Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote naendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kujaalia yaliyotokea mwaka 2015 na hatimaye kupitia wananchi wa Jimbo la Sengerema wakaendelea kuniamini na sasa naungana na timu ya kikosi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea maeneo matatu; la kwanza, nina masuala yangu ya Jimbo ambayo naamini Serikali kupitia Mawaziri husika wanaendela kuyafanyia kazi. Pia nitatoa ushauri kidogo na mwisho nitauzungumzia utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Waheshimiwa Wabunge wengi hapa kuunga mkono hotuba na mapendekezo ya bajeti yaliyoletwa hapa mbele yetu kupitia Mawaziri wawili hapa Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki na wasaidizi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hizi za Waheshimiwa Mawaziri hawa zimebeba mambo mengi sana; na kwa kadiri michango inavyoendelea inaonekana tu wazi ni dhahiri kwamba mambo mengi yamefanyika na kwenye mipango kuna mambo mengi yamepangwa kufanyika.
Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki, nafahamu ninyi mnawakilisha, lakini kuna mambo mnayoyasimamia ninyi yanaingiliana, ni maeneo mtambuka na maeneo mengine na sekta nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ambalo nataka niikumbushe Serikali, pale Sengerema nina ombi langu la muda mrefu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema. Hospitali yetu teule iliyoko pale imezidiwa. Ruzuku inayotolewa pale haitoshi. Nimekuwa nikiomba na leo nakumbusha tena, ni mwaka wa tatu nakumbusha. Ile ruzuku ambayo iliyotumika kipindi kile wakati hospitali ilikuwa na vitanda 150, sasa ina zaidi ya vitanda 375. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ombi hili liendelee kufanyiwa kazi na ninaamini, nimeshazungumza na Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, naamini wako hapa wanaendelea kulifanyia kazi, lakini nasisitiza kwamba wananchi wa Sengerema wanahitaji kuona matokeo ya ombi letu yakifanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nikumbushe, tuna ombi letu pale Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini sasa limerudi kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu viongozi hawa wako mbele yetu, Mawaziri hawa walioko katika Ofisi ya Rais, naamini kwamba, wanalifahamu. Tuna ombi la kupandisha hadhi Mji wa Sengerema kutoka Mamlaka ya Mji hadi Halmashauri ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusisitiza ni kwamba ombi lile pia limebaki kuwa la muda mrefu. Limechukua miaka kadhaa lakini ahadi za Serikali zimekuwa zinafanyiwa kazi. Naomba nisisitize kwa mara nyingine kwamba wananchi wa Wilaya ya Sengerema wana hamu kubwa kuona Mji wa Sengerema unapandishwa hadhi kutoka Mamlaka ya Mji kuwa Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia hizi bajeti lakini tukitambua katikati yake zipo Halmashauri ambazo hivi karibuni zimegawanywa, kumezalishwa Halmashauri nyingine ndani ya iliyokuwa Halmashauri moja. Ombi langu la ujumla, siyo kwa Wilaya ya Sengerema tu ambapo tumepata pia Halmashauri ya Buchosa, naomba Serikali itafakari, ione namna ya kuziongezea bajeti, kwa sababu bajeti tuliyopitisha mwishoni, Halmashauri zote ambazo ndani yake kumetokea Halmashauri nyingine ikiwemo Halmashauri ya Sengerema na Halmashauri ya Buchosa, nimesikia pia Halmashauri ya Chalinze na nyingine. Hili ni ombi la ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kuhusu suala la madawati. Kwa hali ilivyo na kwa mahitaji ya madawati yanayohitajika katika nchi yetu ya Tanzania, Halmashauri zote kwa vigezo vya mapato vilivyopo sasa, siyo rahisi sana kuliweza hilo jambo. Tunaomba Serikali izidi kutafakari kwa siku zilizobaki hizi mpaka mwezi wa sita. Kama katika bajeti hii tunapokwenda kupitisha tunaweza kufanya adjustment katika baadhi ya maeneo, tuziwezeshe Halmashauri zetu kupata fedha za kutengeneza madawati ili tuongeze kasi ya kutengeneza madawati kwa kuhudumia wanafunzi ambao sisi tunawalea kama Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano wa Jimbo la Sengerema. Jimbo la Sengerema tunahitaji madawati 23,000 leo. Maana yake unazungumzia zaidi ya shilingi bilioni moja; kwa hakika hatuwezi kuzipata kwa miezi michache iliyobaki pamoja na juhudi ambazo zinaendelea. Sisemi kwamba wananchi wakae au Halmashauri na viongozi wa Mkoa wakae tu, lakini ninachosisitiza ni kuona ni namna gani ambapo sisi kama Bunge tunaweza kushirikiana kurekebisha bajeti iliyoko hapa ili tuokoe pia tatizo ambalo ni la Taifa na siyo tatizo la eneo moja moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, nashauri kwamba tunapokwenda kuhitimisha mgawanyo wa mafungu huko mbele ya safari, tutafakari suala la kuwezesha upatikanaji wa madawati kwa kurekebisha bajeti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mimi niko kwenye Kamati ya Sheria Ndogo. Tumemsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu jana ameliarifu Taifa habari njema sana, kwamba sasa wameongeza threshold ya Mamlaka ya Halmashauri kupitia vitengo vyao vya sheria kwa maana ya ile mikataba kwamba sasa Halmashauri zote zishughulikie mikataba yote isipokuwa inayozidi kuanzia shilingi bilioni moja na kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo hili tulipe uzito, tukiwezeshe kitengo cha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na hasa Wanasheria walioko katika Halmashauri zetu. Tunaofanya nao kazi, tunaona udhaifu ulioko pale, lakini wakati mwingine ni kwa sababu ya matatizo ya kibajeti. Kwa hiyo, ninachoshauri hapa ni kwamba bajeti yao tuiongeze kwa Kitengo cha Sheria kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ili wanasheria walio kule kwenye Halmashauri zetu waweze kufanya kazi zao vizuri zaidi. Siyo zaidi ya hapo tu, pia kuongeza ikama ya Watumishi katika Halmashauri zetu. Tukifanya hivyo tutafanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa sana kuhusu utawala bora, lakini naungana na Watanzania walio wengi kuunga mkono hatua zote zinazochukuliwa na Mheshimiwa Magufuli kwa sasa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliweka sawa Taifa letu. Historia inaonyesha, nchi zote duniani ambazo zimefanikiwa kupata maendeleo ya kasi, zimepitia vipindi vigumu lakini pia baadhi ya hatua zilizochukuliwa na viongozi wao wa kitaifa ni pamoja na hizi ambazo amechukua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, nitatolea mfano wa nchi ya Singapore. Wote tunafahamu wanaofuatilia historia. Yule Waziri Mkuu wao wa kwanza aliyeiongoza ile nchi kwa miaka 31, yule Lee Kuan Yew aliongoza toka mwaka 1959 mpaka mwaka 1990. Mojawapo ya changamoto alizokutana nazo kipindi kile ni wakati ambapo walivunja muungano wao na nchi ya Malaysia wa mwaka 1965, ni muungano uliodumu kwa miaka miwili tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuvunjika, Waziri Mkuu Yew alipata shida sana kutafakari nini kitafuatia, kwa sababu ni nchi ndogo ambayo ukubwa wake ni sawa sawa na nusu tu ya Jiji la London. Alijiuliza kwa sababu walikuwa hawajajiandaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua zinazochukuliwa leo na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni kwa ajili ya manufaa ya Taifa hili. Nazungumza haya bila kubeza na kwa namna yoyote ile bila kudharau kazi iliyofanywa na watangulizi wake.
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba ni kengele ya kwanza hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya bila kubeza kazi iliyofanywa na watangulizi wa Mheshimiwa Rais wa Awamu Tano, lakini kwa hakika Taifa tulipokuwa tumefikia na sisi wote ni mashuhuda, Taifa hili linahitaji kuumbwa upya. Tunalifinyanga upya ili tusonge mbele kwa pamoja. Kama alivyofanya Waziri Mkuu wa Singapore, Taifa hili linahitaji juhudi hizo. Waziri Mkuu wa Singapore yule baada ya ule muungano wa Malaysia kuvunjika, alijifungia wiki sita, akaenda Kisiwani kule akakata simu hakuwa na mawasiliano na Baraza lake la Mawaziri, hakuwa na mawasiliano na Wabunge wenzake, akasema yeye anajifungia kutafakari mustakabali wa Taifa lile.
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya kuapishwa, aliendesha hii nchi pamoja na Waziri Mkuu kama jeshi la mtu mmoja, akitafakari mustakabali wa Taifa hili. Hatua zinazochukuliwa leo zisitufanye sisi kama Taifa kutoka njia kuu. Tunafahamu hapa wapo watu wanalalamika kwamba hatua anazozichukua zinazidi kiwango, lakini fikiria yanayotokea! Soma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, yanayosemwa haya, ni nini kifanyike kudhibiti? Kwahiyo, naungana na wenzangu na ninawashawishi wenzangu kwamba tuungane pamoja kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia habari za wenzetu kusema Ibara ya 18 ya Katiba imevunjwa. Tuache kuwapotosha wananchi. Kinachosemwa kwenye Ibara ya 18 hapa, ni wananchi kupata kuwa na haki ya kupata taarifa, utaratibu umeandaliwa na Bunge hili. Kilichobadilika ni ratiba tu. Kwa nini tunang’ang’nia live? Kuna haki gani inayosemwa “live” katika Katiba yetu? Hakuna haki live inayooneshwa katika Katiba yetu. Kwa nini hawa wenzetu wanapiga kelele? Mambo mengine yanakatisha tamaa sana. (Makofi/Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma ukurasa wa 17 wa taarifa ya wenzetu, wanasema Serikali isafishe mtandao wa ufisadi uliojengwa na Wakurugenzi wa Halmashauri na wahasibu wao wa kutoa tender kwa upendeleo. Unalikuta jambo hili limeandikwa katika taarifa ambayo inawasilishwa hapa na inajenga historia ya maamuzi na mapendekezo yanayotolewa na Kambi ya Upinzani. Ni jambo la aibu! Kwa sababu jambo hili la tender kutolewa, sisi Waheshimiwa Wabunge hapa ni sehemu ya Madiwani kule, ni jambo la kusimamia sisi; siyo jambo la kuja kulalamika hapa. Unamlalamikia nani? Kama ni udhaifu wa Halmashauri yenu, ni wa kwenu. Miongozo na taratibu zipo wazi hapa! (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema tu kwamba tusiwapotoshe Watanzania kwa sababu ya hasira tulizonazo. Wote tunafahamu tulivyokumbushwa, huu mchezo hauhitaji hasira, ni lazima uwe tayari. Ukiwa na hasira utapata taabu kidogo, kwa sababu ya mambo yanavyokwenda. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimalizie kwa kusema naunga mkono hoja asilimia mia moja.