Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MARIAM D. MZUZURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Kilimo siyo lelemama. Kwa kuanza, naomba nimnukuu Mheshimiwa Waziri ukurasa namba mbili kwenye utangulizi namba nne. Anasema; “Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuanza utekelezaji wa mageuzi kwenye sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na maeneo ya msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni na kuitekeleza dhana na falsafa ya msingi kabisa kwenye kilimo kuwa “kilimo ni uwekezaji wa muda mrefu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumnukuu Mheshimiwa Waziri, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Tupo hapa Wabunge ambao tulikuwepo Bunge lililopita na Mabunge mengine nyuma. Tangu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia aingie madarakani kwenye Serikali ya Awamu ya Sita, na kumteua Mheshimiwa Bashe, kwa mara ya kwanza bajeti ya mwaka 2022 tulipongeza kwamba kilimo kimepewa fedha za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashuhuda. Leo hii nilikuwa napiga hesabu ya asilimia mpaka ikabidi niwaulize wenzangu, fedha za miradi ya maendeleo, tuliwatengea shilingi bilioni 569, zimekwenda shilingi bilioni 470. Pamoja na kasoro ambazo amezitoa mwenzangu, najua majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri yatakuja. Ni asilimia 82 na nukta. Haijawahi kutokea! Jamani, tupigeni makofi na tumpongeze sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bashe amekuta kilimo kipo ICU (Intensive Care Unit), ameomba pesa kwa ajili ya madawa amtibu mgonjwa huyu, mwelekeo tunauona. Nchi hii tatizo kubwa ni kwamba tunao wakulima ambao kwa asilimia kubwa ni peasants. Hatuna farmers, tuna peasants. Sasa hawa mpaka uwanyanyue, na ubaya zaidi Mheshimiwa Waziri kwenye Wizara yake ana sera na mipango, lakini Waziri huyu hammiliki mkulima. Mkulima yuko Halmashauri kule kwenye TAMISEMI, ndiyo maana amekaa anabuni mambo ambayo sasa mwanga tunauona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe moyo Mheshimiwa Waziri, hata unaposikia hapa watu wanasema, ooh, itakuwaje? Umetupa forum ya kuongea, kwa sababu umedhubutu na unafanya. Leo tunaongelea kwamba kwa nini tunaingiza sukari? Kwa nini tunaingiza mafuta? Kwa nini tunaingiza unga wa ngano? Tumeona hizo nchi tunazotoa hayo mazao wamefanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge wa vijana, Mheshimiwa Ng’wasi, ametoa mfano wa nchi ile aliyoitaja, namna gani imeweza kuendelea kupitia mashamba haya makubwa. Kwa hiyo, kwa kweli napongeza hatua hizi, tena nampongeza sana Mkurugenzi wa Tume ya Umwagiliaji, Ndugu yangu Raymond. Kwa kweli moyo wa kilimo sasa upo kwenye tume yako. Ameongea Mheshimiwa aliyetangulia kuchangia kwamba tumepeleka fedha nyingi kuweka miradi ya umwagiliaji, weka mfumo mzuri wa usimamizi hii miradi iweze kuwa endelevu. Tunaona hatua nzuri ambazo mnazifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kabla ya kwenda kwenye ushauri wangu kwanza, naomba niongelee Mkoa wangu wa Dodoma. Mimi kwa niaba ya Wabunge wenzangu wa majimbo, napenda kuwashukuru sana Wizara, mmetupendelea Dodoma. Sisi ndio tuna-pilot Mradi wa BBT pale Chinangali, na hapa ndiyo imeibuka sasa naiwaza hata Dodoma yenye utalii. Leo hii kutokana na jitihada zenu tunaenda sasa kuzungumzia kitu kinaitwa Agrotourism. Leo kwenye shamba lile la Chinangali nimeona Mheshimiwa Waziri mpango wako, pale kutakuwa kuna kiwanda cha wine, pale kutakuwa kuna restaurant, na uzuri umewaza kuweka private sector. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Msalato ikikamilika, mtalii akitoka nje, anashuka pale, anakuja Ikulu kuangalia, maana Ikulu tuna hadi wanyama mle, na pia atapita kwenye shamba lile kufanya Agrotourism. Vile vile ataenda Kondoa, tunayo michoro ya Kolo, tunayo Mkungunero kule, halafu ndiyo hapo ataenda Tarangire na Serengeti. Kwa kweli naunga mkono na ninawapongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi ya BBT kugusa kule Chinangali, Bihawana, Membe na Chemba kule Gwandi, pia miradi ya umwagiliaji tumeipata Chamwino zaidi ya mmoja. Tumepata kule Bahi, Mpwapwa, Dodoma Mjini, Chemba, hata Wilaya ya Kondoa imeguswa, lakini cha kusikitisha tu, kule Kondoa mmegusa Kisese tu ambayo ni Kondoa DC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina salamu kutoka kwa wananchi na vijana wa Kondoa Mjini, wanasikitika, mbona wao hujawakumbuka Mheshimiwa Bashe? Wanafahamu kwamba Diwani wao wa Kondoa TC ndiye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii. Naomba kule kwenye Halmashauri ya Kondoa Mji tunayo Mongoroma Irrigation scheme kwenye Kata ya Seria ambayo ina zaidi ya ekari 3,000. Tunayo Mlangu Block Farm Kata ya Seria zaidi ya ekari 1,000; tunayo King’ang’a Irrigation Scheme, Kata ya Kingare zaidi ya ekari 3,000. Ukija kujumuisha, naomba ukawaguse vijana hawa wa Halmashauri ya Kondoa Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya kazi kwa ukaribu kupitia Kamati, mimi nimshauri tu Mheshimiwa Waziri kuhusu mbegu. Naomba angalia namna ya kuwahusisha wakulima wadogo kwenye kuzalisha mbegu, na pia kwenye sekta binafsi. Huyu ASA nashauri abaki kwenye utafiti, abaki kuwa mdhibiti wa ubora wa hizi mbegu. Hebu kundi kubwa hili la private sector ulipe; tunao wawekezaji wazuri sana ambao wataweza kuwekeza na kuzalisha mbegu zilizo bora, wewe ukabaki kwenye kufanya tafiti na kudhibiti ubora wa hizo mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia kupitia uwekezaji mkubwa wa kwenye umwagiliaji. Leo hii kwa sababu hawa Maafisa Ugani wanasimamiwa na Wakurugenzi. Tumeona changamoto, wamepeleka vifaa lakini ufanisi wa vile vifaa hatuuoni, kwa sababu hauna usimamizi. Umeenda mbali Mheshimiwa Waziri, umewaza kupitia hii Tume ya Umwagiliaji, umeajiri wataalam 320, umeenda kujenga ofisi 121, na pia tumeona mmekabidhiwa magari pale na Mheshimiwa Rais. Hii yote umeona namna gani unaweza kuongeza usimamizi ili sasa uende ukawaguse wakulima wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie wakulima wadogo, mimi ni mkulima mwenzenu, hamjaachwa kuwa wanyonge. Ndiyo maana katika malengo ya Wizara hii, ni kupunguza umasikini kwa asilimia 50 ifikapo 2030? Nani wa masikini? Ni nyie. Mipango ipo dhabiti, na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri ametafuta mfumo mzuri wa kuwafikia na kuwasimamia, na kwa kweli tunamuunga mkono na tunajua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili linaongelewa kuhusu hii BBT. Jamani niwaambie, tunataka kuzalisha ajira mpya milioni tatu. Mnasema tukawafuate wale ambao wako kwenye kilimo, tunataka kutengeneza. Naomba nitoe ushuhuda. Mimi nilimaliza chuo mwaka 2009, nilienda kujiajiri kwenye kilimo. Nilikuwa msomi wa degree na nilikuwa mtoto wa kishua. Kwa jina langu tu ningeweza kutumia mazingira yangu kupata ajira, lakini nami nasema, natamani nijirudishe umri nyuma. Kipindi kile angekuwepo Rais Samia na Waziri Bashe, nami ningekuwa mnufaika wa hii BBT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu alitengeneza terminology ili kuvutia education, akasema education is sex. Mheshimiwa Bashe na Msaidizi wako Mavunde na wote Katibu Mkuu, Naibu Katibu na timu nzima, you are making agriculture sex, ili sisi vijana ambao ni kundi kubwa tuvutiwe na kilimo tuweze kwenda kuinua maisha yetu na tuweze kwenda kuanzisha matajiri wazawa ndani ya nchi yetu, ambao ni matajiri kupitia kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)