Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika nchi yetu; na hilo wala halina ubishi kwa sababu hata ukisikiliza kwenye redio za nje, TV za nje Dkt. Samia ni mwamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye hoja hii na nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Bashe na Naibu wake. Kwa sababu ya muda, tunajua wote wanafanya kazi nzuri, lakini tunao wajibu wa kuendelea kumshauri ili aendelee kufanya kazi. Sasa yako maswali ambayo pengine hata nikimuuliza leo Mheshimiwa Waziri pengine atashindwa kunijibu lakini ninaamini atakuja kuyajibu baada ya kuwa amefanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo moja wapo ni eneo la uzalishaji. Ukiangalia kwenye hotuba yake anasema ilitarajiwa tuzalishe zao la korosho tani 400,000 lakini hadi Aprili tumezalisha tani 182,270. Sasa sababu aliyoitaja amesema kwamba uzalishaji umepungua ama umekuwa mdogo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, inaweza kuwa. Lakini hapa nilikuwa mimi najiuliza, pamoja na wakulima wengine wa korosho; kwa msimu uliopita nadhani umefanikiwa sana; kwamba sulphur ya unga wakulima wa korosho waliipata kwa takribani asilimia 60 ikiwa ni tani 15,000 na dawa ya maji zaidi ya milioni 2.6 sawa na zaidi ya 100%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapo tulitarajia, na wakulima walionufaika ni takribani 483,000 sasa ukiangalia nguvu uliyoitumia na wakulima waliopata hizo pembejeo tulitarajia uzalishaji uongezeke lakini badala yake uzalishaji umepungua. Kwa hiyo yapo maswali ya msingi; tunadhani nini hasa kilichotokea? Ndiyo maana, kwa vile hatuna majibu ya utafiti, hakuna study zilizofanyika ndiyo maana wakulima wanasema zile sulphur ama zile pembejeo ambazo ulitupatia hazina ubora. Siwezi kuthibitisha kwa sabbau bado study haijafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunasema hivyo? Kwa sababu dawa zingine ulivyokuwa ukimaliza tu kumwagilia ama kupuliza kwenye ile mikorosho, mikorosho inanyauka na maua yanadondoka. Kwa hizo hoja na ndiyo maana tunaona pengine kuna walakini kwenye dawa ama pembejeo ama viuatilifu vya korosho ambavyo tumetumia mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye hilo eneo pia mimi bado nina swali. Zamani wakati sisi tuko wadogo tulikuwa tunatumwa Kwenda kuokota korosho na reki, tulikuwa hatuokoti moja moja hivi lakini enzi hizo wataalamu hawakuwepo na dawa hazikuwa zinapatikana hivi, hivyo kwa mkulima wa kule Tandahimba wa kule Malokopareni kwetu Masasi ukimpa dawa ukimpa sulphur yeye anaenda kupiga tu kuanzia pale inapotakiwa kwenye kalenda. Je, wataalamu wetu wapo wa kutosha wa kutuambia kwamba huu mkorosho kwa sasa hauumwi? Hivyo binadamu anapotumia dawa kila siku hata kama haumwi kwa vyovyote vile atakufa. Je, mimea mingine ambayo tunazalisha kwenye mazao ya kimkakati inapewa dawa kila siku? Hayo ni maswali ya kujiuliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la pili, kuhusu bei. Msimu uliopita Mheshimiwa Waziri ni shahidi, wakulima wamelalamika sana. Bei aliyoipata mkulima mkononi, acha ile ambayo pengine ndio iliyokuwa inatolewa kwenye mnada, ile pesa ya mkulima mkononi. Sisi kwenye chama chetu cha MAMCU ni 1,350 mpaka 1,400. Lakini wakati anachangia Mheshimiwa Cecil hapa makato ni 1,100 sasa ukijumlisha hapo utapata bei ya korosho. Bei hii ni duni bei hii ni ya kutupa, bei hii haimlipi mkulima kwa kazi ya korosho ambavyo inavyokuwa kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa ndipo tunapoomba sasa sekta mbalimbali ama Wizara zisomane. Ijumaa tumemaliza Wizara ya Viwanda na Biashara, kama zingekuwa sekta hizi zinasomana pengine kazi yako ingekuwa ni nzuri na ingekuwa ina tija. Kwa sababu sisi kwenye korosho kuna ile korosho ambayo ndio tunalalamika inauzwa ghafi kwa sababu suala la viwanda tumeshasamehe, tumesahahu kwa sababu tunaona huo ni ugonjwa mwingine tunauacha pembeni. Lakini kama tungekuwa tunauza ile korosho halafu tunauza na lile bibo kwa ajili ya kutengeneza mnyororo wa thamani, kwamba zile pombe alizokuwa amezileta Mheshimiwa Condesta hapa tungetengeneza kwa mabibo ina maana zao la korosho kwetu sisi lingekuwa lina tija kubwa, kwa sababu tungeuza ile korosho na yale mabibo yangeweza kutengeneza pombe ndani na hivyo mkulima wa korosho angendela kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nina uhakika hata wabunge wengine wakitoka wakienda Mtwara sasa hivi watajiuliza, hivi hawa Wabunge wa Mtwara miaka nenda rudi wamekuwa wakisema wao zao lao ama dhahabu yao ni korosho, watakuta umasikini uliokuwepo kule ni kwa sababu mnyororo wa thamani huu haujafungamanishwa. Mimi niombe sana, najua Serikali yetu ni Sikivu, wizara zisomane ili na Mheshimiwa Bashe na wewe uvunje, uweke rekodi tuone namna ambavyo wakulima wa korosho tutainuka kupitia Wizara yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo i nilikuwa najiuliza; hivi ni kweli Serikali inaweza kumaliza kangomba? Inaweza? Kwa sababu kangomba kwa msimu uliopita watu wameuza korosho ama wamenunua kwa 2,000 halafu bei ya mnada ni 1,300 sasa mkulima ataenda wapi? Hivi kwa nini asiuze korosho yake kwa kangomba? Kwa sababu kangomba inauzwa 2,000 bei ya mnada mkulima anatoka na 1,300 tena anaisubiria benki mpaka anachakaa, tena juzi juzi tulivyoenda kwenye mwenge tukaambiwa kuna watu sijui wa benki yetu wakulima waliuza korosho mpaka sasa hivi hawajapata hela yao ndiyo maana sasa inakuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi moja ya maswali ambayo nitaomba uje utuambie, je, kangomba itaondoka kama bei ya korosho inaendelea kushuka kwa kiasi hiki? Kwa sababu hivi vitu lazima vyote vitakapokuwa vinashughulikiwa ukishughulikia jambo moja kwa uzuri ndivyo utakavyoondoa changamoto kwenye eneo lingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninadhani hilo ni eneo lingine ambalo Wizara hii itakapokuja kujibu hapa ituambie. Mimi sina shaka kwenye utendaji wa Mheshimiwa Waziri, nina uhakika akiyachukulia haya mambo yote kwa umakini inawezekana tukatoka hapo tulipo tukaenda kwenye hatua nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nisisitize suala la uatafiti kuhusiana na visababishi ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinapelekea zao la korosho kudondoka ni muhimu likazingatiwa. Nimeona bodi ya korosho imesambaza miche 11,000 kwa mikoa 13, nikajiuliza, sasa ilikuwa inapata 900,000 ama 800,000? Lakini hata nikipiga hesabu kwa wale wakulima 483,000 waliopata viuatilifu, nikafanya hesabu pale, nikasema kwa hiyo kumbe kila mkulima pengine angehitaji mbegu ya korosho au miche, angepata miche 0.022. Kwa hiyo ni kama vitu havioani hivi, yaani jitihada hiyo siioni kwa hiyo ni muhimu sana hayo mambo yote yakafungamanishwa Pamoja ili tuweze kuona tija ya zao la korosho na tuone kazi nzuri itakayokuwa imefanywa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja.