Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji na Naibu wake Mheshimiwa Exaud Kigahe na watendaji wote wa Wizara na taasisi zote zilizo chini ya Wizara kwa kazi nzuri wanazofanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye umuhimu wa uwekezaji kwenye sekta ya viwanda hapa nchini kwa kuliwezesha Shirika la Maendeleo la Taifa (The National Development Corporation (NDC) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO). Pia nitagusia changamoto za viwanda katika jimbo langu la Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi yetu, chini ya Mwalimu Julius Nyerere tangu kujipatia uhuru na baada ya kutangaza Azimio la Arusha mwaka 1967 iliandaa mpango wa kutuletea maendeleo kwa falsafa ya ujamaa na kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, kupitia falsafa hiyo, viwanda vingi vilijengwa nchi nzima ili kusindika mazao karibu yote ya kilimo na mifugo. Kwa mfano, viwanda vya nguo vya Kilitex, Mwatex, Urafiki, Mutex viwanda vya korosho, kahawa, magunia, viatu, maziwa, nyama, Tanzania Cigarette Company, Tanzania Breweries na kadhalika. Vilevile mwaka 1965 serikali ilianzisha Shirika la Maendeleo la Taifa (The National Development Corporation (NDC). Shirika hili lilianzishwa kusimamia viwanda nchini.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali iliboresha elimu za ufundi katika vyuo vyetu vikuu na kati ili kuzalisha wataalam wa kuhudumia viwanda vyetu. Ili kuimarisha uchumi wetu, Serikali ilianzisha taasisi za kiufundi kama CAMARTEC, SIDO, TEMDO na taasisi ya utafiti wa viwanda TIRDO.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kama ilivyoelezwa hapo juu, nchi yetu ilibadilika na kukumbatia sera ya kubinafsisha viwanda na mashirika yetu ya umma kama ilivyoelekezwa na Benki ya Dunia kwa masharti ya kupatiwa mikopo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia utekelezaji wa sera hiyo, ramani yetu ya maendeleo ya Taifa ilivurugika na kudhoofisha sekta ya viwanda nchini.
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya viwanda katika miaka ya mwanzo baada ya Uhuru yalipatikana tukiwa na wasomi wachache sana waliobobea katika nyanja mbalimbali, leo hii tunaingia miaka 62 toka tupate uhuru. Kwa sasa tunao Watanzania wengi wenye elimu, ujuzi, uzoefu na maarifa ya namna ya kusimamia viwanda vilivyoko na vitakavyojengwa nchini. Kwa mantiki hiyo, ni wakati muafaka kuchukua hatua ya kuwatumia wataalam wetu wazawa na rasilimali zetu kusaidia kwenye kuwekeza na viwanda vipya hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kama Taifa, sasa ni wakati muafaka wa kutafakari na kufanya maamuzi ya kuliwezesha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ili kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya kuendeleza na kusimamia uwekezaji wa viwanda hapa Tanzania kwa kutumia wataalam wetu wazawa. Hii inawezekana ikiwa watapatiwa rasilimali pesa ya kutosha na wataalam watakaohitajika kwani katika uongozi wa awamu ya kwanza, NDC iliendesha shughuli zake kwa mafanikio makubwa. Shirika la NDC inatekeleza miradi inayogusa sekta zote muhimu kama kilimo, madini, afya, viwanda, nishati na biashara. Baadhi ya miradi hiyo ni Kiwanda cha Viuadudu Kibaha, Migodi ya Makaa ya Mawe Mchuchuma, Mradi wa Chuma cha Pua, Liganga, Mradi wa Magadi Soda, Monduli, Arusha.
Vilevile NDC inasimamia Bandari Kavu ya Nafaka, ETC Cargo, Dar es Salaam na mashamba ya zao la mpira yaliyopo Tanga na Morogoro. Pia NDC inamiliki kiwanda cha kuzalisha vipuli vya mashine na mitambo mbalimbali kilichopo mkoani Kilimanjaro cha KMTC. Kwa mantiki hii, NDC wanatekeleza majukumu makubwa sana kwenye sekta ya viwanda na uwepo wao ni muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TIRDO liliundwa ili kufanya utafiti na kutoa huduma za kitaalam ili kuendeleza viwanda nchini. Shirika hili ni muhimu sana kwani miundo na ujenzi wa viwanda umebadilika sana kutokana na kuwepo kwa teknolojia mpya sehemu nyingi duniani.
Mheshimiwa Spika, hapa Tanzania viwanda vingi vilivyojengwa miaka ya nyuma vimefungwa kutokana na sababu mbalimbali. Kutokana na ukweli huu, huduma ya utafiti ya TIRDO inahitajika ili kutoa ushauri elekezi wa ni nini kifanyike kufufua viwanda hivi.
Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la Moshi Vijijini, moja ya kiwanda kilichokuwa kimepata mafanikio makubwa sana ni kile kiwanda cha kukoboa mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd kilichopo Chekereni – Moshi katika Kata ya Mabogini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kilikuwa kimejengwa kwenye eneo ambalo linazalisha mpunga mara mbili hadi tatu kwa mwaka. Kiwanda hiki hakifanyi kazi tangu Septemba. 2014. Kiwanda cha kukoboa mpunga kilikodishwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahawa (KNCU) na baada ya kushindwa kukiendesha, mkoa ulimshauri Msajili wa Hazina kukirudisha Serikalini ili atafutwe mwekezaji mwingine anayeweza kukiendesha. Tayari Msajili wa Hazina amerejesha kiwanda hiki Serikalini tangu tarehe 18 Oktoba, 2018 lakini bado hajapatikana mwekezaji na shughuli zimelala. Kutokuwepo kwa kiwanda hiki kimeondoa fursa ya wakulima kupata bei nzuri ya mpunga na ajira kiwandani kwa wana Moshi Vijijini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda cha pili kilichopo jimboni kwangu na hakifanyi vizuri ni kiwanda cha bidhaa za ngozi Msuni kilichopo Kata ya Uru Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, kiwanda hiki kinamilikiwa na Kamati ya Maendeleo Kata ya Uru Kaskazini (WDC). Kina uwezo wa kuzalisha bidhaa mbalimbali za ngozi kama viatu, mikoba na mikanda.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoomba katika bajeti ya mwaka juzi na mwaka jana, narudia tena kuiomba Serikali itume wataalam wa TiRDO kwenye kiwanda hiki ili ushauri wa kitaalamu upatikane na kiwanda hiki kifufuliwe na kuunga juhudi za wana ushirika huu kwenye kukuza uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, jimbo la Moshi Vijijini ni maarufu sana katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo. Kama Serikali itakuwa na mikakati ya kuhamasisha uwekezajj wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuzindika mazao ya kilimo na mifugo, hii itasaidia kutengeneza ajira na kuongeza kipato cha wananchi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naishauri Serikali ifanye yafuatayo: -
Kwanza, Serikali ichukue hatua haraka na kuliwezesha Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ili litekeleza kikamilifu majukumu yake ya kuendeleza na kusimamia uwekezaji wa viwanda hapa Tanzania. Hii itawezekana ikiwa wataongezewa raslimali pesa na wataalamu wa kutosha.
Pili, kwa kuwa huduma ya TiRDO inahitajika sana kwenye kutoa ushauri elekezi wa ujenzi wa viwanda nchini, ninaishauri Serikali itenge fedha za kutosha na kupeleka wataalam wa kutosha kwenye fani zote ili kuliwezesha shirika hili kutekeleza majukumu yake.
Tatu, Wizara itafute mwekezaji katika kiwanda cha kukoboa mpunga cha Kilimanjaro Paddy Hulling Co. Ltd kilichopo Chekereni - Moshi, katika Kata ya Mabogini. Kiwanda hiki kinaweza kuwa ni chanzo cha kusafirisha nje mchele ulioongezwa thamani na kuwapatia wakulima kipato na Taifa kwa ujumla.
Nne, Vyama vya Ushirika vilivyopo Jimbo la Moshi Vijijini vihimizwe na kuhamasishwa kuwa na viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali ya kilimo na mifugo na kuyaongezea thamani ili kuzalisha bidhaa zinazotokana na kahawa, ndizi, mboga mboga, nafaka, mikunde, maziwa, asali, alizeti na mengine mengi. SIDO na TEMDO wanaweza kusaidia sana kwenye hili.
Mheshimiwa Spika, tano, kama nilivyoomba kwenye bajeti ya mwaka juzi na mwaka jana, bado naliomba tena Shirika la Utafiti wa Viwanda Tanzania (TiRDO) lishiriki kikamilifu kwenye kutoa ushauri wa kitaalam kukifufua Kiwanda cha Bidhaa za Ngozi Msuni kilichopo Kata ya Uru Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.