Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nishiriki kutoa mchango wangu, ushauri wangu, kwenye sekta hii muhimu kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Taifa letu limepita katika kipindi tofauti na katika kila kipindi tulikuwa tunashuhudia kauli mbiu mbalimbali kuhusiana na hii sekta ya kilimo. Wakati wa Hayati Baba wa Taifa tulianza na kilimo cha kufa na kupona, ikapita tukaja na Kilimo uti wa Mgongo, ikapita, tukaja na Kilimo Kwanza ikapita. Sasa tumemaliza maneno yote ya kiswahi tumekuja na maneno ya kiingereza, bado kilimo kipo pale pale ni changamoto kwa Taifa letu, tunasema (BBT) Build a Better Tomorrow (Jenga Kesho Iliyobora). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mwandishi mmoja wa kiingereza anaitwa Shakespeare aliwahi zungumza kauli hizi mbili; ya kwanza alisema if wishes were horses, baggers would ride them (Kama matamanio yangekuwa Ngami hata omba omba wangeweza kuendesha. Lakini akaaza kuchanganya msemo mwingine tena akisema wishes are weak salad to dine with (matamanio ni sawa na kachumbali iliyochacha haifai kwa kitoweo). (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, tukiendelea kuwa na matamanio kama Taifa kwenye sekta ya kilimo na bila kuwa na jitihada, bila kuwa na utayari, bila kuwa na commitment kwenye sekta ya kilimo, nina wasiwasi hata hii ya BBT (Build a Better Tomorrow). Namwamini sana Kaka yangu Mheshimiwa Bashe na Ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri, katika hili wazo ni jema lakini nitashauri hapa tuboreshe kidogo Ili tusiishie tu kuwa na matamanio, matamanio tukumbuke ni sawa na kachumbari iliyochacha haifai kwa kitowewo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nia ni njema na dhamira ya Serikali ni njema kabisa, naomba nishauri kuboresha eneo hili la ajira hasa kwa hawa vijana hii programu ya BBT.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mheshimiwa Bashe, naomba unisikie kwa makini eneo hili. Mimi ni mkulima na bahati nzuri na kifahamu kilimo hasa cha zao la mpunga, nililipa ada ya elimu ya sekondari kwa kuuza mchele na mpunga. Nitaeleza kidogo hapo am not speaking from without, am speaking from within. Sizunguzmi habari ambayo siifahamu, nazungumza habari ambayo ninaifahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunawachukua vijana na ninaomba nishauri kufikiri kimakakati kwenye eneo la BBT. Kijana yeyote ni desperate anataka pesa ya chap chap, kijana yeyote anataka maganikio ya haraka. Ukichukua kundi la vijana ukawapeleka mahala tukaandaa mashamba ya block farming, zao ambalo litachukua miaka minne, kijana anakimbia, habaki ataondoka. Kwa sababu matamanio yake apate fedha ya chap chap.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwenye eneo hili, twende kwenye maeneo husika ambayo vijana wanajishughulisha na kilimo. Usichukue watu wapya, usichukue watu wa Dar es salaam, usichukue watu wa mjini uwapeleke wakalime, kilimo ni tiresome work sio kazi ya mzaha mzaha ni kazi ya kujituma kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, twende Mororgoro kule Mlimba tukatazame vijana wanajishughulisha na kilimo pale tukawawezeshe wale. Wale wakiwezeshwa, kijana mkulima wa Mlimba anaelima mpunga akalima vizuri, akanunua V8, akajenga nyumba bora anaendesha, vijana wengine watajua kilimo kinalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini hawa watawachukua Dar es Salaam, wamenyoa punk, tunawaweka mahala wakalime kilimo ni tiresome work, sio mchezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe kwanza kufikiri kimkakati jambo moja, aina ya mazao tutakayokwenda kulima yawe ya muda mfupi. Nimeona pale Dodoma ili zabibu ivunwe sio chini ya miaka minne. Nani atakaa miaka minne asubiri hii zabibu? Nina wasi wasi na matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zabibu yenyewe haina soko hapa Dodoma, wananchi mazao yanaoza. Twende tukaimarishe mazao ya muda mfupi. Mahindi, mpunga, kijana ndani ya muda wa miezi minne, au sita ana fedha mfukoni. Mje Mlimba pale mfanye kilimo, muende na maeneo mengine. Mazao ya muda mfupi haya ndio yatakayowasaidia vijana wengi kuvutiwa na kilimo kwa sababu watapata pesa ya chap chap. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine tunazungumzia kilimo cha biashara, ili kilimo biashara kiweze kufanikiwa: -
Mheshimiwa Spika, moja; lazima uwe na ardhi inayofaa kwa kilimo. Sasa na hii ningependa kusikia unapokwenda kuhitimisha, namna gani wizara ya Kilimo inashirikiana na sekta ya ardhi katika kuhakikisha mwananchi wa kitanzania anakopesheka?
Mheshimiwa Spika, leo hii mkulima wa Mlimba ana eneo la heka 50 hakopesheki benki hana title, hawezi kuwa na kilimo biashara. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa
kuwaasa benki zote washushe riba. Ninashukuru benki wameitikia sasa hivi benki mikopo ni single digit asilimia 9. Pia nimekopa juzi CRDB nimekopa wa-vester mikopo mizuri lakini sasa nani anakopesheka? Nimekopesheka kwa sababu nilikuwa nina collateral nina hati. Sasa mkulima wa kawaida asilimia zaidi ya 70 ya wakulima hawana hati miliki. Sasa kilimo biashara itakuwa nikauli ile ile isiyotekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namna gani tunaunganisha sekta ya kilimo na viwanda na Biashara? Hii lazima unapokuja kwenye winding up nipate majibu, unieleze namna gani viwanda na biashara inashirikiana na kilimo katika kuanzisha agro based industries. Hilo nalo ni jambo lingine kwenye suala la zima la masoko. Kwa hiyo, najaribu kueleza haya yote na ni muhimu Mheshimiwa Waziri, ukayaeleza ili tuone kama watanzania kwamba ni kweli tunaona tuko tayari kwenda kuwa na kilimo biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho najua kengele ya pili imegonga, ni ya kwanza naenda ya pili? Ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumzia hoja ya zao la bidhaa ya mchele. Duniani takribani watu bilioni 3.5 wanakula mchele lakini leo hii NRFA hawajajenga hata ghala moja la kuhifadhi mpunga. Mahindi kule Marekani ni chakula cha mifugo. Mahindi yanagharama kubwa kuyahifadhi kuliko mpunga, mpunga hauhitaji dawa yoyote utakaa hata miaka kumi. Adui wa mpunga ni maji tu, mje NFRA na mpango sasa muanzishe maghala ya kuhifadhi mpunga. Hilo ni jambo lingine natoa ushauri kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kwenye suala la umwagiliaji. Unajua nasikitika sana kwenda sehemu kame na kuanza kuchimba visima vya maji tutengeneze mabwawa, gharama ni kubwa. Hii nchi Mungu aliibariki jamani yaani hoja yangu tunataka ku–achieve nini? Yaani tunapokuwa na mpango wa jambo fulani tunataka ku–achieve nini? Ushauri wangu kaka yangu Mheshimiwa Bashe, nakuomba nenda maeneo ambayo uwekezaji wa umwagiliaji ni rahisi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Haya ahsante sana, kengele ya pili imekwishagonga.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)