Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja hii muhimu ya Mheshimiwa Waziri wa uwekezaji viwanda na biashara. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema ambaye ametujaalia kukutana siku hii ya leo tukiwa na afya njema kuhakikisha tunapitisha Bajeti hii muhimu ya Wizara ya uwekezaji viwanda na biashara.
Mheshimiwa Spika, pili nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini, niendelee kutumikia nchi hii katika nafasi ya Naibu Waziri katika Wizara ya uwekezaji viwanda na biashara.
Mheshimiwa Spika, tatu nishukuru sana viongozi wetu Wakuu, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu lakini pia nikushukuru sana na wewe Mheshimiwa Spika, Naibu Spika lakini na Wenyeviti wa Bunge hili lako tukufu kwa kuendelea kusimamia na kuhakikisha tunatekeleza na majukumu yetu vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Waziri wangu Dkt. Ashatu Kijaji Kwa kuendela kunisimamia vizuri na kunielekeza katika kutimiza wajibu wangu. Naanza kushukuru sana Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara Kilimo na Mifugo kwa namna
pekee mwenyekiti wetu Mheshimiwa Kihenzile lakini pia na Makamu na wajumbe wote. Pia kwa namna ya pekee niwashukuru sana wajumbe wa kamati lakini pia na waheshimiwa wote Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendela kushirikiana nasi katika sekta hii ya uwekezaji, viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bajeti iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri imebeba dhamana kuu ya kuendeleza kasi ya uwekezji na ujenzi shirikishi na unganishi wa uchumi wa viwanda kwa kutambua nafasi ya sekta binafsi kama injini ya ujenzi wa viwanda na shughuli za ubia kwa sekta binafsi na umma na hii dhahiri kuwa mfumo huu na maboresho mengine yanayoendelea katika nchi hii ikiwemo utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara Mkumbi au blue print unalenga kuboresha mazingira ya biashara na kuchochea hali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kuleta maendeleo endelevu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa na mimi nichangie hoja kwa kutoa maelekezo au ufafanuzi kwa baadhi ya hoja zilizowasilishwa kuhusiana na Bajeti ya uwekezaji, viwanda na biashara kwa mwaka 2023/2024.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara Kilimo na Mifugo imetoa maoni mengi na maelekezo katika maeneo kadhaa na ambayo kimsingi mengine yameshatekelezwa na yanaendelea kutekelezwa ikiwa ni matokeo ya kazi kubwa ya kamati hii kutuwezesha sisi kama wizara kutekeleza majukumu hayo. Mosi, ni kuhakikisha tunalipa fidia ya eneo lile la mradi huu mkubwa ambao umeongelewa na wabunge wengi Mchuchuma na Liganga.
Mheshimiwa Spika, tunashukuru Serikali ya Awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upenzi mkubwa kuhakikisha sasa anaweka historia kama ambavyo Wabunge wamesema kwamba sasa tunaweza kutekeleza mradi huu ametoa hizo fedha bilioni 15.4 ambazo zinaenda kulipa fidia ya wananchi wale ambao sasa ni hatua ya awali ya kutekeleza mradi ule mkubwa katika mkoa wa Njombe katika Halmashauri ya Ludewa. Ambapo tunaamini katika zoezi hili la kulipa fidia, mosi ni kitu kikubwa uchumi wa nchi hasa wana Ludewa, lakini pili tutatoa elimu ili fedha hizo malipo haya yanayolipwa yawe na faida yawe na manufaa ili wananchi wale waweze kutumia vyema na siyo baada ya hapo warudi tena kwenye umasikini kama ambavyo baadhi ya wabunge walisema katika maeneo mengine fidia hizi zikilipwa wananchi wale wanatumia fedha vibaya halafu wanarudi kwenye hali ngumu na kuwa masikini zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Mheshimiwa spika, pili kulikuwa na suala la kiwanda la viuwa dudu. Tunajua changamoto kubwa ilikuwa ni kuona namna gani kiwanda kile kinaendela kuzalisha kadri ambavyo kilipangwa na sisi kama Serikali tumeishakubaliana kupitia Wizara ya Afya lakini na wenzetu TAMISEMI kuhakikisha lile soko la awali ambalo ni sisi watanzania kutumia dawa zile zinatumika na katika mwaka huu wa fedha tunaenda kutekeleza hayo lakini zaidi tunatafuta masoko ya nje, zaidi na haya yameshaanza na tumeanza kuuza katika badhi ya nchi dawa hizi katika nchi za majirani kwa upande wa SADC na EAC na tunaamini kiwanda hiki kwa mwendo huu wa mauzo sasa na utaratibu unaokwenda kwa kuzalisha viuwa wadudu lakini viwatilifu na amini kwa kuwa sasa fedha zimeanza kupelekwa katika kiwanda hiki na uzalishaji umeanza na kwa historia ya kwanza walikuwa wanapewa fedha na Serikali.
Mheshimiwa Spika, lakini sasa hivi kuanzia mwaka huu wa fedha wameanza kujilipa wao kutokana na mapato ndani ya kiwanda hicho, kwa hiyo tunaamini huko tunakokwenda tukikamilisha haya tutaweza kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Spika, lakini kulikuwa na hoja ambazo Kamati ya Kudumu ilielekeza kuhusiana na eneo la Engaruka nalo hili tunalifanyia kazi na kutakuwa na fidia kwa wananchi zaidi ya 599 ambao tukisha kamilisha uhakiki kama ambavyo tumeanza kwenye Mchuchuma na Liganga na huku pia tutaenda kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Spika, vilevile kulikuwa na hoja ya nini tunafanya kuhakikisha Shirika letu la Maendeleo la Taifa NDC wanaendelea kutimiza wajibu wao au uwepo wao. Nitoe taarifa kwamba Shirika letu la Maendeleo ya Taifa NDC kwa sasa lina jumla ya miradi 13 ambayo moja ni hili la Mchuchuma na Liganga lakini kuna Mradi wa Engaruka Soda ash au Magadi ya soda lakini Maradi wa Makaa ya Mawe Ngaka ambako ndiyo kuna ile Kampuni ya Tancol Mheshimiwa Kapinga amesema.
Mheshimiwa Spika, pia tuna Mradi wa Chuma Ghafi cha Maganga Matitu lakini tuna kongane za viwanda lakini zaidi pale TAMCO, Nyanza Grass, Kange na KMTC lakini pia tuna Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools pale kwa Mheshimiwa Saashisha Mafuwe, tuna Kiwanda cha Mang’ula Mechanical Machine Tools ambacho hiki kilikuwa mboni ya viwanda vile ambavyo vilikuwa vimebinafsishwa amavyo tumevirudisha Serikalini kikasimamiwa na Shirika letu la Maendeleo ya Taifa NDC lakini pia tuna Mradi wa Bandari Kavu ambao unaendelea lakini pia Kiwanda hiki cha Viua dudu pale Kibaha na Mradi wa Umeme wa Solar Singida, Mradi wa Upepo Singida lakini pia tuna Mashamba ya Kihui na Kalunga ambayo ni Mashamba ya Mpira.
Mheshimiwa Spika, katika miradi hiyo 13 miradi ambayo inaenda vyema kwa sasa au tunatekeleza kwa hatua ya awali ni mitano ambayo inafanya kazi ikiwemo ni kongane za viwanda pale TAMCO Nyanza grass kiwanda cha Machine Tools Mradi wa Bandari Kavu lakini pia Kiwanda cha Viua dudu na Mashamba ya Mpira ya Kiuwi Muheza Mkoa wa Tanga lakini pia Kalunga Kilombero Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kuanzisha Kituo cha Ugavi wa Biashara cha Kurasini au Kurasini Logistical Centre. Ni kweli mradi huu ulikuwa utekelezwe chini ya Wizara lakini ninyi ni mashahidi kutokana na msongamano mkubwa pale bandarini, kwa hiyo, kulikuwa na maelekezo maalum kwamba sasa lile eneo liweze kutumika katika upanuzi wa huduma ya bandari pale Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, lakini mradi ule bado unaendelea na dhamana ya kuendeleza mradi ule ni kuhakikisha kituo hicho cha bishara ya ugavi kinafanya kazi chini ya mamlaka yetu ya EPZ. Na dhamira hiyo bado ipo kwa sababu, tulikuwa na changamoto na sasa bado tunayo changamoto ya masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo chai.
Mheshimiwa Spika, na kwa sababu hiyo, mradi huu mpango wake ni kuhakikisha tunatumia eneo lile la Bandari Kavu la Kwala, ambapo kule sasa kutakuwa pamoja na viwanda vingine, lakini pia kutakuwa na hii agro-processing na mambo mengine ambayo yatatekelezwa katika eneo lile la Kwala. Kwa hiyo ule mradi haujafa, lakini tumehamisha eneo kwa sababu ya umuhimu wa Bandari yetu pale Dar-es-Salaam ili iweze kufanya kazi vizuri kupunguza msongamano ambao nao ni changamoto kubwa katika kuhakikisha uchumi wa nchi hii unasonga mbele.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya lumbesa. Nitoe taarifa, kulingana na kanuni na sheria kwa kutumia Sheria ya Vipimo Sahihi na Kanuni za Ununuzi na Uuzaji wa Mazao, The Weight and Measures Act, tunataka vifungashio visizidi kilogram 100 pamoja na kiasi cha uhimilivu asilimia kama tano. Na kwa mujibu huo kwa hiyo maana yake tafsiri sahihi ya ufungashaji ni kwamba tusifungashe tofauti na vifungashio ambavyo vimewekwa, iwe ni kilo 100 au ni chini ya hapo.
Mheshimiwa Spika, na kwa sababu hiyo, tumesema lumbesa, kwa maana ya kuongeza kilemba au kofia ni marufuku kwa sababu inaleta dhana potofu ya kuwalinda au kuwanyonya wakuluma au wazalishaji wa mazao katika nchi yetu. Kwa hiyo tutahakikisha tunasimamia sheria hiyo.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, tumeshakubaliana Wizara yetu, Wizara ya Kilimo na wenzetu TAMISEMI, ambao wao ndio wako kule kwenye masoko, kuhakikisha tunakuwa na collection centers au masoko, maeneo ambako kutakuwa na uuzaji wa bidhaa au mazao haya ili kuhakikisha vipimo sasa, ili Wizara yetu kupitia wakala wa vipimo wawe na mizani pale ambayo itawasaidia kupima mazao haya yanayouzwa kwa wakulima au kwa wanunuzi badala ya wanunuzi kwenda mashambani kwa wananchi au wakulima na kuwanyonya. Kwa hiyo, hili ni elekezo; na tumekuwa na fine kadhaa kwa wale ambao wanakiuka sheria hii.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala la uhuishaji wa leseni. Kwa mujibu wa Sheria ya Leseni za Biashara, leseni zote za biashara kundi A na B zinatakiwa kuwa hai muda wote. Kwa hiyo, kwa sasa tunahuisha kwa sababu ziko manually, tunakokwenda tutaenda kwenda automation kwa maana ya kuwa electronic. Hiyo itatusaidia kuhakikisha tunafuatilia kwa urahisi zaidi. Tunaamini hata kama kutakuwa na gharama basi itakuwa ni ndogo zaidi kuliko hivi sasa, lakini badaye kadiri maendeleo yanavyoenda tunaamini hii tutaitoa ili kuhakikisha biashara inafanyika vema na kupunguza usumbufu kwa wafanyabiashara.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala la uingizaji wa bidhaa mbalimbali, vikiwemo vyakula hapa nchini, kuhakikisha tunasimamia ubora wa bidhaa hizo. Ikumbukwe kuwa madai ya uwepo wa mchele wa plastic si jipya na lilishakuwepo hata huko nyuma, lakini kupitia taasisi yetu, shirika letu la viwango, tumepitia na kubaini kwamba bado si taarifa sahihi. Lakini tutaendelea kufanya hivyo pamoja na vyakula vingine au bidhaa nyingine ambazo hazina ubora ili viweze kukidhi viwango ambavyo tumejiwekea kama nchi na kuhakikisha wananchi hawadhuriki kutokana na bidhaa ambazo hazina viwango.
Mheshimiwa Spika, kuliongelewa kuhusu masuala ya ubunifu. Nitoe taarifa kwamba, kulingana na mwongozo wa ubunifu ambayo ni Sheria ya COSTECH, Sura ya 5, ambao wameanzisha Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia; mfuko huu tayari umesaidia wajasiriamali wengi kupitia COSTECH, lakini pia TIRDO; na Waheshimiwa Wabunge wengine wamefika pale TiRDO; tunawalea vijana hawa. Kuna wengine ambao kwa mfano wabunifu wa mita za maji, hapa Dodoma, Mvumi, lakini pia kuna wengine wazalishaji wa mbolea ambayo inatumika kwenye parachichi na wengine. Tunaamini Serikali inaendelea kuwapa motisha na kuwapa fedha, na wengine wamepata fedha kupitia Global Fund, ambao wanajihusisha na utekelezaji wa ubunifu mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tunaendelea kuwalea wabunifu na tutaendelea kuhakikisha wanapata uwezeshaji zaidi kadiri ambavyo tunaendelea na maboresho haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ya kulinda viwanda vya ndani. Lazima sisi kama nchi tujielekeze kuhakikisha tunalinda viwanda vya ndani. Na sisi kama Wizara tumeshaanzisha mchakato wa maandalizi ya Sera ya Taifa ya Ushiriki wa Watanzania kwa maana ya a local contents policy.
Mheshimiwa Spika, sasa kuliongelewa kuhusu kiwanda cha magari pale…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Dakika moja, malizia Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa hiyo, tunaenda kuwalinda wazalishaji wa ndani.
Mheshimiwa Spika, lakini nimalizie kidogo kuhusu hoja ya pombe zinazotengenezwa kienyeji. Kama utaruhusu kwa dakika moja niweze kuelezea kidogo nini tunafanya. Kwa mujibu wa viwango vya pombe kali, pombe kali inapaswa kuwa na kiwango cha pombe, ethanol, kuanzia asilimia 37 hadi 42 volume, ambayo inammanisha kwamba mchanganyiko wa pombe na maji na haipaswi kuwa kiwango kikubwa zaidi ya hapo. Sisi kama Wizara tumeendelea kusaidia wazalishaji wa pombe hawa wa ndani, wa kienyeji, wengi ikiwemo na mimi kule nyumbani kuna pombe ya ulanzi, tayari wameshapata ithibati ya kutengeneza. Pia kuna Kampuni moja ya Businde Distillers, Rubisi, kule karagwe, tayari wamepitishwa kupitia Wizara hii kwa kusaidiwa na TIRDO, TBS na SIDO, ambao wanawasaidia.
Mheshimiwa Spika, tunaamini wajasiriamali wengine kupitia SIDO wajiandikishe na sisi tutaendelea kuwasaidia kuhakikisha kwamba nao wanazalisha kwa tija, ili kuondokana na dhana kwamba hatuwalindi wazalishaji wa ndani na hasa kwenye sekta hii ya vinywaji ambayo inachangia pato kubwa sana la Taifa kwa maaba ya kodi katika uchumi wetu wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda na mimi nakushukuru sana kunipa nafasi. Baada ya kusema hayo machache naomba kusema naunga mkono hoja na ninaomba Waheshimiwa Wabunge wote tuweze kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri, ili tuweze kutekeleza majukumu yake katika mwaka wa 2023/2024. Naomba kushukuru kwa nafasi hii. (Makofi)