Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ili nami nichangie bajeti iliyo mbele yetu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwenye Wizara hii kwa mambo makubwa matatu. Jambo la kwanza ni kutupatia pembejeo za korosho bure kwa msimu uliopita, jambo la pili kwa kutupatia mbolea za ruzuku kwenye msimu huu uliopoita, na jambo la tatu tulipatiwa mahindi ya msaada pale wanyama pori walipotupeleka kwenye njaa kwa hiyo ninamshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kushukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia viuatilifu vya bure. Lakini wako wajanja wenzetu ambao wanatumia hizi lugha za kisasa “kutumia fursa.” Kwa kweli Mheshimiwa Waziri hangaika na hawa watu wanaotumia fursa kwa kutupatia viuatilifu vilivyokosa ubora. Jambo hili limetushushia uzalishaji wa korosho kwenye mkoa wetu wa Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo kubwa lilionisimamisha leo hapa, kuna dude moja hivi sijapata kulielewa linaitwa COASCO. Niko kwenye Bunge hili mwaka wa nane, hii taasisi inayoitwa COASCO sijajua inafanya kazi gani. Na Mheshimiwa Waziri hata ukileta semina leo watu wa COASCO hapa wakaja kutoa maelezo mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuelewa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano nina AMCOS zangu tano Liwale mwaka juzi walifanya vibaya, likaitwa hilo dude la COASCO likaja. Wamefanya kazi pale takriban kwa wiki tatu hivi kama siyo mwezi. Lakini findings walizozikuta pale mpaka leo ni makabati ya kwao wao, hatujui kinachoendelea. Viongozi wa AMCOS wanafahamu, lakini wanachama wa AMCOS zile hawajui chochote mpaka leo. Sasa sijaelewa hiyo COASCO imewekwa pale kwa ajili ya kulinda au kuchunguza? Yaani sijaelewa. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri hebu hiyo semina ije pengine na mimi nitaweza kuelewa; lakini nilisha sema nitakuwa wa mwisho.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo; ziko findings ambazo ukiwauliza watakuambia hizi tumempelekea Mkuu wa Wilaya, hizi zingine tumewapelekea TAKUKURU; lakini mbona huu ni mwaka wa tatu sasa AMCOS zile bado watu wanalalamika? Kuna AMCOS mimi kule kwangu mizani na matrekta vimeuzwa. COASCO wamekwenda kufanya uchunguzi lakini findings zile hawajaweka wazi mpaka leo. Hawa watu COASCO kama kuna sheria ya kuunda hiyo COASCO; kwanza mimi sielewi wamewekwa pale kwa kazi gani, sheria inasemaje, wamewekwa pale COASCO kwa sababu ipi?

Mheshimiwa Spika, Kama AMCOS tano wamezikagua leo mwaka wa tatu bado zinahangaika! Ukienda TAKUKURU huelewi chochote ukienda kwa Mkuu wa Wilaya anakuambia findings ziko TAKUKURU.

Mheshimiwa Spika, lakini hilohilo jambo la COASCO nalipeleka moja kwa moja mpaka kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika. Kwa sababu moja ya swali ambalo nilimuuliza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa wa Lindi, nilimuuliza wewe kama mlezi wa AMCOS kuna AMCOS zina matatizo moja mbili tatu umezifanyia nini? Ananiambia suala lao liko COASCO. Nikamwambia mrajisi kuna matrekta yameuzwa, wanachama wanalalamika matrekta yameuzwaje? Anasema matrekta haya yameuzwa lakini fedha zilingia kwenye account ya AMCOS; lakini fedha zile zimetoka kwenye account ya AMCOS zimefanya nini yeye haimuhusu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ina maana kwamba Mrajisi wa Vyama vya Ushirika uwezo wake ni kujua tu kwamba matrekta yameuzwa fedha zimeingia kwenye AMCOS, AMCOS wamefanya nini yeye hajui. Nako kuna shida, nako huko kwenye vyama vya ushirika nako kuna shida. Mimi kwa ufahamu wangu Mrajisi wa Vyama vya Ushirika yeye ndiye msimamizi wa vyama vya ushirika, kama kuna chama cha ushirika kina mgongano labda kati ya viongozi na wanchama yeye anaingia kati.

Mheshimiwa Spika, unajua nini kilichofanyika; wakati hawa COASCO wameleta ripoti walikuja na Mrajisi wa Mkoa akaitisha mkutano wa wanachama, alikwenda pale akasoma tu zile findings za COASCO akasoma akaondoka akasema mkutano huo sitaki maswali. Hao ndio viongozi wetu.

Mheshimiwa Spika, na mimi nikashangaa sana mimi nikajua hiyo COASCO sikujua kwamba iko chini yake Mheshimiwa Waziri. Kwa sababu yeye kwa sifa aliyo nayo kwa utendaji na weledi wake kuwa na hili dude liko pale limuharibia… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Kuchauka, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo kwa sababu kiu yangu ilikuwa ni COASCO, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)