Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniaptia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Kilimo. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuongeza bajeti kwa 29 percent kwenye bajeti yetu ya kilimo, ambayo itatusaidia sana hasa sisi ambao tunatoka katika maeneo ya kilimo. Mwaka huu tunakabiriwa na ukame mbaya sana ukilinganisha labda wa mwaka 1974, kwa hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunahitimisha Wizara ikiwemo na kamati moja, mimi leo nitaanzia Wizara ya Mifugo na uvuvi ambayo ilianza mwanzo.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mwanasheria Mkuu wa Serikali yupo hapa; tunaomba, kwa wafugaji wetu ambao ng’ombe wao wamekamatwa kwenye hifadh,i wanapokuwa wametolewa hukumu wapelekwe kwenye mnada kwenda kuuzwa kihalali badala ya mtindo wa sasa hivi ambapo watu wa kule hifadhi wanapiga mnada wao. Wapelekwe mnadani kama sheria ya Serikali ilivyo na mnada wa Serikali ndio unaotambulika, itawasaidia sana. Wafugaji wetu watapata kinachobaki na wao Serikali watapata kinachobaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la kufunga Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria. Sisi maeneo yetu uchumi wetu pia unategemea maziwa haya. Maziwa haya yakifungwa tutakuwa tumeingia kwenye mgogoro mkubwa sana hata sisi watu wa Kahama na Shinyanga, hasa wakati huu ambao ni mgumu sana kwetu.
Mheshimiwa Spika, niwapongeze Wabunge wa Kigoma kwa mchango mzuri sana ambao walionesha wakati wa kutetea. Lakini kikubwa, na hoja yangu ya msingi hapa ni kwamba lazima wataalamu wetu watumie muda mrefu sana wa kufikiri. Ng’ombe anazaa mtoto mmoja kwa mwaka, mbuzi anazaa mtoto mmoja kwa mwaka, na kondoo pia, lakini hatujawahi kuona shortage inatokea. Ni lini tumepata shida kwamba nyama ya ng’ombe hakuna au ng’ombe hakuna; na hata sasa hivi tunazozana kupunguza ng’ombe?
Mheshimiwa Spika, samaki anazaa watoto laki mbili mpaka milioni moja; tunahakika wamekwisha? Ni uongo wa mchana. Kinachoendelea hapo ni kwamba gharama ya uvuvi imepanda. Leo drum moja la petrol ambalo ni lita 200 unahitaji zaidi ya shilingi 800,000 mpaka 1,000,000. Sasa kama una ma-drum matano unaondoka kwenda kuvua huna darubini, hujui samaki walipo, umeondoka na gharama ya shilingi milioni tano, unategemea utapata samaki wa milioni nane? Haiwezekani, ni report za uongo.
Mheshimiwa Spika, je, hawa wangekuwepo siku Yesu alipowakuta akina Simon na Petro wamekosa samaki wangelifunga Ziwa la Galilaya? Uvuvi ni kubahatisha; haiwezekani kazi ya kubahatisha, hakuna uvuvi duniani asili yake ni kubahatisha. Hata siku ya Bwana Yesu alikuta akina Simon na Petro wamekosa Samaki ndipo akawaombea wakapata. Sasa angekuwepo mtaalamu wetu angelifunga Ziwa la Galialaya? Haiwezekani, hatuwezi kuwa na wataalamu ambao ni wavivu wa kufikiri, watatuingiza kwenye migogoro mikubwa mno. Mnaona tunazozana hapa suala la herein, tunazozana kweli wananchi mpaka wanauliza, kwa nini ninyi huwa hamleti mijadala ya kutupa nyasi za kulisha ng’ombe? Ninyi mijadala yenu yote ni kuja kwetu kuja kutukamata. Hakuna mawazo mapya yanayotoka kwenu? Wananchi wanahitaji mawazo mapya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakwenda kwenye suala la kilimo. Ni kweli kwenye jimbo langu nina viwanda zaidi ya sita vya pamba na vinategemea pamba, lakini kwa bei inayoonesha, ya mwaka huu, labda tu tumuombe ndugu yangu Mheshimiwa Bashe mbegu za pamba na viuatilifu vya pamba viuzwe madukani kama zilivyo mbegu za mahindi na mazao mengine, itatusaidia. Kwa sababu sasa hivi mwananchi atakatwa shilingi 490 mpaka 500 kwa kilo moja, Mheshimiwa Bashe ni huruma na huruma, lazima ufanye huruma ngumu sana. Mwananchi anapata kilo 200 kwenye ekari moja shilingi laki mbili; akikatwa huyu mtu, na hali ya chakula ilivyo, ni lazima kufikiria sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, ruhusu watu wanaoweza kununua mbegu zao wanunue ili wao wakati wanauza pamba yao wawe huru kama mazao mengine. Kwa nini mimi mnanilazimisha nikaungane kwenye group lingine? na kwa nini mimi nimlipie mtu ambaye mimi sihusiani naye? Mimi nimelima pamba kidogo, sikutumia dawa, sikutumia mbolea, nimelima na wanangu, naendaje kumlipia mtu mwingine aliyetumia mbolea na dawa? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, trend hii ikienda zao la pamba tunakwenda kulinawa, a hundred percent tunakwenda kulinawa; kwa sababu mazao ni mengi mno Kanda ya Ziwa. Alizeti leo heka moja mtu atapata shilingi laki saba au nane kwa nini akalime pamba yenye matatizo mengi na migogoro mingi? Halafu ndiyo iwe na sheria kali. Kwa hiyo namuomba sana Mheshimiwa bashe aliangalie kwa mapana sana suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la mbolea hii ya kupima. Mheshimiwa Waziri yeye ana bucha; sasa nashangaa; wewe Mheshimiwa Bashe kwenye bucha lako unapima nyama watu wanaenda kula; sasa unamkataza mtu kupima mbolea ikaende ardhini, inawezekana kweli? Yaani haieleweki ni kwa nini. Na ukiisoma hiyo sheria ya kupima mbolea ni miaka miwili jela? Sasa, mwananchi hana hela laki moja na nusu, anataka kulima mchicha, sasa anafanyaje? Au unataka kuweka kwenye garden? Kwa nini mbolea iwe na thamani kuliko chakula? Wote tunaona, sukari tunapima.
Mheshimiwa Spika, karibu na kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu pale kuna nyama za kuku ziko nje, tena zimechomwa na Waheshimiwa Wabunge wote mko pale. Sasa iruhusiwe kula nyama iliyochomwa iko nje lakini mtu anayechukua mbolea kusaidia mwenzie anakamatwa matokeo yake wananchi wanauziana kwa magendo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri aruhusu, hizi sheria mengine za kikoloni kwa sasa hivi hatuzihitaji tena. Kama mama ametoa fedha zote hizi tunaendeleaje na sheria mbaya za kikoloni?
Mheshimiwa Spika, Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Viwanda na Biashara anafahamu vizuri. Kuna sukari ambayo inatengenezwa kutoka kwenye viazi vya kienyeji; na hoja hiyo imeletwa mara nyingi sana kwenye Kamati wakati mimi bado niko kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara; na sukari hiyo ni sukari ambayo inatumika kwenye soda na vitu vingine, hata kwa chakula, na ni nzuri mno, lakini inapigwa vita na watu wa viwanda vya sukari. Kwa sababu wananchi wakianza kulima viazi hivi vya kawaida wakatengeneza sukari teknolojia hii itawaondoa wao kwenye miwa.
Mheshimiwa Spika, leo mmesikia mabadiliko makubwa yaliyotokea China, China nusu wanatengeneza gari za umeme. Si na sisi tutatupa gari zetu huku? Kwa nini wao wazuie wananchi wasilime viazi ambavyo vinaiva miezi miwili, havihitaji dawa na havihitaji kitu chochote ili wakatengeneza sukari, lakini baada ya makapi yale yakawa ni chakula? Sasa kwa nini watu wakatae kibabe, kwamba wamekataa?
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Khenzile ni shahidi, anafahamu, wafanyabiashara wamekuja mle wanalia, kwamba jamani ruhusuni viazi hivi vya kawaida.
Mheshimiwa Spika, maana sisi hata kwa kienyeji viazi ukivikausha ukaja ukavichemsha inayotoka ni sukari, wala haina hata ubishi. Kwa hiyo ni kiasi cha Wizara ku-promote ili kuondokana na hili la kulalamikia mazao ya kila aina.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia nimshukuru sana Mheshimiwa Bashe, umetusaidia sana hasa wakati wa njaa. Ametusaidia mahindi ya kutosha na kila wakati tulikuwa tukihitaji msaada wowote amekuwa akitusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huo nakushukuru sana. (Makofi)