Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwenye wingi wa rehema, kwa kunipa kibali cha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naunga mkono hoja. Nami niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuamua kwa moyo wake wa dhati kufanya kilimo cha Tanzania kiwe cha kuwaletea wananchi chakula, kilimo cha kuleta ajira vilevile kiwe ni kilimo cha kibiashara, nampongeza sana Rais wangu. Pia nampongeza Makamu wa Rais, Dkt. Mpango, kwa uhamasishaji wa zao la mchikichi. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Bashe Waziri wa Kilomo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Kilimo, hongera sana kwa kazi mnayoifanya. Nitakuwa sijatenda haki nisipompongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu nitajielekeza katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni mchikichi, eneo la pili nitazungumzia mbolea. Kwa nini nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, tangu mwaka 2018 Serikali ilipoamua mchikichi kuwa zao la kimkakati Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa akija Mkoani Kigoma kuhamasisha kilimo cha zao la mchikichi na wananchi walihamasika wanaendelea kuhamasika na kwa sasa ni miaka mitano michikichi ile aliyokuwa akiihamasha na mchikichi alioupanda yeye mwenyewe katika eneo la JKT Bulombora tayari umeishaanza kuzaa matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashe, Naibu wako ameshafika Kigoma, ninakuomba ukimaliza Bunge hili uje ujionee maajabu yanayofanyika Mkoa wa Kigoma katika zao la mchikichi. Gereza la Kwitanga wanafanya vizuri sana, wana mashamba makubwa sana ambayo tangu kilimo cha mchikichi kilipoanza kuhamasishwa wameweza kulima. JKT Bulombora wana mashamba makubwa sana na wanaanza kuzalisha michikichi kuwagawia wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bashe tunakuomba ufike Kigoma.

Mheshimiwa Spika, wananchi wamehamasika, wamelima, bado kuna changamoto kwenye miche ya michikichi, mahitaji bado ni makubwa. Lakini niishukuru Serikali kwa kutenga ruzuku kwa ajili ya miche ya michikichi. Ninakuomba sasa Mheshimiwa Bashe ufike Kigoma.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Benki ya TIB. Wananchi wamekuwa wakihamasishwa kwenda kuomba mkopo TIB, lakini ni ukweli usiofichika kwamba masharti bado ni magumu. Ninaiomba Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, waweze kupimiwa mashamba yao ili waweze kupata hati miliki, mashamba yao yaweze kuwadhamini, hatimaye waweze kukopesheka, bila hivyo bado masharti ni magumu. Kwa hiyo, ninaomba Serikali ihamasishe, Waziri wa Ardhi, wananchi wapimiwe mashamba yao wapate hati miliki ili waweze kukopesheka kupitia hati miliki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuzungumzia kuhusu mbolea. Ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwapatia wananchi mbolea. Tuliipata mbolea ambayo wananchi wameweza kupata kwa shilingi 70,000. Kwa kweli tunashukuru, kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Kigoma ninamshukuru sana Mama kuweza kutupatia mbolea ya ruzuku. Bado kuna changamoto.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashe nikushukuru kwanza, yalipokuwa yakitokea matatizo madogo madogo wakati wa ugawaji wa mbolea kila tulipokupigia simu ulipokea simu na ulitoa maelekezo na watendaji wako waliweza kufanya kama ulivyowaelekeza.

Mheshimiwa Spika, mwanzoni mbolea zilikuwa zinapelekwa Makao Makuu ya Wilaya. Ninakuomba sasa Mheshimiwa Bashe, mbolea ziende kwenye Tarafa na kila Kata ili kila mwananchi atakapohitaji mbolea iwe karibu yake. Kwa sababu wananchi wamepata mateso sana kwa ajili ya ufuatiliaji wa mbolea kutoka vijijini kuja Makao Makuu waliweza kupata shida sana, walilazimika kulala mjini siku mbili, tatu, wakipanga foleni kusubiri mbolea, pia walilipia nyumba za wageni ili waweze kujihifadhi wakati wanasubiri mbolea. Naomba marekebisho yafayike ili waweze kunufaika kwa kupata mbolea bila kupata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vipo vifungashio, mara nyingi mbolea inafungwa kwenye mifuko ya kilo 50 na kilo 25. Wale wakulima wadogowadogo na hasa akina mama wengine ambao hawana uwezo wa kununua mfuko wa kilo 50 au kilo 25, naomba uhamasishe iweze kuwepo mifuko inayofungasha kilo 20, kilo 15, kilo 10, kilo tano hadi kilo mbili ili mbolea iweze kuwafikia hata wananchi wa kipato cha chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimuombe Waziri, yapo malalamiko ya mawakala waliofanya kazi ya kusambaza mbolea zaidi ya miaka mitano na wamekaa kwa matumaini kwamba ipo siku watalipwa pesa zao, Mheshimiwa Waziri nataka nikuulize; je, watu hao watalipwa pesa hizo wanazozidai? Kama hawatalipwa waambieni ukweli waache kusubiri wakati uwezekano wa kulipwa pesa hizo haupo! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo nakushukuru sana, ninaunga mkono hoja. (Makofi)