Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kutokana na suala la muda nalazimika pia kuchangia kwa maandishi na mchango wangu utajikita kwenye zao la korosho pekee kutokana na anguko lililotokea msimu uliopita.
Mheshimiwa Spika, ili kuhami zao la korosho linaloyumba kila mwaka nashauri yafuatayo; kwanza Serikali ikubali kupunguza makato kwa mnunuzi na mkulima (kwa rejea ya msimu uliopita ni wastani wa shilingi 1,130 kwa kilo) ili kuhami bei ya soko.
Pili, Serikali ifute ushuru wa shilingi 110 inayoitwa ya maendeleo ya korosho huku ukweli ukiwa ni fedha za kulipia pembejeo kwani tayari Serikali ile ile iliwatangazia Watanzania kupitia Bunge na sheria ikapitishwa ya kurejesha fedha za export levy asilimia 50 kwa wakulima.
Tatu, Serikali ifute ushuru wa shilingi 81 ya magunia na ieleze ziliko fedha za magunia za misimu ya mwaka 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022 ambazo wasambazaji wa magunia ya mwaka 2017 hawajalipwa hadi leo na deni linazidi kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, nne, Serikali ifute ongezeko la ushuru wa shilingi 20 kwa watunza maghala na kufanya kuwa shilingi 52 hadi itueleze wakulima sababu za msingi za ongezeko hili kubwa la ushuru.
Mheshimiwa Spika, tano, Serikali ipeleke haraka muswada wa sheria kupunguza makato ya export levy kutoka asilimia 15 ya FOB hadi asilimia tisa (single digit) kuhami bei ya soko na Bodi ya Korosho iharakishe mchakato wa kuandaa mapendekezo kwenye kikao kijacho cha wadau kutazama kama bado haya makato yana tija kwa wakulima na ikibainika hayana tija, yafutwe.
Mheshimiwa Spika, sita, Serikali ianzishe mfumo maalum wa ruzuku ya kufidia soko la korosho (subsidies) ili ikitokea soko limeyumba, Serikali iwe na uhakika wa kumuokoa mkulima. Tunaweza kutenga sehemu ya mapato ya export levy kwa ajili hii.
Mheshimiwa Spika, saba ni muda muafaka wa kuanza kutazama upya muundo wa vikao vya wadau wa zao la korosho ambao ndio hupitisha makato kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kupata wawakilishi kwenye kikao cha wadau upoje na wawakilishi wa wakulima ni asilimia ngapi ya wajumbe wote?
Mheshimiwa Spika, kuhusu pembejeo na kushuka kwa uzalishaji wa korosho; zao la korosho linashuka uzalishaji mwaka hadi mwaka toka tani laki tatu mwaka 2017/2018 hadi tani laki mbili mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kushuka huku kwa uzalishaji ambako pia kwa mwaka huu makusanyo halisi ni tani laki 1.7; moja ya sababu ya kushuka huku kunatokana pamoja na mambo mengine kama utaratibu usiofaa wa pembejeo, pembejeo zisizozingatia hali ya hewa ya eneo, usambazaji wa pembejeo fake.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwanza utaratibu wa awali wa mkulima kuchangia pembejeo anayoitaka, kwa kiasi anachokitaka urejeshwe huku Serikali ikifidia bei ya ziada kupitia export levy. Hii itasaidia sana mkulima kupata pembejeo aitakayo kutokana na hali ya hewa.
Mheshimiwa Spika, pili, Kamati ya Pamoja ya Ununuzi wa Pembejeo chini ya MAMCU ivunjwe, tuendelee na utaratibu wa zamani kwani kamati hii imetumia fursa hii kujineemesha huku ikiingia mikataba na wazabuni wasio na uwezo, wenye pembejeo fake na pembejeo ambazo hazijawahi kutumika kwenye korosho na zinazoshusha uzalishaji. Kasi ya pembejeo mpya kujaa sokoni ni kiashiria kimojawapo.
Tatu, export levy isitumike kuchangia pembejeo na tuifute shilingi 110 ya maendeeo ya korosho kama tulivyoshauri hapo juu.
Mheshimiwa Spika, nne, Serikali itoke hadharani iseme hatua alizochukuliwa msambazaji wa pembejeo fake zilizokamatwa Masasi, Nachingwea, Tandahimba na Newala ambaye alijinasibu kushirikiana na vigogo wa Serikali huku akikimbizwa China kupisha joto la mijadala na aliporejea hakuna hatua alizochukuliwa.
Mheshimiwa Spika, tano, Serikali ieleze ziliko pembejeo fake ambazo kila mwaka zimekuwa zikikamatwa kila msimu wa korosho unapofika.
Mheshimiwa Spika, mwisho ila sio kwa umuhimu, ni vyema Serikali itoe athari za makisio ya pembejeo vs uzalishaji iliyotolewa na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho ya tani laki nne na tukaagiza pembejeo kulingana na makisio hayo. Hii bakaa ya tani laki 230 ambayo Serikali inalipa bila mshirika (mnunuzi) tunatoa wapi.
Mheshimiwa Spika, kwa msimu wa mwaka huu wa 2022/2023 indirect charges kwenye kila kilo moja ya korosho ambazo zimeathiri bei ya soko zipo kama ifuatavyo; hizi analipa mnunuzi (mkulima in fact); makato ya maendeleo ya zao la korosho (pembejeo) shilingi 110; ushuru wa watunza maghala shilingi 52; deni la magunia shilingi 81; usafirishaji shilingi 120; export levy ambayo ni sawa na asilimia 15 ya FOB shilingi 380; ICD shilingi 120; Ushuru wa Bandari shilingi 100; vibali shilingi 10; offload shilingi 10; provisional income tax shilingi 70; forwarding charges shilingi 10; na other charges shilingi 50.
Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile gharama hizi mwisho wake zinarudi kwa wakulima, hivyo nashauri tufanye marejeo ili kuwaongezea morale wakulima na wanunuzi pamoja na kupata mbegu bora. Ahsante kwa nafasi.