Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia. Kwanza, nianze kumpongeza Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na Wakurugenzi wa Wizara. Hapa ndipo ninapoendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwamba ametuteulia watu wazuri, watu wenye mtizamo, siyo msimamo. Kwa kweli, niliposoma hotuba ya bajeti, mimi binafsi nataka nikueleze kwamba, naunga mkono hoja ili huko mwisho kama dakika zinapungua niwe nimemaliza kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio chetu kikubwa ilikuwa ni kutatua tatizo la msingi. Tatizo la msingi ni ukame. Wakati wote wananchi wanalima, lakini hawana uhakika wa kuivisha. Kwa bajeti hii ambayo imelenga umwagiliaji kwa kiasi kikubwa, pamoja na kuchimba visima virefu kila Wilaya kwa ajili ya kumwagilia mashamba, huu ni mwarobaini kabisa. Kwa kweli unaweza ukaandaa mbegu, lakini mvua ya kuivisha isiwepo; unaweza ukaandaa mbolea, lakini mvua ya kuivisha isiwepo. Kwa hiyo, jambo hili la kwenda kuweka umwagiliaji mkubwa, tunakwenda kutatua tatizo la msingi. Hapa ndipo tunakwenda kukuza uchumi wa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo inatenga fedha na iko vizuri sana, tatizo hapa ni kupewa fedha za utekelezaji wa miradi hii ambayo wameiweka. Ndipo tatizo kubwa lilipo. Naiomba sana Serikali, tufike mahali tuwe tunaamua mambo makubwa, haya mambo ya mapinduzi ya kilimo. Kwa sababu ukiangalia leo, mimi nataka nikwambie, kule Magu, Busega, Kwimba walilima vizuri sana, mvua ikaishia Christmas, kwa hiyo, mahindi yote yakakauka kwa jua lililopiga miezi mitatu. Hakuna mavuno ya mahindi kwenye maeneo hayo. Kwa maana hiyo, njaa ipo. Hapa namwomba Waziri sasa aandae mahindi ya bei nafuu yaje yauzwe kule Magu, Kwimba na Busega kwa sababu wana njaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha tunapotenga fedha, tunaomba zipelekwe kwa wakati. Leo ukisoma vizuri ripoti ya Waziri, kuna miradi ya umwagiliaji ndiyo inaanza sasa, wakati tuko mwezi wa tano. Kwa hiyo, hapa tunachelewa wapi? Tuangalie kipaumbele chetu kwa sababu bila kuwa na kilimo endelevu, uchumi wetu bado utakuwa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napendekeza pia mfuko mwingine. Tuwe na mfuko wa umwagiliaji. Kama ambavyo tuna mfuko wa maji, kama ambavyo tuna mfuko wa barabara na hii tuweke tena Shilingi mia moja kwenye mafuta, tusiogope. Tatizo la Watanzania ni kuogopa. Tunaogopa wakati wananchi wetu wanakufa masikini! Hatuwasaidii. Naomba sana kwa sababu, kama tutaweka shilingi 100 tukapeleka kwenye mfuko wa umwagiliaji, maana yake ni kwamba tutatengeneza scheme za umwagiliaji za kutosha kila mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma sana. Ukiwa kule Jimbo la Magu, bonde la Bugando Chabula, mkono mwingine ni maji ya Ziwa Victoria; ukiwa kwenye Bonde la Nkwiji Lugeye mkono mwingine ni maji ya Ziwa Victoria; ukiwa kwenye bonde la Ngashe Nkwizu Ngongwa, mkono mwingine kuna maji ya Ziwa Victoria; ukiwa kwenye bonde la Magu pale Kandawe, mkono mwingine kuna maji, mita 300 maji; ukiwa kwenye bonde la Mwambanga kuja Sawenge, mbele yake kuna maji ya Ziwa Victoria; ukiwa Mwabuyenga kuna mto Simiyu; ukiwa kule Chandulu, kuna bonde zuri sana linaloweza kutengenezewa bwawa la maji ya kukinga, Kabila, Igombe na Mahaha vile vile. Sasa inauma sana; na ili tutekeleze, lazima tuwe na mfuko. Tunaogopa nini? Kwa sababu Watanzania ni hawa hawa ambao wanahitaji wawe na uchumi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye maduka yoyote, biashara zozote, viwanda vyovyote, hawauzi, hawazalishi kama ilivyotarajiwa. Maana yake nini? Ni kwamba mkulima ndiye anayekwenda kununua kwenye bidhaa mbalimbali. Akinunua kwenye bidjhaa mbalimbali huko, mfano akinunua mabati, kuna kodi ya Serikali; akinunua godoro, kuna kodi ya Serikali; akininua cement, kuna kodi ya Serikali; akinunua nguo, kuna kodi ya Serikali, huko ndiko kujenga uchumi na kupanua wigo wa kodi kwa Serikali. Kwa hiyo, naomba sana, tuje na mpango wa kuongeza Shilingi 100/= kwenye mafuta, tupeleke kwenye umwagiliaji pekee, tutakuwa tumemeliza matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulinda wakulima. Katika Bajeti ya Wizara ya Viwanda nilichangia, nami nampongeza Mheshimwa Waziri. Nchi yoyote duniani lazima ilinde wakulima wake. Nawe kwa sababu ni Mwenyekiti wa Bajeti, angalia vizuri, import duty ambayo tuliiondoa mwaka 2022 kwenye mafuta ya nje, iwekwe mwaka huu 2023, ili kulinda wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nakuomba sana kwa sababu wewe ndio unasimamia. Wakulima wote wa mazao yote hasa wanaochakata mafuta, wanapata bei ndogo kwa sababu sisi tulikubaliana hivyo. Tulikubaliana hivyo kwa sababu, hali ya mfumuko wa bei ilikuwa hivyo ili kuvusha kidogo mfumuko wa bei. Sasa hivi alizeti wamezalisha nyingi, pamba wamezalisha nyingi, yaani mbegu zote na mazao yote yanayotoa mafuta yamezalishwa kwa wingi sana. Ni lazima tuwe na wivu kuhakikisha kwamba tunalinda wakulima wetu ili kuhakikisha wanazalisha, na mabenki haya yanapata fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie tu kwamba, pamba haina ruzuku. Nimesema hapa, Waziri amesema atapeleka ruzuku kwenye mazao ya alizeti, (ngoja niangalie hapa) kwenye mazao ya alizeti, ngano na miche ya michikichi. Pamba haina ruzuku. Hatuna ruzuku ya mbegu, na hatuna ruzuku ya madawa. Pamba inajihudumia yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie tu ruzuku ya madawa, kwa sababu ndiyo tatizo kubwa ili wakulima wetu waweze kuzalisha. Halafu kuna tatizo kubwa, inapofikia mahali ile pamba inataka kuzaa, majani yanabadilika, yanakuwa brown. Nadhani kuna wadudu ambao wananyonya. Naomba tufanye research ya kutosha kwa ajili ya dawa hiyo. Wakulima wanalalamika sana kwa sababu hawana namna ya kuweza ku-control ugonjwa huo. Mwaka huu tulitegemea zao liwe kubwa, lakini litashuka kwa sababu ya mnyauko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nimesema sina shaka na Wizara yako, sina shaka na wewe Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, naomba…

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cherehani.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, wakulima wa pamba katika nchi yetu ni Mikoa 18, na mwaka huu malengo ni kuzalisha kilo milioni 350 na wametumia pembejeo bilioni 100. Kwa hiyo, hawana ruzuku wakulima wa pamba.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Boniventura, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa sababu kwa kweli anayesema kwanza ni mhanga, nami ni mhanga, na mikoa yote 18 ni wahanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake alisema tunazalisha tani milioni moja. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, wewe ni m-NEC; Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Fedha ni wa NEC, naomba tujibu Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ambavyo Mheshimiwa Rais wetu amekusudia kujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye ngano. Tunatumia fedha nyingi sana za kigeni kwenye ngano, lakini tuna maeneo potential ambayo yanaweza kulima ngano. Mkoa wa Njombe ni potential sana kwa kulima ngano, Katavi kuna eneo potential la kulima ngano, Arusha, na maeneo mengine. Lazima tuamue kama Taifa. Hivi tutagiza malighafi kutoka nje mpaka lini? Kwa nini tusiamue? Hivi tukisema, baada ya miaka mitatu, wale wanaoagiza sasa waanze kulima mashamba makubwa, wapewe mashamba, watapanua ajira, watafungua uchumi kwenye nchi hii ili baada ya hapo miaka mitatu au minne tusiagize ngano nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linauma sana. Kama hatutaweka mwisho, tukaruhusu tu kuagiza agiza, mfanyabiashara anapenda tu kununua na kuuza. Mfanyabiashara hapendi kuwekeza kwa muda mrefu, kwa sababu ni gharama kubwa. Anataka anunue leo, auze kesho. Naomba sana, kwa Waziri aliyepo, Katibu Mkuu Gerard aliyepo na Wakurugenzi wa Wizara waliopo, naomba sana kama nchi tuzuie ngano baada ya miaka kadhaa, tulime ya kwetu ili kuhakikisha kwamba tunapanua uchumi na kuwekeza sana kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja tena kwa mara ya pili. (Makofi)