Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja ya bajeti ya mwaka 2022/2023 Wizara yetu ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya kukibadilisha Kilimo cha Tanzania akiamini kabisa kwamba tukiboresha kilimo cha Watanzania maana yake ndiyo unaboresha uchumi wao na ni majority ya Watanzania ambao wanafanya kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nichukue nafasi hii kumshukuru tena Mheshimiwa Rais, nimshukuru zaidi Mheshimiwa Waziri Bashe kwa namna ambavyo watu wa Ikungi tulipokuwa tuna changamoto ya njaa ya upungufu wa chakula wakatuletea chakula cha bei nafuu. Tulipata chakula kile kilitusaidia sana na kwa hakika leo tunaenda kufanya mavuno chakula kile kimetusaidia tunashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kutupa kibali kupata NFRA wasogeze chakula pale kwenye Wilaya yetu na wananchi wale nilikuwa kwenye ziara siku mbili hizi wanatoa shukrani nyingi na wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo nichukue nafasi hii kushukuru kwa bajeti, kwa maana ya wasilisho la Mheshimiwa Waziri ambalo aliwasilisha pale jana, ni bajeti nzuri imeonekana kila mwaka inapanda, maana yake ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba kilimo kinakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda mbali ninahitaji nionyeshe tu kwamba kuna document kubwa yenye heshima ambayo nchi hii tumeipitisha, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 inaeleza wazi na inakazia sana suala la kilimo. Ukienda kwenye ile Ibara ya 35 inaeleza wazi kuhusiana na kilimo, imeweka tamko. Imeweka tamko kwamba kilimo cha kisasa ndiyo msingi katika kujenga uchumi na kina nafasi ya kimkakati katika kukuza ustawi wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi kwenye ilani imeeleza wazi kwamba makadirio mpaka 2025 tunapaswa tufikie Pato la Taifa tufikie asilimia 28 ya Pato la Taifa. Ukiangalia katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri tumewasilisha vizuri kwamba sasa tumefikia asilimia 26.1 maana yake tunaenda vizuri miaka miwili na nusu ijayo huenda tukafikia asilimia 28 ambayo iko kwenye lengo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri mnaenda vizuri niwapongeze sana wewe na wataalam kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya kwa sababu ni jambo ambalo litaenda kufanya vizuri, wananchi wengi zaidi ya asilimia 65 wanafanya kilimo. Maana yake ukiwagusa asilimia 65 ni kama watu milioni 40 wanafanya kazi ya kilimo katika nchi yetu. Kwa hiyo, nilitaka nianze na hilo ili kwanza kuonesha kwamba tunaona matokeo ya kweli yanaenda vizuri na ambayo kwa kweli tukiyasimamia vizuri na ushauri ambao tunatoa Wabunge huenda tukabadilisha kilimo chetu na kikawa kilimo chenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo ambalo ni mkazo uliowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi. Ilani ya Uchaguzi imesema ni kusimamia kikamilifu hifadhi ya matumizi endelevu ya maji, ardhi ya kilimo na kuongeza miundombinu ya umwagiliaji. Nataka nianze kwenye eneo la umwagiliaji. Ninaamini kabisa tabianchi imeathiri sana kilimo cha Tanzania, siyo kilimo cha Tanzania, cha maeneo mengi Afrika, kama tutaendelea na hali ya kusubiria huruma ya Mungu kuleta mvua peke yake hatutakisogeza kilimo hiki. Kila mwaka tutakuja na sababu kwamba mwaka jana hatukufikia lengo kwa sababu mvua hazikunyesha za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, ninaona kwamba kuna package nzuri kwenye eneo la skimu za umwagiliaji. Niombe huenda tunaweza kuweka fedha nyingi, kwanza tunaiona dhamira ya Wizara tunaiona dhamira ya Waziri, tunaiona dhamira ya watendaji lakini tunapelea kwamba fedha hata Wabunge wote wanaomba hapa skimu za umwagiliaji, lakini nani anaenda kuzitunza zile skimu kule chini? Skimu nyingi zimekufa, skimu nyingi hazisimamiwi vizuri. Skimu nyingi hazitoi matokeo lakini kama haitoshi kuna baadhi ya maeneo hata hawajui maana ya skimu zenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo maana yake tunaenda ku-dump fedha, tunaziacha pale, hakuna usimamizi. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tutafute mechanism nzuri ya kusimamia skimu ya fedha nyingi tunazopeleka kwa wananchi kule chini. Ninaamini tukifanya hivyo tutaleta matokeo tunayoyatarajia kwa sababu tusipofanya hivyo tutakuwa hatuna maana yoyote, tunawekeza fedha hakuna uendelevu wowote, maana yake hatuna matokeo ambayo tunayalenga. Tuna maeneo ya mito mingi, tuna maji yanapita kila mahali lakini tusipoyazuia maji na kuyatumia vizuri maana yake kilimo chetu hakiwezi kubadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili Mheshimiwa Waziri nikuombe sana tunajua kwenye Wizara yako umeniangalia katika skimu ya Mang’onyi pale, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri mliniambia kwamba mtafanya. Niombe wakati wa ku-wind up nataka kusikia watu wa pale Mang’onyi wanataka kusikia Wizara inasemaje. Mwaka huu wa Fedha tujengewe ile skimu tuboreshe kwa sababu sasa hivi tuna soko la mboga mboga katika Mgodi mkubwa wa Shanta ambao uko pale Mang’onyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri baada ya kuwa nimeeleza eneo la skimu ambalo litaleta matokeo nieleze kidogo kwenye eneo la transformation ya kilimo katika nchi yetu. Tukitaka ku-transform kilimo cha nchi yetu tunahitaji mambo matatu. Tunahitaji utaalamu kwa maana ya technology au elimu, tunahitaji uwekezaji au fedha lakini tunahitaji pembejeo ambazo zinafaa katika maeneo yetu. Mambo haya matatu tukifanya vizuri tutakibadilisha kilimo chetu. Leo ukienda kwenye utaalam ni Maafisa Ugani wangapi ambao wana uwezo wa kumsaidia mkulima pale kijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Maafisa Ugani wengi Mheshimiwa Waziri, wakulima wana uwezo mkubwa kuliko Maafisa Ugani uliowapeleka kule vijijini. Maafisa Ugani
wamefanana na wananchi lakini wengine wamezidiwa uwezo na wananchi, kuna haja ya kuwasaidia, kuwabadilisha mtazamo wa kazi wanazozifanya. Uwekezaji kama nilivyosema tunaiomba Serikali iongeze fedha za kutosha kwenye sekta ya kilimo ambayo watu milioni 40 wanafanya kazi hii, tukifanya vizuri eneo hili tutaweza kubadilisha kabisa kilimo na uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni eneo la mbolea, viuatilifu, na mbegu. Eneo hili tukiongeza utafiti, tukaongeza mbegu za kutosha zinazofaa, zitamfanya mkulima awe na matokeo makubwa kwenye eneo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nchi hii imekuwa sasa, kutoka Mtwara mpaka Kigoma watu wanataka wote walime zao moja linaitwa korosho, haiwezekani. Hatuwezi kuwa na kilimo cha korosho nchi nzima. Hata mazingira au hali ya hewa hairuhusu. Maana yake hata concentration ya namna ya kusaidia kilimo haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo kila mtu anataka kulima alizeti nchi nzima. Haiwezekani mtu atoke kule Tandaimba, anataka kwenda mpaka kule Mwanza alime alizeti, haiwezekani Mheshimiwa Waziri! Tufike mahali tuwe na kanda maalum kwamba hii kanda ni ya alizeti. Kama ni Singida, tu-concentrate pale Singida na mikoa ambayo inaweza kutoa alizeti. Leo hii mahindi hayawezi kulimwa nchi nzima. Mfano, kama Singida leo, hatuwezi wote kulima mahindi. Tutalima mtama, tutalima uwele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Parseko Kone, aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, alizuia kabisa kilimo cha mahindi kwenye maeneo ambayo hatuwezi kulima mahindi, akasema lazima watu walime mtama. Mtama ukizalishwa kwa wingi, nao ni nafaka, itauzwa, tutanunua chakula kingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwe wakali, tuwasimamie wananchi, tuwasaidie ili Ilani ya CCM iweze kutekelezwa vizuri, tuwe na usalama wa chakula na mwisho wa siku pato la Taifa liongezeke kupitia sekta hii ya kilimo. Tusipofanya hivyo Mheshimiwa Waziri, tutakuwa tunayumba kila siku, kila mmoja anakuja na proposal yake. Lazima sisi kama nchi, tukubaliane kwamba kanda hii ni chakula hiki, kanda hii ni zao hili, mwisho wa siku nchi ikikusanya, tutasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndio nilitaka niyaseme…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuunga mkono hoja, nawatakia kila la heri.