Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii ya Kilimo ambayo ni muhimu sana, Wizara ambayo ina mchango mkubwa sana katika Taifa letu. Asilimia 26.1 ya pato la Taifa linatokana na Wizara hii. Wizara hii ni muhimu sana kwa sababu inatoa ajira ya wastani wa asilimia 65, lakini siyo hivyo, viwanda vyetu na malighafi zake asilimia 65 zinategemea Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais, anafanya kazi kubwa sana, lakini nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu, anafanya kazi kubwa sana katika Mkoa wetu wa Kigoma na hasa katika zao la chikichi. Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya jambo kubwa sana la chikichi ambapo pamoja na ukuaji mkubwa tunaupigia kelele, lakini jambo la kudhibiti vipimo vya mafuta ya mawese ni jambo kubwa sana katika Mkoa wetu wa Kigoma. Tunatuma salaam hizo za shukrani kwake na kwa Serikali yote na pia kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama, kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya katika Mkoa wetu wa Kigoma. Hivi sasa vipimo vya lita 30 ambavyo vilikuwa vinamnyonya mkulima wa Mawese, vinaonekana kama bangi katika Mkoa wetu wa Kigoma. Hilo tunalishukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri ni kijana, kaka yangu Mheshimiwa Bashe, namshukuru sana kwa kazi anayoifanya. Pamoja na mambo mazuri sana aliyoyafanya katika Wizara yake, natambua Benki ya Kilimo (TADB) imetoa mikopo shilingi bilioni 169, lakini shilingi bilioni 108 zimekwenda kama direct landing. Siyo hivyo tu, bado ametoa shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kwenda kwa wakulima wadogo wadogo. Kwa hilo tunamshukuru sana na tunaendelea kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. hapa liko jambo moja tu ambalo tunamwomba Mheshimiwa Bashe, sisi kama vijana, naye ni kaka yetu atusikie. Hapa kuna changamoto kubwa sana. Kwenye benki hii ya kilimo, hebu uwape mtaji kaka yangu wafanye kazi.
Mheshimiwa Spika, wakulima wanahitaji mitaji. Benki hizi usipoziwezesha, hawawezi kupata manufaa makubwa na benki hii. Mheshimiwa Bashe nitakupa mfano mmoja. Hivi sasa hii Benki ya TADB inaweza kukopesha wakulima wetu kwa asilimia tisa, lakini wakulima bado wana mizigo mikubwa, ndio maana tunaomba uweze kuiongezea pesa ili angalau asilimia ishuke nane mpaka saba ili mkulima asiwe na mzigo mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini si hivyo Mheshimiwa Bashe, wapo watu ambao wanaingia kama ma-middle men kwenye hii benki ya kilimo, ambao ukiangalia kama Mkoa wa Kigoma, ili hizi AMCOS ziweze kukopesheka lazima kuwe na mtu anaitwa PASS. Huyu PASS ndiye atakuwa mdhamini wa mkulima ili mkulima aaminike, watu hawa jaribu kuwa Cut off. Kwa sababu huyu PASS ana percent yake kwenye mkopo ambao mkulima atachukua. Ukiwaondoa hawa PASS unamuondolea mkulima mzigo mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye kahawa Mheshimiwa Bashe, umefanya jambo kubwa sana katika Mkoa wetu wa Kigoma. Umeweza kufanya jambo la msingi sana mpaka wanunuzi wamekwenda kwa mkulima direct. Wamenunua kahawa na angalau kwa Mkoa wetu wa Kigoma bei si haba, tunakushukuru sana kwa jambo hilo. Lakini mzigo umeutoa ulikokuwa mwanzo umeuhamishia kwenye pembejeo. Hivi sasa lita moja ya dawa ya kutibu kahawa iliyokuwa inanunuliwa kwa shilingi 15,000 hivi sasa ni 50,000. Huo ni mzigo mkubwa sana Kaka yangu Bashe, uweze kuangalia namna gani tuweze kumpunguzia adha mkulima huyu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, my brother nitazungumzia jambo lingine, jambo la mkulima na pembejeo. Wabunge wengi wamezungumza katika hali hii ya mbolea ya ruzuku na nimekusumbua sana kipindi cha mbolea hii. Mheshimiwa Bashe, nia ni njema ya suala hili na tunaipongeza sisi Wabunge ambao tunatoka kwenye majimbo ya vijijini. Lakini ziko dosari ambazo zimeingia hapa katikati zilitaka kuchafua nia hii, na jambo hili Mheshimiwa Bashe, tutafurahi zaidi ukilifanyia kazi kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfano tu mdogo ili niweze kumalizia, naona na muda unakwenda. Mheshimiwa Bashe, kwenye hii program ya mbolea ya ruzuku wapo watu wanne, kuna Serikali, kuna supplier, kuna agency ambaye ni wakala lakini kuna mtu wa mwisho ambae ndiye mkulima.
Mheshimiwa Spika, sasa tunapata shida kubwa sana ambapo tunaona mkulima anapiga kelele. Mbolea muda mwingine inamfikia kwa bei ya juu sio hiyo ya ruzuku. Wakulima wa Mkabogo kule jimboni kwangu, wakulima wa vijiji vya kule Kalinzi wameweza kufikiwa na mbolea kwa bei ya 120,000 mpaka shambani, wakati ili hali hii mbolea ni shilingi 70,000. Ukiangalia hapa katikati ni kwa sababu hawa mawakala wana sababu kuu mbili.
Mheshimiwa Spika, sababu ya kwanza; wao wanaweza kutoa ile mbolea kwa mkopo. Maana yake ninyi mnamlipa supplier mnamwacha agent, huyu agent hana mtaji mkubwa wa kuweza kupeleka mbolea mpaka kwenye tarafa na vijiji lakini angekuwa na mtaji mkubwa angeweza kufikisha mbolea hii hadi kwenye vijiji.
Mheshimiwa Spika, sasa, changamoto kubwa unakwenda kumlipa supplier cash unamwacha agent huyu aende akazungushe mbolea kwa pesa yake, matokeo yake mbolea haifikishi. Ukiangale pale Kigoma Mjini agent alikuwepo mmoja. Kigoma mjini hakuna mkulima sisi vijijini ndio tunalima lakini hakukuwa na wakala hata mmoja, kitendo ambacho kimeongeza hii nia njema ikaonekana kuwa nia mbaya lakini tunaamini kwa jambo kubwa ambalo unaendelea kufanya, ukaifanye hii kazi kwa ustaarabu mkubwa sana ili wakulima wetu waweze kunufaika na hali hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nisimalize bila kuunga mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)