Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Kilimo. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu, Samia Suluhu Hassan, kwa kweli anatuheshimisha sana Wabunge kila tunaposhauri humu anachukua hatua. Tulishauri kwamba Wizara ya Kilimo iongezewe fedha, tunaona mzigo umemwaga hapo bilioni 970, kwa kweli tunampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watenda kazi wote wa Wizara hii, kwa kweli wamekuwa wabunifu na wanafanya vizuri. Sio hivyo tu, nampongeza nimepita kwenye hotuba hii kwa kweli watu wa Hai tunasema ahsante sana, tumeona Bwawa la Mtambo pale wanaenda kutengeneza skimu yetu, lakini tumeona wametuwekea fedha kwa ajili ya kwenda kufanya upembuzi yakinifu kwenye Bwawa letu la Bolutu na ile Skimu ya Metrum. Pia nimeona wametuwekea kwenye mpango barabara zinazoelekea Soko la Kwasadala tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze leo taratibu sana. Nimekuwa nikizungumza hapa kuhusu matatizo ya ushirika, sasa sijui huwa naongea kwa haraka, leo nataka niongee taratibu Mheshimiwa anielewa, taratibu kabisa. Nilizungumza hapa matatizo ya ushirika, akaenda Waziri wakati huo akiwa Naibu Waziri kule Kilimanjaro Akafanya tathmini ya mashamba 20, akabakiza mengine 20. Yale aliyofanyia tathmini akagundua yale ninayozungumza ni kweli na taarifa yake hii hapa, ameandika mwenyewe hii, kwamba kuna matatizo, lakini nauliza hivi huu ushirika matatizo yataisha lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunazungumza taarifa ya Waziri imeeleza wanafahamu matatizo yaliyoko kule, leo tunazungumza Shamba la Makoa, nilizungumza hapa mwekezaji anatuchezesha pale shere yaani amewekewa zuilio na Mahakama kwamba asiendeleze, leo watalii wanaendelea kule. Hana kibali cha kufanya biashara ya utalii, Halmashauri ya Wilaya ya Hai haipati chochote, hakuna tunachonufaika nacho na ana kiburi cha hali ya juu. Sijui ni nani yuko nyuma ya huyu mtu. Ni nani yuko chini ya Elizabeth huyu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe ifike mahali Serikali na Wizara zinazohusika wote wanafahamu, Waziri wa Utalii anafahamu, alishaenda mpaka kule kwake tukatembelea akaona uhuni anaofanya pale, lakini huyu mtu anaendelea. Naomba hii ifike mwisho. Chama cha Msingi Mrososangu Waziri anakifahamu, tulihangaika wote, lile shamba likarudi mikononi, tunataka tumpe mwekezaji atuwekee kiwanda cha parachichi na lenyewe linaingizwa siasa. Wananchi wa Jimbo la Hai tumerudi nyuma kiuchumi, vyama hivi vya ushirika ndivyo vimetusomesha, ndio vimefanya maendeleo kule kwetu. Tunatamani ushirika ukue tena, lakini watu wachache wanaturudisha nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tumepata mtu ameonesha nia ya kujenga kiwanda kikubwa cha parachichi ikiwa ni zao ambalo litaenda kuinua uchumi wa watu wa Hai kama eneo mbadala kahawa yetu imeshaisha, amezungumza Mheshimiwa Maleko hapa, lakini maeneo ya mashamba yetu ni machache.
Kwa hiyo, kwa tathmini yetu tukaona zao la parachichi linaweza kutusaidia, tunapigwa maneno. Niombe Mheshimiwa Waziri asimame tunataka kiwanda. Kiwanda chetu na kahawa yetu yule mwekezaji akija asiguse, lakini ajenge kiwanda cha parachichi, tafadhali sana na lisichukue muda. Hili naamini Mheshimiwa Waziri analiweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mkuu kuna mgogoro, Lyamungo kuna mgogoro, Narumu kuna mgogoro, hivi hii migogoro itaisha lini? Nami niseme kuna makosa ambayo tulifanya pengine. Zamani vyama vya ushirika vilikuwa vinaenda vizuri kwa sababu wale viongozi wa ushirika na wale makatibu wa ushirika walikuwa wanatokana na sisi wenyewe. Walipotuletea watu wanaitwa Maafisa Ushirika ambao hawana uchungu na sisi, hawajui kahawa yetu inalimwaje, wao ndiyo wanakuwa ndiyo wapiga dili mwanzo, mwisho. Ni siasa tu, wanaingia huku wanaenda huku, lakini hakuna kinachofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe leo si nimejitahidi kuongea taratibu, Waziri si amenielewa? Hebu amalize jambo hili. Namwomba sana, amalize jambo hili, Waziri ni mbunifu, mbona hili dogo tu linamshinda? Kila siku tuzungumze jambo hilo hilo? Ametuletea skimu za umwagiliaji hizi hapa, sasa tunaenda kulima wapi na Waziri anajua hatuna mashamba. Tunategemea hayo 17 yaliyoko kwenye ushirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabisa chonde chonde Waziri amalize jambo hili. Naunga hoja mkono kabisa wala sishiki shilingi kwa sababu ametuwekea hela humu, lakini amalize hili jambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, linalofanana na hilo, siku hizi kuna watu wanaitwa Bonde la Maji Pangani. Hawa jamaa na wao wawapelekee fedha. Nafikiri wanakusanaya hela kwa njia ambazo siyo sawa. Sasa hivi kwa Mkoa wa Kilimanjaro wale wawekezaji wakubwa ndiyo wanaopewa maji. Sisi wakulima wadogo hatupati tena maji. Kwa hiyo, mgawanyo wa maji hauko sawa. Naomba hiki chombo hiki wakipelekee hela, wanapiga dili kwa sababu hawana hela. Wawatengee hela ili waweze kufanya kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine hivi kwa nini suala la mbolea linakuwa kama biashara ya bangi? Yaani mbolea tunakimbizana nayo hivi, Mheshimiwa Waziri anaona nilivyomsumbua kupata mbolea. Nashukuru leo nimeambiwa ndiyo imeingia mbolea. Wananchi wa Hai wanataabika kwa sababu ya mbolea. Niwaombe, waweke utaratibu mzuri kama alivyoshauri Mheshimiwa Olelekaita, muda wangu unaisha, wahakikishe kwamba mbolea zinakuja kwa wakati na lazima wajue sisi kule Hai sasa hivi ndiyo watu wanalima. Hii misimu ya kilimo inatofautiana kulingana na mazingira, waweze kutambua eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe nimtajie leo Waziri skimu ambazo ataondoka nazo. Tuna skimu 25 za umwagiliaji. Mheshimiwa Waziri akitupa hizi zikajengewa, sisi tunamuahidi tutalima kwa nguvu na anajua sisi watu wa Kilimanjaro ni wachapakazi. Naomba Metrum nimeiona hapo, lakini naomba Kalali, pale Mfereji wa Kalali uende ufanye nao kazi. Mfereji wa Mbwera, Mwanamganga, Mshara, Muro, Mfereji wa Mriri, Uru, Sufi, Mfereji wa Isuke, Mfereji wa Maisawa, Mfereji wa Maswai, Mfereji wa Sanya Stesheni, Kwamaleko, Kimashuku, Kingereka A, Mapacha A, Kikafu Chini, Mfereji wa Mwasha, Mfereji wa Isimai na mingine iliyoko pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachomwomba Waziri, aliniahidi hapa kwamba atanipa shilingi bilioni moja, nami nikaenda kwa watu wa Hai nikasema Mheshimiwa Bashe siyo mwongo, tunaletewa shilingi bilioni moja kwa ajili ya skimu zetu, hazijafika. Naomba hizo hela zije ili sisi tutengeneze skimu zetu, tumletee Waziri mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ninalomshauri Waziri hapa, nimeangalia mahitaji yetu ya mahindi. Hili jambo Waziri alitazame vizuri. Haya mahindi tunagawana na mifugo. Kwenye Wizara ya Mifugo hawajatenga mahali kwa ajili ya chakula cha mifugo. Haya mahindi ndiyo wanayoenda kubadilishwa yanatengenezwa chakula cha kuku, wakati ukienda kwenye bajeti ya Waziri anapanga haya ni mahindi kwa ajili ya binadamu tu, lakini yanapotoka ukisikia kuna njaa haya mahindi tunagawana nayo. Tunasema pale Hai tunapeleka tani kadhaa, zikiingia mtaani zile tani tunagawana zinaenda kutengenezwa chakula cha kuku, zinaenda kutengenezwa chakula cha ng’ombe. Kwa hiyo niombe ama Wizara ya Kilimo au ya Mifugo itenge maeneo maalum kwa ajili ya chakula cha mifugo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Hiyo ni kengele ya kwanza au ya pili?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze suala la...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, hiyo ni kengele ya pili.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Basi naomba kutoa hoja.
NAIBU SPIKA: Kutoa hoja? Unga mkono tu.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naam?
NAIBU SPIKA: Unga mkono.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)