Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda nishukuru kwa kupata nafasi hii ya mwanzo kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Kwanza kabisa, napenda nitoe shukrani zangu kwa Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, pili, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na wasaidizi wake wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuimarisha Wizara hii ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Spika, pia napenda kutoa pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuleta uwekezaji hapa nchini. Kwa kweli Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana, wawekezaji katika nchi hii sasa hivi wanakuja kwa wingi sana, na nina imani kabisa Tanzania itakwenda mbele zaidi kibiashara pamoja na Sekta ya Viwanda.
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie suala moja kuhusu ushindani wa kibiashara. Katika suala hili, kidogo bado kuna changamoto, na hasa katika suala la biashara ya mafuta ya kula. Pale kwangu Bagamoyo, pamoja na shughuli nyingine za watu wa Bagamoyo, biashara kubwa sana pale inayofanyika kupitia Bandari yetu ya Bagamoyo ni ni biashara ya mafuta. Wafanyabiashara wengi wa Bagamoyo wanatoa mafuta kutoka Zanzibar, wanayaleta Bagamoyo na hatimaye kwenda kuyauza katika sehemu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara hawa wanapata changamoto kubwa sana ya ushindani. Wanalalamika kwamba wenye viwanda, Serikali katika bajeti iliyopita wamewapatia zero percent ya import duty, lakini hii zero percent wafanyabiashara wanatakiwa walete mafuta ghafi (crude oil). Inavyosemekana ni kwamba wafanyabiashara hawa hawaleti mafuta ghafi, wanaleta mafuta yaliyosafishwa ambayo ni refined oil na kwenda kuya-park katika viwanda vyao, na hivyo kwenda kuyauza. Hili linajidhihirisha wazi kwamba mpaka sasa bei ya mafuta pamoja kwamba Serikali imeshusha, wanafanyiwa zero percent, lakini bado bei ya mafuta iko juu, pamoja na kwamba Serikali imewapunguzia kodi hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfanyabiashara wa kawaida anachajiwa asilimia 25 ya kodi, lakini mfanyabiashara mkubwa anawekewa zero. Sasa hii kweli tutaleta ushindani wa kibiashara na tunaweza kuwakuza kweli wafanyabiashara wetu katika nchi hii?
Mheshimiwa Spika, leo hii mtu wa Bagamoyo anachukua dumu la mafuta kutoka Zanzibar, likifika Bagamoyo pale linachajiwa shilingi 33,000 kodi, ukijumlisha bei ya manunuzi aliyonunulia kule, na gharama nyinginezo za TBS, mionzi, sijui nini, dumu hili linafikia mpaka shilingi 75,000 au shilingi 78,000 mpaka shilingi 80,000. Hivi huyu mtu anafanya biashara gani?
Mheshimiwa Spika, ile bandari kipindi cha nyuma tulikuwa tunafanya biashara, TRA walikuwa wakipata mapato makubwa sana. Ilifikia wakati tunatengeneza mpaka Shilingi bilioni mbili na zaidi kwa mwezi kwa kupitia Bandari ya Bagamoyo na wafanyabiashara wa Bagamoyo, lakini leo hali ni tofauti. Namwomba Mheshimiwa Waziri, katika ushindani wa biashara azungumze na Wizara ya Fedha, hizi kodi ambazo wanawapunguzia wafanyabiashara wakubwa katika mafuta ya kula, zinawapa changamoto wafanyabiashara wadogo, wanashindwa kuendelea, hawafiki mbali kibiashara.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nataka kuzungumza ni suala la SEZ (Special Economic Zone) Bagamoyo. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kipengele cha 195 ameelezea vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2023/2024 katika maeneo maalum ya uwekezaji. Nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri hili. Nimeona Bagamoyo katika mipango yako ya vipaumbele umeiweka katika kipaumbele. Nashukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo kuwajali katika hili.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika malengo ya Wizara kwa mwaka 2023/2024 sehemu ya 196 Mheshimiwa Waziri amezungumzia uendelezaji wa miradi ya Kitaifa ya kielelezo, (National Flagship Projects). Kwa kweli kwa hili wananchi wa Bagamoyo wanampongeza sana Mheshimiwa Waziri na wanamshukuru sana, amewatendea jambo la haki sana.
Mheshimiwa Spika, haitoshi, katika kipengele hicho hicho Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala la fidia kwa watu wanaopitiwa na huu mradi wa SEZ. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa kweli amefanya kazi kubwa sana, wananchi wa Bagamoyo Kata ya Zinga, maeneo ya Mlingotini, Pande na maeneo mengineyo ya Kondo walikuwa wanalalamika sana kuhusu hili jambo, na kwa bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ameituma timu kule inayoongozwa na Dkt. Mchome wa Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam, wanafanya kazi nzuri, nami nimezungumza nao, wanaendelea na kazi nzuri kabisa ili kuweza kuliweka jambo hili sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, itakapofikia kipindi, wananchi wa Bagamoyo wamelipwa katika hili jambo kwa kweli watampongeza sana Mheshimiwa Waziri na watamwombea sana kwa Mwenyezi Mungu. Maana ni mwaka wa 13 sasa hivi, wananchi wa Bagamoyo wa sehemu hizo bado hawajapata malipo yao. Kwa bajeti ya mwaka huu, kwa kulizungumzia hili la fidia ya wananchi hawa, kwa kweli sina budi kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri katika jambo hili.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala ushindani wa biashara, naomba Mheshimiwa Waziri wa hii Wizara na Waziri wa Fedha waangalie jinsi gani ya hizi kodi zitashuka ili wafanyabiashara nao wapate kufanya biashara zao na kupata faida. Bagamoyo inaendeshwa na bandari, wafanyabiashara wengi wanaendeshwa na bandari ya ile, mama ntilie wanafanya kazi kupitia ile bandari, wabebaji mizigo wanafanya kazi kupitia ile bandari, lakini suala la mafuta ya kula, itakapokuwa kodi kubwa, wafanyabiashara wa Bagamoyo hawatapata fursa ya kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)