Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nami niungane na wenzangu katika kuwapongeza sana Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kufanya kazi nzuri sana, sana, sana ambazo zimekuwa reflected kwenye takwimu na taarifa mbali mbali. Vile vile nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hali na azma yake kubwa ya kutamani kuona Tanzania ikikua kiuchumi kwa kubadilisha sheria mbalimbali na pia kubadilisha mifumo na kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji ndani ya nchi yetu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza pia hasa kwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara miradi ambayo imesajiliwa kwa kipindi hiki tu kifupi; ukiangalia mwezi Julai, 2022 mpaka Machi, ni zaidi ya miradi 240, ambayo thamani yake ni Dola za Kimarekani milioni 438 na hii imesaidia sana katika kukuza uchumi. Sambamba na hilo, kumekuwa na ongezeko la ajira watu zaidi ya 39,245 ambao wamenufaika na ajira katika usajili wa miradi hiyo mipya.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Mheshimiwa Rais pia ameweka mikakati mbalimbali ya kukuza ajira. Moja ya mikakati ni hili la kuweza kukuza viwanda hasa katika suala la kwenye sekta ya uwekezaji. Tumebadilisha sheria, na pia tumerahisisha mazingira ya uwekezaji nchini kuweza kuwa rahisi zaidi ili uwekezaji ukue na kuweza kupata kipato. Nchi nyingi duniani leo zimetoka kwenye masuala ya kufanya biashara kwa maana ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, Serikali sasa imekuwa inatengeneza mazingira wezeshi na kukusanya kodi. Vile vile sehemu kubwa ya biashara, mfano ajira zinatokana zaidi na private sector ambayo sasa hivi Mheshimiwa Rais ameamua kui-enhance kwa sehemu kubwa sana, tunaona kwenye kilimo mapinduzi makubwa; kwenye uwekezaji tunaona mapinduzi makubwa; na kwenye viwanda tunaona uwekezaji mkubwa ambao unafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika upande wa ajira, tunaweza kuona kwa upande wa ajira za kisekta ni maagizo ya Mheshimiwa Rais na maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Wizara zote za kisekta lazima kwenye mwaka wa fedha unazopewa bajeti, zizalishe ajira ili Watanzania waweze kunufaika na ajira hizo katika ngazi mbalimbali. Hilo limekuwa likitekelezwa.
Mheshimiwa Spika, vile vile katika miradi tu ya Wizara za maendeleo, zaidi ya Watanzania 1,226,925 walipata ajira. Sasa kwa muktadha huo huo wa spirit ya Mheshimiwa Rais ya kutaka kuongeza ajira, kukuza uchumi na kutengeneza uchumi jumuishi ili kila mwananchi aweze kunufaika, ni pamoja na kutengeneza mazingira ya kuwasaidia wawekezaji, na pia kusaidia kwenye sekta ya uchumi ya biashara ili iweze kufanya vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, nimesikia hili suala la Tanga ambalo limesemwa sana na Waheshimiwa Wabunge hapa. Nimelazima kufuatilia kwa sababu limegusa hasa kwenye sekta na Wizara yetu ya kwenye masuala ya ajira. Ni kweli nimefanya utafiti na nimeangalia kwenye rekodi mbalimbali zilizofanywa ikiwa ni pamoja na hesabu za kihasabu zilizofanywa kwenye Kampuni ya Tanga Cement, inathibisha kwamba Tanga Cement haina uwezo tena wa kujiendesha, ina-run kwa hasara. Zaidi ya hapo, hata fedha zile ambazo inazipata kidogo katika operation, inajikuta inashindwa kulipa kodi; na kwenye eneo la kodi lazima uangalie kama ni faida. Unaangalia faida ghafi ambayo ni jumla ya gross profit, na pia utaangalia net profit baada ya operational cost. Pia utaangalia gharama nyingine ambazo utazipata kama unapata faida baada ya kulipa kodi, na vile vile utaangalia kabla ya kulipa kodi na baada ya kulipa kodi. Hizi zote zinathibitisha kampuni hiyo haina uwezo kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, katika maamuzi ambayo yalifanyika, FCC katika malalamiko yaliyopelekwa tarehe 2 Novemba, 2021 FCC iliamua kwa misingi miwili ambayo imeainishwa kwenye Sheria Ushindani ambapo katika Kifungu chake cha 5 (6) (a) na (b) kinatoa masharti kwamba kampuni haipaswi kuwa na nguvu kubwa kwenye soko, lakini pia (yenyewe peke yake) isiwe na uwezo ambao unaweza kuathiri watu wengine kufanya biashara. Katika tafsiri ambazo zilitumika FCC, waliweza kuzingatia matakwa pia ya Sera ya Taifa na pia mwendendo na mtazamo wa Serikali ya Awamu ya Sita, na pia katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayotaka kukuza uchumi wa Taifa, uchumi wa Watanzania na mtu mmoja mmoja na pia kukuza uchumi jumuishi na kutengeneza fursa za ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kipengele kilichotumika waliangalia muktadha huo na kuona kwamba katika kipengele cha 5 (a) kinachohitaji nguvu ya soko, ambayo kwa lugha ya kigeni inasema ni sales volume ambayo inahitaji isizidi asilimia 35, ndicho kigezo pekee ambacho kilionekana. Sheria hii katika kipengele cha pili inahitaji pia huyo mtu ili aweze kuonekana ana dominance kwenye soko, ni lazima awe amekidhi vigezo vyote katika kifungu cha 5 hicho, kipengele (a) na (b).
Mheshimiwa Spika, tafsiri iliyofanyika katika Fair Competitions Tribunal, wao walijikita zaidi kwenye kigezo kimoja tu cha installed capacity ambapo waliangalia katika kipengele cha asilimia 35 bila kuangalia kwamba sheria inataka vyote kwa pamoja vitamkwe kama jinsi sheria inavyosema katika kifungu hicho. Kwa hiyo, wakafanya maamuzi ya ku-crash decision ile na kusema kwamba maamuzi ya FCC yaondolewe na muunganiko huo usiwepo.
Mheshimiwa Spika, sheria hiyo hiyo pia katika kifungu chake cha pili inaitaka mamlaka katika kutafsiri sheria; haitafsiri katika mazingira yale, na ni principle ambayo hata kwenye sheria ipo, ya kusema kwamba every case should be judged from its own circumstances, kwamba kila kesi lazima iangaliwe na kutafsiriwa kwa mazingira yake kama jinsi ilivyo. Katika msingi huo huo, hata kwenye Sheria za Kiuchumi pia maamuzi yanaangaliwa kutokana na jinsi ambavyo hali ya kiuchumi, na mazingira yaliyokuwepo kwa wakati huo.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2020, maamuzi yaliyofanywa na FTC (Fair Competition Tribunal), wao walifanya uamuzi kwa ku-base zaidi na tafiti ambazo zilifanyika katika kipindi cha mwaka 2020. Hali ya sasa hata ukiiangalia, mwaka 2020 aliyekuwa anaongoza kama kiwanda kwenye kupata mengi na uzalishaji ilikuwa ni Twiga Cement anafuatiwa na Tanga Cement na Dangote. Kwa hali ya 2022 kwa tafiti zilizokuja kufanyika na takwimu kwa mujibu wa data ambazo zipo, inasema anayengoza kwa sasa, siyo kama ilivyokuwa 2020 tena, takwimu zinaonesha sasa Twiga Cement ndiyo anaongoza, anafuata Dangote na kuna kiwanda kingine ambacho hakikikuwepo kabisa kwenye soko, wakati huo kilikuwa hakizalishi, kilikuwa kinaanza, lakini sasa kinazalisha zaidi ya tani 900,000, ambacho ni Kiwanda cha Shuwan Maweni na kiwanda kingine ambacho kinafuata sasa ndiyo Tanga ambacho bado pia kinashuka katika uzalishaji, ambacho ndiyo maana ya maombi haya kuweza kufanya uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji huyu amekuwa anazalisha na anafanya kazi ya kuzalisha cement za Twiga lakini pia anaenda kuingiza capital, ku-inject new capital ya zaidi ya Shilingi trilioni moja ili kuongeza capacity. Katika maamuzi yaliyotolewa awali ya FCC, yalikuwa na masharti. Masharti hayo yalikuwa kumi, kati ya masharti matatu.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba dakika moja nimalizie.
SPIKA: Utakuwa unachukua muda wa Waziri hapo. Malizia dakika moja.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, katika masharti hayo yaliweza kukubaliwa pia na hao wadau wa maendeleo. Zaidi nimalizie tu kwa kusema kwamba, hili jambo siyo jipya. Ipo kesi ya Afrika Kusini ya mwaka 2019 na imefanyiwa maamuzi, ambapo kesi hiyo ilikuwa hivyo hivyo kwamba walirudi tena katika kufanya review baada ya maamuzi ya awali. Kwa hiyo, hakuna suala la kudharau Mahakama au maamuzi hapa. Suala lipo, linatoa haki. Sheria hiyo ni kwamba unaweza ukarudi tena kupeleka maombi kulingana na hali iliyopo kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, kuna kesi nyingine pia ya Toyota na Sifao Motors, ambayo nayo pia ilifanyiwa maamuzi hivyo hivyo na FCC ikakataa ombi lao, lakini pia ilivyokuja kurudi FCT, nayo pia ilikuja ikabariki maamuzi yaliyofanywa na FCC. Kwa hiyo, jambo hili siyo geni, tunachelewesha uwekezaji, tunachelewesha Watanzania kuweza kupata uchumi, tutaenda kupata hasara ya kupoteza ajira 3,000 za Watanzania, tutaenda kupata hasara za uwekezaji wa kukosa zaidi ya Shilingi trilioni moja kama maamuzi haya tutaenda kuyafanya kishabiki na bila kuangalia maslahi ya nchi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono kwamba suala hili la uwekezaji ni muhimu. (Makofi)