Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa hotuba nzuri ya bajeti iliyobeba maudhui ya mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha bajeti ya kilimo kupanda kwa asilimia 29 na kuruhusu mradi mzuri, mkubwa wa kuwawezesha vijana na wanawake kunufaika na kilimo wa BBT.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mpango wa BBT awamu hii ya kwanza, vijana zaidi ya 800 wako vyuoni wanapatiwa mafunzo. Faida za mpango huu wa BBT ambapo wanawake na vijana wanufaika wa mpango huu watapata ni kama ifuatavyo; ardhi iliyopimwa, hivyo watawezeshwa kumiliki ardhi; mafunzo juu kilimo cha biashara; mikopo ya kutunisha mitaji yao. Kutakuwa na dirisha la utoaji mikopo; itaondoa unyanyapaa wa vijana kwa kilimo na vijana watalima, watapata ajira na kutajirika.

Mheshimiwa Spika, ili mradi huu uwe endelevu, napendekeza watakaohusika katika kuwagawia hao vijana na wanawake maeneo, wazingatie kutenga eneo kwa wanawake na vijana wazawa wa maeneo hayo ili kuondoa malalamiko yanayoweza kutoka kwa wenyeji wa hayo maeneo.

Pia napendekeza TAMISEMI iagize Halmashauri zote nchini zibaini na kutenga maeneo ili tuwe na benki ya ardhi ya kutosha, kusudi ifikie wakati mradi huu utakapoweza kuendeshwa katika Halmashauri zote nchini na hivyo wanufaika kuwa wengi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kilimo cha vanila kinawanufaisha watu wengi duniani huko inapolimwa, mkoani Kagera kilimo cha vanila kina zaidi ya miaka 20. Lakini hadi leo hakuna soko la uhakika. Mnunuzi ambaye tena ndiye mwanzilishi wa zao la vanila Kagera, Shirika la Mayawa wana changamoto kubwa. Vanila za wakulima walizonunua tangu mwaka 2021, baadhi ya wakulima hawajalipwa hadi Leo. Mayawa walipata mkopo wa TADB wakalipa baadhi ya wakulima na wengine hawakulipwa. Hivi sasa Meneja wa Mayawa bodi imemsimamisha kazi. Wakulima wanalalamika, wanaumia hawajalipwa sasa mwaka wa pili.

Mheshimiwa Spika, Mayawa wanasema wao vanila walizonunua tangu mwaka 2021 wamekosa mnununuzi na hivyo hawajauza. Hivyo katika msimu wa mwaka 2022 hawakununua vanila na hata katika mwaka wa 2023 hawatanunua vanila.

Mheshimiwa Spika, ili kuwaokoa wakulima naomba Serikali imsaidie Mayawa kutatua changamoto hii, watafutiwe mnunuzi wa vanila kavu. Katika msimu wa mwaka jana alikuwepo mnunuzi mkubwa mmoja anayeitwa NEI. Kwa sababu alikuwa peke yake aliwawekea wakulima masharti magumu ikiwemo wakulima kulazmishwa kuvuna vanila zote kwa mara moja, hata zile ambazo hazijakomaa. Mnunuzi aliwapa muda mfupi wa yeye kununua. Sasa tunaingia katika msimu wa kuvuna mwaka huu, tunaomba Serikali ihamasishe na kuwezesha upatikanaji wa mnunuzi mwingine mkubwa wa vanila.

Mheshimiwa Spika, zao hili kwa sasa linalimwa katika mikoa mingi lakini hakuna miongozo, hakuna huduma za ugani na bei ya miche bado iko juu sana. Je, ni lini Serikali italipatia zao la vanila umuhimu unaostahili na kuweza kuwasaidia wakulima kwa kutoa huduma za ugani na kwa kupitia idara ya masoko Wizarani na TANTRED kuwatafutia soko wakulima hawa?

Mheshimiwa Spika, kuhusu mbolea ya ruzuku; tunaishukuru Serikali kwa kusambaza mbolea katika msimu uliopita. Mkoa wa Kagera ni kati ya mikoa ambayo matumizi ya mbolea bado yako chini sana. Mbolea iliyopelekwa mkoani Kagera kiasi kikubwa ilienda Kagera Sugar kwenye kilimo cha miwa. Mawakala wa usambazaji mbolea ni wachache mkoani kwani wanaogopa wasije wakaleta mbolea, ikakosa mnunuzi.

Naiomba Serikali kwenye maeneo na mikoa mingine kama Kagera ambapo wananchi matumizi yao ya mbolea yako chini, uhamasishaji juu ya matumizi sahihi ya mbolea na Serikali iwasambazie mbolea hadi kwenye vituo mbalimbali mkoani ili wakulima waipate mbolea kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, tunaipongeza Serikali kwa kuwapatia pikipiki Maafisa Ugani wote 342 walio katika mkoa wa Kagera. Hii itawawezesha kufanya kazi zao vizuri. Mkoani Kagera kuna upungufu mkubwa wa Maafisa Ugani, wapo 342 kati ya 732 wanaotakiwa. Tunaomba kupatiwa Maafisa Ugani wa kutosha waweze kusimamia na kutoa huduma za ugani kwa wakulima wa mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.