Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara muhimu, Wizara ambayo imebeba maisha ya watanzania walio wengi. Awali ya yote nipongeze Serikali Kupitia Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo. Ni wazi kwamba kwa kufanya hivyo wanagusa watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitaenda moja kwa moja kwenye mchango wangu. Jambo la kwanza; Jimbo la Kasulu Vijijini lina kata 21, kata 10 kati ya 21 wanalima pamba. Ukienda kwenye Kata ya Asante Nyerere, Kata ya Rungwe Mpya, Kigembe, Pwaga, Shunguliba, Nyamidaho, Kitagata, Kurugongo na Lusesa, kata kumi, kata zote hizi ni wakulima wa pamba.
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali tangu mwaka 2019 mpaka leo 2023 imeweka baridi kwenye sekta ndogo ya pamba. Baridi kivipi? Kuna madai ya key players kwa maana ya makampuni ya ununuzi wa pamba lakini na makampuni ambayo yana–supply pembejeo wanadai Serikali zaidi ya bilioni 102 kwa zaidi ya miaka minne sasa Serikali inadaiwa, imeshikilia pesa hiyo haijawalipa fedha zao. Kwa kufanya hivyo, kumefanya sekta ndogo ya pamba iweze kuathirika na kusinyaa. Wananchi kule ndio ambao wanateseka kwa sababu hawa ndio key players. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumefanya vikao mara kadhaa na hata hapa Bunge lako liliazimia kwamba Serikali inapaswa kulipa fedha hizo. Tunataka tujue wakati waziri akija hapa kwenye majumuisho atueleze ni lini Serikali italipa fedha hizi za key players hawa kwenye sekta ndogo ya pamba ili kuchangamsha sekta hiyo otherwise hatutakubaliana. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nichangie kuhusu Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Mheshimiwa Waziri, unisikilize kwa umakini, CPB ilikuwa ni taasisi ambayo inaenda kufa kabisa it was a loss-making company. Sasa hivi imeanza kutengeneza faida na inakwenda vizuri, lakini ziko taratibu ambazo bado zinaishika. Tumewasikiliza kwenye Kamati yetu ya PIC mara kadhaa. Hawa CPB wanafanya biashara kama wafanyabiashara wengine, wana–competitor wengi tu kwenye kuuza unga, kwenye kuuza sijui nini, kwenye kuuza mafuta, kwenye yote wanayoyafanya wana competitors wengi.
Mheshimiwa Spika, sasa kuna changomoto ya kwanza ni kuhusu mtaji. hawa watu kwa sababu wanafanya biashara na wanapata faida wala hawahitaji Serikali ichukue mtaji iwape ila iwawekee utaratibu mzuri wakitaka kukopa fedha.
Mheshimiwa Spika, CPB wakitaka kukopa fedha kwa ajili ya biashara wanatakiwa kwenda kuomba kibali. Yaani bodi ya CPB haina mamlaka wala nguvu ya kuweza kwenda kukopa, yaani kwenda kukopa benki mpaka waombe kibali kutoka Wizara ya Fedha, mchakato ambao huwa unakwenda mpaka miezi mitano au sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sasa wakati kuna competitor wengine wakitaka mtaji wao wanakwenda benki wanakopa wana-invest kwenye biashaara sisi taasisi yetu hii lazima kwanza tusubiri miezi sita. Yaani bodi ilishapanga kukopa, imepitisha inaenda kwanza Wizara ya Fedha, unasubiri sijui miezi mitano au sita ndipo majibu yaje wakope.
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuisaidia taasisi hii. Kama tutataka kumsaidia Mheshimiwa Waziri taratibu hizi zirekebishwe, hawa watu wawe na uwezo wa kwenda kukopa. Bodi ikshaidhinisha wawe na uwezo wa kukopa, wakikopa tutakuwa tunafungua minyororo ambayo tumewafunga na tutakuwa na spidi nzuri sana kwenye ku- compete na wengine ambao wako kwenye soko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa ubunifu wake wa wakugusa sasa wakulima wadogowadogo kupitia bajeti yake ya mwaka huu. Nimesoma kwenye ukurasa wa 138 wa bajeti yake; kwamba anakwenda kujenga miundombinu kweye kila halmashauri. Kila halmashauri itachimbiwa kisima kirefu, kwa kuanzia, kwa hiyo watachimba visima 184. Pia amesema atawawezesha wakulima, yaani kila kisima kimoja kitatumiwa na wakulima 150, kila mkulima atapewa eka mbili. Kwa hiyo zaidi ya ekari 69,000 zitaendelezwa, hii ni hatua kubwa sana. Hata wale ambao walikuwa wanalalamika kwamba BBT haijachukua vijana wao, sasa unakuja mradi ambao kila halmashauri, kwa kuanzia, ina uwezo wa kuwa na watu au wakulima 150 ambao watawekewa utaratibu mzuri na hatimaye waweze kujiajiri, huu ni mwanzo mzuri. Ninaamini kila mwaka utakuwa unazidi kuongeza fedha ili badala ya kuchukua wakulima 150 uende mpaka 500 na zaidi katika kila halmashauri ili kuhakikisha kwamba wakulima tunawasaidia; hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu Benki ya Kilimo, Benki ya Kilimo tulishasema hapa pia, lilishaweka Azimio la Bunge; kwamba wapewe bilioni 100 ili kuwea ku-bust mtaji wao waweze kuwafikia watu wengi. Kila mtu anasema Benki ya Kilimo inafanya vizuri, wengine wanasema hatujakopeshwa; ni kwa sababu wanania ya kukopesha lakini mtaji ni mdogo.
Mheshimiwa Spika, mimi najifikiria, kwa nini Benki ya Kilimo, yaani iwe chini ya Wizara ya Fedha, why? Hili Serikali mkalifikirie vizuri. Yaani kwa nini isiwe Wizara ya Kilimo huko huko? Yaani Benki ya Kilimo iko Wizara ya Fedha, sidhani kama kuna ulazima sana Benki ya Kilimo iende kuripoti kwa Waziri wa kilimo.
Mheshimiwa Spika, hii inaweza kusaidia sana kuepusha baadhi ya delaying communication na maamuzi, wala hakuna shida yoyote. Tunashudia kuna baadhi ya Wizara hapa zinamiliki vyuo; kwa nini wasiseme kwamba chuo cha kilimo ki-repot kwenye Wizara ya Elimu? Mbona kina-report kwa Wizara ya Kimo wenyewe? Chuo cha Biashara kina- report kwenye viwanda na biashara; kwa nini kisi-report kwa Wizara ya Elimu? Kwa hiyo hii nayo inawezekana. Wizara ya Kilimo wapeni benki yao ili kupunguza hizo delaying za communication kati ya Wizara na Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.