Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi. Nawapongeza Wizara kwa mipango na mikakati mizuri ambayo wanaendelea kuifanya na kuleta matumaini makubwa ndani ya sekta ya viwanda na biashara.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia maeneo machache, la kwanza nitazungumzia viwanda ambavyo Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amevielezea kwamba ana mpango wa kufufua viwanda vya kimkakati. Nitajikita kwenye viwanda vya pamba ambavyo unatoka Kanda ya Ziwa kule, ndio sehemu kubwa ilikuwa na viwanda vya nyuzi enzi za utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Sasa atakuja kutuambia mikakati hiyo ameiweka kuhakikisha kwamba viwanda hivi vya kuchakata zao la pamba, naamini asilimia 70 ya zao la pamba tuna export asilimia 30 inabaki ndani ya Nchi. Sasa na mpango huu ukifanikiwa utatengeneza uchumi wa Taifa lakini vilevile utaongeza ajira kubwa kwa Watanzania hususan vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye zao la pamba lina vitu vingi ambavyo viko mule ndani. Kuna mbegu ambazo hutengeneza mafuta lakini kuna pamba yenyewe ambayo itatengeneza majora, itatengeneza khanga na vitu vingine. Jambo kubwa hapo ili kulinda masoko yetu ya ndani lakini na kuongeza thamani ya maji tunayozalisha hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, la kwanza; ni vizuri makorido ambayo yanaingiza khanga kwa njia za uchochoro yakadhibitiwa ili kuongeza thamani ya pamba katika Nchi yetu ya Tanzania. Vilevile na kuweka mkakati kwa sababu ameweka kwenye hotuba yake kwamba wanaenda kufufua viwanda. Sasa viwanda unavyovifufua hivi lazima tuweke utaratibu, taasisi zote za umma, magereza, jeshi, MSD na vitu vingine vyote vinavyotumia rasilimali hiyo ya pamba. Naamini kwa mpango huu mkiingiza hiyo component naamini kwamba tunaweza tukafanya vizuri zaidi na kuhakikisha kwamba viwanda vinafanya kazi kwa muda unaotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwenye viwanda vyetu vya korosho kule Mtwara, tunayochangamoto lakini naamini kwenye mpango wenu Wizara mlivyojipanga mkilisimamia vizuri na tukaja na majibu sahihi ambayo yataleta tija kwa Watanzania naamini jambo hili linaweza likafika mwisho na tunatengeneza historia kwenye nchi yetu tukaondokana na maneno ambayo kila siku tukiamka tunahubiri. Sasa tunahitaji tutoke hapa twende kwenye vitendo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni suala la kibiashara. Nchi yetu tangu ipate uhuru ilikuwa na viwanda vya cement vichache, kuanzia uhuru mpaka 2020 tulikuwa na viwanda tisa. 2020 mpaka 2023 leo tuna viwanda 14 na maana yeke ni nini? Maana yake wafanyabiashara wanapoongezeka ndio ushindani unaongezeka kupunguza mahitaji kwa wananchi wetu wa kawaida hususan watu tunaotoka mkioa ya Kanda ya Ziwa na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, viwanda vyote viko Dar es Salaam, viko Tanga na maeneo mengine lakini wahitaji wakubwa ni nchi nzima kwa maana ya kanda zote kwenye mikoa ambayo inauhitaji kwenye vitu hivi.

Mheshimiwa Spika, ijulikane kabisa, tunajenga barabara, tunajenga hospitali, tunajenga madarasa na wananchi wanajenga nyumba yote inahitaji cement.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikisikiliza jana mjadala huu wa Tanga Cement, ukiangalia Tanga Cement kibiashara pale na Simba ndio ipo kwenye soko na hii Simba iko kwenye soko na zamani Twiga cement nayo ilikuwa inachechemea pale Dar es Salaam. Watu walikuwa wakitumia magari kwenda kupakia, umebahatika sana unachukua wiki tatu au wiki mbili na Tanga Cement leo ndivyo hivyo hivyo ilivyo. Sasa ninajiuliza kama viwanda vinaongezeka na huyu anataka kuuza mali share yake sijui anamuuzia nani? Na ninyi Serikali kama mna mpango mzuri basi mashirika yenu ya umma yaunganisheni yanunue hiyo hisa asilimia 68 ili ninyi mmiliki kuondokana na sintofahamu iliyoko hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tumefikia viwanda 14, bado tunaanza kulalamika kwamba tuna hofu. Mimi sidhani mtu anayefanya biashara awe na hofu, hofu ya aina gani kwenye shughuli ambayo anajipatia kipato. Kwa hiyo, hili jambo ni vyema sana Serikali mkatueleza kwamba kuna nini humu ndani kimejificha ambacho Wabunge hatukifahamu na jamii haijui. Kwa sababu mambo haya yanayojitokeza haya kweli yanatoa taharuki ambayo hatuielewi elewi lakini mimi naamini pale Tanga kuna kiwanda kingine kinaitwa Mawenzi.

Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza au kuongezeka kile na kile kiwanda cha Tanga Cement kiufupi hakizalishi vizuri, kiuhalisia kabisa. Hata sasa ukituma magari kwenda kupakia unachukua zaidi ya wiki tatu mpaka nne, wanasubiria. Sasa huyu mwingine ameingia, sasa hapa sijui kunakaushindani kakibiashara. Sasa hapa mtusaidie ninyi takwimu zenu za kitaalamu, kwamba takwimu za uzalishaji kila kiwanda. Hivi viwanda 14 vinazalishaje na mahitaji yetu kama nchi ni kiasi gani na bado sisi hapa tumepakana na nchi ambazo ni jirani Rwanda na Burundi, naona cement wanachukua kutoka Tanzania inatokea Tanga inaenda kule Uganda na Burundi.

Mheshimiwa Spika, sasa yote haya ni vizuri watu wa Serikali mkitueleza mtatusaidia sana kwamba mkakati wenu ni nini na hiki kinacholalamikia ni kitu gani. Ili kusudi tuwekane vizuri tuweze kufanya kazi hii ambayo imetuweka humu ndani kwenye Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, niwapongeze sana taasisi kwa maana ya BRELA na TIC sasa hivi BRELA pale na TIC pale mtaji wako wa dola milioni 50 unapata incentive maisha yanaendelea. Kwa hiyo, waendelee kuboresha mifumo yao, isiwe ina kwama kwama kwa maana ya kwamba ili tusicheleweshe mambo, watu wanahitaji kuwekeza na Watanzania wanahitaji kufanya kazi nzuri kwa ajili ya maendeleo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye Kiwanda chetu cha Vifaa Tiba Dutwa tusifanye maigizo na kama kweli tuko serious tuna fedha za walipa kodi na huku tuna tatizo la ajira. Tunazitenga hela tunazila zinapotea halafu mradi unasimama. Jambo hili halikubaliki na sio sawa sawa, ilikuwa hakuna sababu yoyote ya kuanzisha mipango mikubwa na shughuli zingine zikawa zinakwama kufanyika, tukiamini kwamba tunakuja kupata mwarobaini, matokeo yake ikaka kimya na tukaanza kusikia sikia, mara kinakwenda Morogoro sijui kinakwenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani mipango ya Serikali anayoianzisha mtu yeyote kwenye eneo ambalo linalenga jamii ya wananchi. Basi anayekuja mwingine ni kuendeleza na ndio maana mama akasema kazi iendelee. Sasa kazi iendelee maana yake yale yote yaliyokuwepo yaendelee kutekelezwa. Kiwanda kile ni kikubwa na kikifanyiwa kazi naamini kabisa kitatoa solution ya zao letu la pamba katika Kanda yetu ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara hivi karibuni kule kwetu, pale Maswa kuna kiwanda cha chaki hivi ndio kiwanda cha kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vyema ile fedha inayohitajika kutoka kwa vijana wa Maswa basi iende ili kiwanda kile kianze kufanya kazi. Sasa pale kuna bilioni nane zimesimama halafu mambo haya hatuyatekelezi. Niwaombe sana Mheshimiwa Waziri tuna imani kubwa na wewe ni mchapakazi na una weledi wa kutosha. Ni imani yangu ya kwamba mambo haya yakikamilika naamini kabisa tutakwenda vizuri na hitaji kamili litatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)