Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa kabisa nitumie fursa hii kukushukuru wewe na kiti chako kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu kwa ustawi wa Taifa langu na watu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba ni– declare Mwalimu Dkt. Ashatu ni mwalimu wangu alienifundisha Mzumbe University masomo nikiwa mwaka wa kwanza alinifundisha masomo ya uchumi. Kwa hiyo, ninachangia Bajeti ya Waziri ambaye ana sehemu ya kunifanya kuwa hivi nilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwanza kabisa ninakwenda kuchangia maeneo matatu la kwanza Statistics za Nchi zinaonyesha Kanda ya Mikoa zaidi ya kumi na nne inayojihusisha katika shughuli za kilimo cha pamba ambacho takwimu zinaonyesha ndani ya Taifa letu la Tanzania wakulima waliyojiajiri katika Sekta ya Kilimo ya Pamba wanakadiriwa kuwa takribani wakulima laki sita mpaka laki saba na wengi wanatoka kwenye Mikoa ya Mara, Geita , Mwanza, Simiyu, Tabora, Shinyanga, Singida na baadhi ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, chama kilichopo madarakani kwa mara ya kwanza ninaona dhamira ya Rais Samia kwenda kuandika unique record katika Taifa letu kwa sababu ya initiative hizi zilizofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza; nimesoma Hotuba ya Mheshimiwa Waziri na Mwalimu wangu Hotuba ya Waziri inaonyesha Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba wawekezaji wote wanaofanya uwekezaji katika viwanda vya pamba mwaka huu pamba yote ya kulima niliyowataja kutoka Mikoa hiyo ambayo wanafanya jumla ya watu waliyojiajiri hizi ni ajira zaidi ya laki saba Rais wetu ameonyesha uzalendo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu toka nimekuwa Mbunge term yangu ya kwanza mwaka 2015 nimekuwa nikiwasemea wakulima wa pamba juu ya uhaba wa bei ndogo wanayoipata katika mazao yao ya pamba. Lakini kwa juhudi hizi za Rais tunaambiwa ya kwamba wakulima wote watakwenda kuuza pamba yao kwa viwanda vya ndani na nini kinakwenda kufanyika? Tunaona mikakati ya Serikali kuhakikisha kwamba viwanda hivi vinakwenda kutengeneza vitambaa vitakavyo ongeza thamani ya pamba ya mkulima na kuongeza export nje hilo litakwenda kuleta nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, statistics Waziri alizozisoma zinaonyesha sales yetu ya nje ime–raise kwa asilimia 64.4 na vitu vilivyochangia ku–raise kwa hiyo sale ya nje ambayo ni dollar kama milioni 4,000 bidhaa zinazo ongoza ni gold, cotton, coal na mengine kwa mpango huu Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie mwalimu wangu ninakupa big up sana, tunampa big up Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hichi anachokifanya anatafsiri kwa vitendo yale yote yaliyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kumsadia mkulima wa zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie, nataka nilipe Bunge lako tukufu taarifa; wakulima wa pamba katika Taifa letu wanachukua idadi ya ajira ya watu wanaokadiriwa laki saba. Tukiweza kuwasaidia wakulima kuuza pamba ndani na bei yao ikapanda hiyo ni sawa na kusema ya kwamba dollar milioni 4,000 tulizozirekodi za sale kwa sababu tutakuwa tumeongeza thamani tutakwenda kuifanya Tanzania kupata fedha za kigeni na wakati huo tutakwenda kuinua pato moja moja la zaidi ya ajira laki saba nje ya ajira ambazo zitakuwa zimeguswa kutokana na spiral over impact ambayo itatokea katika uwekezaji huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mkija na mipango mizuri lazima tutawaunga mkono, lazima tutawasemea hongera sana Waziri, hongera sana Mwalimu wangu Dkt. Ashatu sisi tuna kuunga mkono katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuweka rekodi nyingine Taifa letu lilikuwa linakumbwa na uhaba mkubwa sana wa uzalishaji wa sukari katika nchi. Nimesoma ripoti kutokana na Hotuba ya Mheshimiwa Waziri statistics zinaonyesha kwa juhudi za makusudi zilizofanywa na Serikali ya Rais Samia uwekezaji katika viwanda vya sukari umeongezeka na tume–observe ongezeko la tani 80,000 kwa mwaka peke yake wa 2022/2023 nani kama Mama Samia jamani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwenye hilo hatuna sababu ya kuacha kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, kwa kuwezesha mikakati hii na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha ya kwamba tunapanua uwekezaji wa zao hili la miwa pamoja na kuongeza uwekezaji katika uzalishaji wa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeambiwa nimesoma ripoti viwanda vinaonyesha TCDS zao walizokuwa wameziweka mwanzo expansion itafanyika zaidi kuhakikisha ya kwamba sukari inakuwa ya kutosha katika taifa letu tuweze kutosheleza soko la ndani na kufanya exportations na kiusababishia Serikali yetu kupata faida zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu; nalotaka kulizungumzia nina mpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Tauhida inawezekana ameondoka. Mheshimiwa Tauhida amesema Mheshimiwa Waziri wewe ni msimamizi karibia wa Wizara zote katika masuala ya uwekezaji jambo ninalokushauri Mheshimiwa Waziri wangu na Mwalimu wangu Ashatu tunakuomba uweke jicho lako la karibu sana katika Taifa letu lazima tuwe na kitu kinaitwa continuity katika investment hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inajitokeza wakati mwingine makampuni yamekuja yamewekeza, wamefanya uwekezaji mkubwa, wanapotaka ku–renew mikataba wanakuja na plan kubwa za kuweka uwekezaji, sisi tunaona kwamba mtu akiwekeza eti miaka kumi, ishirini eti miaka mingi. Kuna mataifa mengine makampuni yanawekeza mpaka miaka mia mbili na rekodi zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Tanzania makampuni yanakuja mtu anawekeza miaka ishirini, kwa mfano nilikuwa natolea mfano hawa watu wa Songas. Kampuni ya Songas imewekeza kwenye umeme na wamefanya juhudi kubwa kuzalisha umeme wa uhakika chini ya Wizara ya Kaka yangu Mheshimiwa January Makamba leo kwenye kusaini mkataba tunasikia eti wanabembeleza Serikali muwaongeze mkataba hivi jamani kwa umeme tuliokuwa tunauziwa senti sita na watu hawa na hawa ni mashirika ambayo wamekeza Serikali za Uingereza na Norway kweli watu hawa sasa hivi waanze kutuomba kuongeza mkataba na Taifa letu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa wito. Tujenge utamaduni wa kuwa na continuity ili tujenge trust kwa investors walioko nje wajue umuhimu wa kuwekeza Tanzania watapewa nafasi ya kutosha. (Makofi)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka wapi?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, unilindie muda wangu hizi taarifa hizi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Stanslaus Mabula.

TAARIFA

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kumlindia muda nataka nimpe tu taarifa kwa sababu amewataja Songas, TPDC ambao ni wabia wakubwa wa Songas kwa miaka yote waliyokuwepo hapa nchini wameokoa zaidi ya trilioni kumi na sita kwa hiyo nadhani Mheshimiwa Kingu anahoja ya msingi namuongezea tu nyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kingu, unapokea taarifa? Na muda wako umekwisha.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa hiyo ninapokea nimalizie, nimalizie na kama ametaja Shirika la Serikali mimi naunga mkono Mheshimiwa Waziri, tunakuomba Wizara yako inagusa Wizara zote katika mambo ya biashara, usiwekewe mipaka fuatilia uwekezaji katika Wizara zote tumsadie Rais na sisi tuna kuunga mkono mwalimu wangu, kiongozi wangu tuko pamoja na wewe kazi iendelee. (Makofi)