Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na kuwa mmoja katika wa wachangiaji katika Wizara hii ya kilimo. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja na pili niipongeze Serikali na nimpongeze Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kuwatetea wakulima wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza katika mambo manne, jambo la kwanza pongezi nimeshawapongeza Serikali na Wizara. Jambo la pili nitaelekeza maombi matatu. Jambo la tatu nitajielekeza kwenye ushauri na jambo la nne sintofahamu ambayo inaendelea kwangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza nimwombe Mheshimiwa Waziri, nimeona bajeti ya mwaka jana aliandika skimu za umwagiliaji. Nimshukuru kwangu uliniletea bwawa la bilioni sita Kata ya Goweko, lakini mpaka sasa hivi nimpe taarifa liko asilimia 15 na wanatakiwa kukabidhi mwezi Septemba. Kwa hiyo, nimwombe alisukume hili bwawa liweze kukamilika kwa wakati na upembuzi yakinifu wa mashamba uweze kufanyika, ili sasa kwenye msimu huu tuweze kuanza kuzalisha kupitia Bwawa letu la Goewko. Mwaka jana aliniwekea Skimu ya Umwagiliaji ya Mwamabondo na mwaka huu amenirudishia Mwamabondo Loya. Naomba hii skimu sasa Waziri aitengee fedha iende ikajengwe kwa sababu wananchi wa Loya wananiuliza kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nimeona hapa mpango wa kuchimba mabwawa mapya. Wilaya ya Uyui tuna majimbo mawili, uko mpango wa kuchimba bwawa kule Majengo, Tabora Kaskazini. Niombe wataalam wa umwagiliaji waende Kata ya Igalula, kule waonane na Mheshimiwa Diwani Hussein Simba, basi kuna sehemu nzuri ambayo wanaweza kuchimba bwawa na likaleta tija kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili, Mheshimiwa Waziri anafahamu wakulima wengi sasa hivi wanategemea mbolea. Palikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa mbolea hasa katika vituo vya upatikanaji wa mbolea. Mtu wa kutoka Makoesengi, Mmale, Lutende, Mwamabondo, kwenda kuifuata kilometa 200 mbolea ilikuwa ni adha kubwa sana. Serikali ilitakiwa itoe kauli kwenye hili, lakini kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alikuwa na nia thabiti, lakini kuna watu ambao walikuwa wanamkwamisha; niiombe Serikali, mwaka huu achukue fedha zake zote za mbolea ya ruzuku akae nazo, ili sasa a-deal na wale wanao-supply, isiwe kigezo fedha sijui imefanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali impe fedha zote za mbolea ya ruzuku Waziri wa Kilimo kwa sababu, mwaka huu wamewacheleweshea wakulima na wamesababisha upatikanaji mdogo wa mazao. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kusaidia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Wizara ya Kilimo itusaidie, watoe maelekezo kwa wanunuzi wanaowanyonya wakulima. Wakulima wananunuliwa na vipimo visivyokuwa sahihi. Sasa Serikali itoe maelekezo vipimo viwe vya aina moja, sana sana twende kwenye kilo ili kuweza kuwasaidia. Sasa kumekuwa kuna ngosha, kuna lumbesa, imekuwa vurugu mechi huko. Mtu anakwenda kununua hapohapo, ukimwambia akuuzie kwa kutumia hichohicho anakataa. Sasa kwa nini wakulima wetu waendelee kuibiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, Mheshimiwa Waziri anafahamu Kata ya Tula, Kijiji cha Kalangazi waliunda mpango wa kuweka block farm. Humu katika mpango wa Waziri sijaiona block farm ya Mkoa mzima, hajatenga sehemu yoyote ya mashamba makubwa. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Uyui lilipitisha azimio la kujenga block farm ya ekari zaidi ya elfu 11 na Mheshimiwa Waziri akiwa Naibu Waziri, alikuja pale, akatoa maelekezo ile block farm akaungana na wananchi wa Kalangazi, akaungana na Baraza la Madiwani na akatoa maelekezo ya kwamba, block farm lazima ianze hapa na akaahidi ataniletea tractor. Najua akinipa ahadi lazima nimdai. Naomba tractor lile nilipeleke kule haraka, ili sasa wananchi wakaendelee kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha ajabu na kushangaza na wananchi wanashangaa hapa, ndio maana nasema sintofahamu naiona hapa, sasa kama Waziri anatoa maelekezo, halafu Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa anakwenda tena anasema mimi sasa kutokana na sulphur inayotumika kwenye korosho sio nzuri, sijui nini, naombeni mlime alizeti; yakatoka tena maelekezo mengine ya alizeti. Halafu sasa baadaye tena akaja Mheshimiwa Waziri wa Mazingira tena, akasema kutokana na kutunza mazingira naomba tena tuweke mizinga ya asali, hao wote wateule wa Rais, kauli tatu hata hazieleweki; wa kwanza block farm, wa pili kulima alizeti, wa tatu mazingira weka mizinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe, Mheshimiwa Waziri ndiye alikuwa bosi kwa sababu, Mkuu wa Mkoa sidhani kama yuko juu ya Waziri, kama kauli ya Waziri alisema block farm ni korosho na Baraza la Madiwani likasema block farm ni korosho na kijiji kimesema block farm ni korosho, sasa sisi kama wananchi naomba kabla ya Bunge hili hatujalimaliza, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Ofisi ya Mazingira, Waziri wa Mazingira, wakae watoe direction nini kifanyike kuliko kukaa kimya. Wasipofanya hivyo mpaka tunamaliza Bunge, nikimaliza Bunge nitawaomba wananchi wangu wa Kata ya Tula, Kijiji cha Kalangasi, tukusanyike tarehe nitakayoisema, tutavamia lile shamba, tutafyeka, Waziri atakuta kule na tunaomba atuletee korosho na sisi tutakuwa tayari kupanda korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naiomba sana Serikali, kwenye hili sina mchezo kwa sababu kama tulipanga na Wizara mkakubaliana haiwezekani sasa ikawa kuna danadana, sasa hivi imebaki haieleweki! Mlisema tulime alizeti, wameenda kulima pale heka 80 ikapata gunia tatu! Hiyo ardhi inahitaji korosho, Mzee lete korosho tumalize kazi kwa sababu wananchi wanahitaji korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nilikuwa na mambo hayo matatu tu, ninakuunga mkono kwa kazi kubwa ambayo unaifanya, Bwawa la Goweko naomba uliwekee msisitizo ili liweze kufanya kazi kwa msimu huu ambao tunaendelea nao. Nakushukuru sana. (Makofi)