nikisimama namuongelea kijana kwa sababu nukiongelea kijana nimemuongelea mwanamke; mwanamke ndiye mwenye mzigo wa kukaa na kijana wake, asipokuwa na ajira mama ana huzuni, asipokuwa na ajira na hajui mtoto wake anapokwenda mama anahuzuni. ndio maana muda mwingi namuongelea kijana wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hapa kwako juu hakuna shida hebu angalia hapa chini kwako kuna nini? Chungulia; unafanya kazi kubwa na kazi unazozifanya zinaitwa kazi, ni zile kazi kubwa chungulia chiniyako kuna nini? Kunaendelea nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mimi muda mfupi niliokuwepo kwenye Kamati hii ya viwanda dada yangu niseme kuna vitu haviniridhishi na kuna vitu naweza kuongea hapa lakini kuna vitu ninaweza nikakushauri kama Waziri tutakapokutana. Mheshimiwa Waziri angalia kuna kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani jambo kubwa sasa Tanzania tunalotaka kuona tunataka kuona milango ya ajira za vijana ikifunguka; Wizara yako imebeba Wizara ya Uvuvi Wizara yako imebeba Wizara ya Kilimo leo tunahamasisha watu walime kama wewe viwanda hukuvifungua watapeleka wapi? Watauza vingine vitabaki vitaoza. Naomba tuwe na mikakati ya sasa na ya baadaye. Mikakati ya baadaye tutauza nje, ya sasa tutatengeneza bidhaa za ndani kwa kuona wakulima wanapata nguvu. Mheshimiwa Waziri umebeba Wizara nyingine nyuma yako, wizara ulizozibeba tunaomba tuone mabadiliko. Pambana, mwanamke hajui kushindwa, mwanamke anajua kupambana, mwanamke siku zote anaonesha dira, anaonesha njia, analeta mabadiliko, hiyo ndio kazi ya mwanamke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ataniwia radhi, sijasema nimejisikia tofauti kwenye hili suala la Tanga Cement. Nimetafakari toka asubuhi linavyochangiwa, sijui lakini ni dhahiri kwamba sioni kama limetendewa haki na Bunge hili, kwa sababu Mheshimiwa Waziri leo ukienda kwenye Kamati ya Sheria hawaujui huu mgogoro ukoje, Kamati yetu ambayo Waziri yupo, hatulijui hili jambo likoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala sasa kwa namna nilivyolisikia linavyochangiwa, maana yake nimekuja kulipima, nimekuja kulikuta, Wabunge wanaotoka Tanga kwa namna wanavyotetea wana haki yao na sioni walipokosea, lakini nikamsikiliza kaka yangu Musukuma alipozungumza nikasema, hee! Ndio yaliyopo haya. Hebu hili suala Mheshimiwa Waziri aliweke kinaga ubaga tulifahamu likoje, kwa sababu linaleta dhana mbaya ndani ya Bunge, linaleta sintofahamu ndani ya Bunge, watu watakuja kutafsiriana sivyo ilivyo, lakini kila mmoja ukimsikiliza ana haki yake ya kusema hayo anayoyasema. Katika suala hili nadhani Wizara ina Mwanasheria, nafikiri zaidi lipelekwe kwenye sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yetu kwenye hili sio Tanga kanunua nani, cement kanunua nani, hofu yetu tuko salama? Hofu yetu Watanzania kwenye haya wako salama? Ndio maana watu wanalichangia. Ukikaa ukisikiliza hoja kwa makini hutokuwa na maswali ya kujiuliza na kila mtu utampa haki yake. Asubuhi nimemsikiliza Mheshimiwa Mnzava, kaka yangu hapa nimemsikiliza, kwa hiyo nilichoona mimi kwa tafsiri yangu wanatetea Tanga yao, wanatetea vijana wao, ndicho nilichokitafsiri, lakini mbele hakuko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Musukuma Kaka yangu kasema, kunakuwaje na kampuni ya mfukoni. Nimwambie Mheshimiwa Waziri, nikitaka nilichambue sana kwa upana, nahisi sintoitendea haki Serikali yangu, kwa sababu kunakuwaje na kampuni ya mfukoni? Nikushauri Dada yangu Mheshimiwa Waziri kwa upendo, hili jambo waliangalie, kama mchakato umefika sehemu haujakaa vizuri warudi hatua tatu nyuma. Kurudi nyuma tukatoa maamuzi sahihi sio kitu kibaya na haifanyi kuwa amefanya vibaya, amekuwa mtu wa busara zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sakata hili au tatizo hili tunakosa mchango mzuri kwa sababu halileti tafsiri nzuri kwa umma, halileti tafsiri nzuri kwa Bunge na nafikiria hata Spika wetu kwa sasa linamuumiza kichwa. Mheshimiwa Waziri aliweke wazi, kuna shida gani, kuna siri gani zimejificha ambazo wengine hatuzifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo liende kisheria, lipelekwe kisheria kama mchakato kuna sehemu umeharibika urudiwe upya, kila mwananchi na kila Mtanzania hususan Wabunge wanaowakilisha Tanzania waelewe kuna nini, ili tutakapokuja kulichangia tena kabla ya kutoa maamuzi lipi liwe lipi tunaomba hili jambo tushirikishwe, tuisaidie Tanzania kama Wabunge wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa hayo machache, naomba kuwasilisha. (Makofi)