Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii ya Kilimo ambayo ndio uti wa mgongo kwa kuwa tumeona asilimia 65 ya wananchi wetu ni wakulima. Nami nianze kwa kuunga mkono hoja. Pia niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya, lakini kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima kwa jinsi ambavyo wanaitendea haki Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jinsi ambavyo utekelezaji wa mbolea katika majimbo yetu ulivyofanyika kwa ufanisi mkubwa sana. Ukisoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri inaonyesha kabisa kwamba upatikanaji wa mbolea umepatikana kwa asilimia 126, zaidi ya lengo ambalo waliokuwa wamejiwekea la kuingiza mbolea tani 650,000. Hii imetokana na kwa sababu waliingiza tani 617,000 kutoka nje, lakini 75,000 zilitoka ndani ambayo ni takribani kama asilimia saba tu ilitoka ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na mwenzangu aliyepita kusema mbolea ni usalama wa nchi na mbolea ni usalama wa chakula. Tumejionea wenyewe jinsi tulivyopata magonjwa ya mlipuko wa Covid na tuliingia kwenye adha kubwa ya kukosa mbolea lakini vita ya Ukraine na Urusi ndio imekuwa wimbo wetu kwamba imesababisha tumekosa mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni muda muafaka sasa kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya ndani ili kuepukana na changamoto hiyo. Hii ni pale tu ambapo tutaamua kupeleka ruzuku kwenye viwanda hivi, kwanza ili tuweze kuwapa motisha lakini kama mwenzangu alivyochangia tunaenda kupata hizi trickle down effect. Tutapata ajira, hela yetu itabaki humu humu ndani, pesa itazunguka ndani, tutapata ajira, watalipa kodi, lakini wananchi wetu watafaidika CSR ni hapa hapa ndani na wawekezaji wengine wa nje watafurahia kuja ili sasa tuwe na uhakika wa mbolea kutoka nchini mwetu ili hii asilimia 92 inayoagizwa kutoka nje, basi iwe ya viwanda vya ndani. Tunayo Minjingu, tunayo intercom, wawezeshwe kwa kuwapa motisha ili na wawekezaji wengine waweze kuvutiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tutaweza kuuza malighafi maana yake samadi tunayo nchini, gesi tunayo, phosphate tunayo, chokaa tunayo, kwa hiyo tutafaidika pia kuweza kuuza haya material yetu katika viwanda vyetu vya ndani na Serikali sasa itafanya kazi zingine kwa sababu kwanza watumishi ni wachache, kwa hiyo uratibu wote tutawaachia wafanyabiashara kwa sababu Serikali basically haifanyi biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hoja ya umwagiliaji. Ninapongeza Serikali kwa ajili ya umwagiliaji, taarifa imetuambia mabadiliko ya tabianchi yamechangia kuleta matatizo mengi. Ninaishukuru Serikali nimeona sasa hivi na mimi nimewekwa kwenye upembuzi yakinifu, niiombe Serikali kama kweli tunataka kupata kubadilisha kilimo hiki cha umwagiliaji basi tuende kwa vitendo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri ameonesha kabisa yeye ameshaingia mikataba 48 katika mikataba 69 ambayo ni asilimia 70. Kama ameingia mikataba ya shilingi bilioni 234 ni ukweli usiopingika kwamba miradi hii haijatekelezeka, na hii inathibitika kwenye taarifa ya CAG ambayo inasema Serikali imepeleka shilingi bilioni 48 tu sawa na asilimia 18 kwenye miradi ya umwagiliaji. Ndiyo maana hapa kila mtu anasema sijaona skimu hata mimi sijaona skimu. Mheshimiwa Waziri Kaka yangu Mheshimiwa Bashe nakushukuru nimepangwa kwenye upembuzi yakinifu kwenye skimu za Kigina, Muhambwe, Kumbanga, Nyendara. Ninakuomba skimu ya Nyendara naomba ifanyiwe kazi mapema, kwa sababu ilijengwa ikafikia nusu na sasa imekuwa ni majanga. Tumeshapata matukio ya vifo vifo sita pale maana it’s incomplete work, watu wanatumbukia kwenye ile skimu, niombe kama haiwezekani kuisha tufunike wananchi wa Muhambwe wamesema bora tufunike iwe hamna ili watu wasife, kuliko wananchi kutumbukia kwa sababu skimu ile haijaisha. Skimu ile ili iishe inahitaji shilingi milioni 300 mpaka 500 tu. Imefikia asilimia 80, niwaombe katika mpango huu nami niwekwe kwenye mkakati ili wananchi wangu wa Nyendara, wananchi wangu wa Kata ya Misezelo waweze kuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuiombe Serikali sasa kwa hali hii hatuna sababu ya kuendelea kutumia nguvu nyingi sana kusema kwamba Serikali imeongeza bajeti. Tutumie nguvu nyingi sana kuwaambia wananchi mnaona skimu, mnaona hiki, mnaona hiki itakuwa kazi rahisi sana kuliko kutumia nguvu nyingi kuwaambia bajeti imeongezeka. Wananchi wetu wanataka kwenda kuona uhalisia wa hii bajeti kwenye maisha yao ya kila siku kwa maana waweze kuzalisha kwa sababu ndiyo kazi yao ya kila siku. Kwa hiyo, naamini Mheshimiwa Bashe katika hili mtakwenda kunisaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninaipongeza Benki ya Kilimo nimeona imetoa mikopo kwa wananchi lakini wananchi wa Muhambwe hawajafaidika kwa sababu bado benki hii ina pesa kidogo. Naomba Serikali iiongezee mtaji ili na wananchi wa Muhambwe waweze kufaidika kupata vitendeakazi. Hatuna matrekta, hatuna magari, tunalima bado kwa jembe la mkono, ninaiomba benki hii iweze kuongezewa fedha ili sasa iwafikie wakulima wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye taarifa wakulima wadogo wadogo wamekopeshwa shilingi bilioni 60 tu ni ndogo sana kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, niiombe Serikali iwasaidie wakulima wadogo wadogo kwa kuongeza mtaji kwa benki hii ili wananchi wetu waweze kujikwamua na waondokane na hiki kilimo ambacho wanaona kwamba ni shida kwa sababu hawana vitendeakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba mradi wa BBT unakwenda kuleta mabadiliko kwa vijana wetu, lakini niungane na wenzangu, wale watu waliokuwa wanalima hiki kilimo ambao walikuwa wanahangaika wenyewe na wametulisha kwa miaka mingi waangaliwe pia kule kule waliko ili nao waweze kusaidiwa. Vijana wasaidiwe lakini na wale watu waliotutunza miaka yote wasaidiwe. Changamoto zao tunazifahamu nao tuwalenge kule kule waliko ili waweze kusaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu liko mpakani, ninaiomba Serikali kwa sababu mazao yetu mengi na hasa muhogo tunawauzia nchi jirani, niombe kusaidiwa maghala ili tuweze kutunza kwa sababu wale wa nchi jirani wananunua mashambani kwa hiyo wanawaibia wakulima. Niombe maghala ili wananchi wangu waweze kutunza mazao na tuwe na masoko ya ujirani mwema kwa sababu tutawauzia ile mihogo nchi jirani kwenye soko la pamoja. Nikipata maghala, nikipata soko, nikapata na vitendeakazi basi wananchi wangu wa Jimbo la Muhambwe watakwenda kufaidika na watakwenda kuzalisha kwa kiwango cha hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi naamini kwa haya machache, naunga mkono hoja kwa sababu kilimo ni uti wa mgongo wa Jimbo la Muhambwe. (Makofi)