Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo na mimi niweze kusema mambo machache ya muhimu kuhusu hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kaka yangu Mheshimiwa George Boniface Simbachawene. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameonesha namna gani anataka kuirudisha Tanzania kwenye msimamo hasa wa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu. Kwa sisi Wagogo tuna usemi unasema; mdabula nhili mwana na kalanga ganyina mmeso. Ukitaka kuonja uji wa mtoto, mtazame kwanza mama yake usoni. Ukimwona namna alivyokaa, unaweza ukaamua aidha, uonje au usionje. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Magufuli ameonesha yuko makini na mkali sana kwenye matumizi ya hovyo hovyo. Nataka niseme haya mnayoyaona wengine kushindwa kumwelewa ni kwa sababu Rais Magufuli amewashangaza wengi katika utendaji wake wa kazi. Ndiyo maana mtasikia mengi! Mtasikia Katiba imevunjwa, mtasikia nini! Kwa sababu wengine hawana namna ya kusema, inabidi waseme hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri, tunakufahamu kwa msimamo wako Mheshimiwa Simbachawene. Tuna hakika utaitendea haki kama ambavyo umeonesha tangu mwanzo Wizara hiyo, ni Wizara kubwa, tuna hakika mkijipanga vizuri na Jafo kama mlivyokaa, mna uwezo wa kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele. Tunawapa big up, tunawaomba mwendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme maneno machache hapa. Tunapozungumzia pengine kuna mtu hapa ameshindwa kuelewa anasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali anatafsiri mambo ki-CCM. Ndugu zangu, nchi hii Ilani inayotekelezwa ni ya CCM. Nchi hii hakuna Sera ya Serikali peke yake tu inayojiendesha! Mlikataa wakati wa Bunge la Katiba. Tulipowaambia tuwe na Sera ya Serikali tuachane na Sera za Vyama, mkakataa! Leo tumeenda kuuza sera kwa wananchi; CHADEMA walikwenda nayo, CUF walikwenda nayo na CCM walikwenda nayo. Wananchi wamechagua ya CCM. Sasa mtu anaposema unaongea ki-CCM hata wewe Mbunge unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tuelewane hapo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala tusitake kuzungumza hapa vitu kama vile tunaimbiana mapambio. Upinzani watakuwa wanafanya kazi kama vile ambavyo tunaweza tukasema, wanafanya kazi waki-support kazi ya shetani, kwamba unapinga lakini wenzako wanaotawala wanafanya kazi ya Mungu. Wakati unaeleza upungufu, kwanza unashukuru kwa vichache vilivyotolewa. Hawa kazi yao ni kuponda, halafu baadaye wanaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kazi yetu ni kusifu baadaye tunaomba. Wote kazi yetu ni moja, lakini utajiuliza mwenyewe, je, wa kuponda anafurahisha? Maana kwanza anaponda, halafu baadaye anapiga mzinga. Sisi tunasifu baadaye tunapiga mzinga. Kwa hiyo, tunafanya kazi ya Kimungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namwomba Mungu sana, anipe uwezo watu wanielewe. Sitaki kuingia kule kwenye siasa ambazo watu wamepanga; anasema tu kwa sababu Lusinde tumemwona, yeye anataka kuhamisha vita kutoka kwa Mawaziri kuja kwake; tutampakazia! Wewe useme kwamba Lusinde amepigiwa simu ya Mheshimiwa Rais, kaambiwa asiwatetee. Mimi Wakili? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Wakili, sifanyi kazi ya Mahakama na wala simtetei mtu yeyote katika Mahakama yoyote ya nchi hii. Kwa hiyo, unaweza ukaona; na mimi nataka niwaambieni mkitaka kuleta siasa za uzushi mimi ndiyo natisha kwenye upande huo. (Makofi)
Nirudie tena kuwaonya, mimi mtu kunitaja namruhusu kwasababu hili jina kubwa na nimelitengeneza kwa gharama kubwa. Kwa hiyo, kuna watu watajitahidi kutaka kulifikia jina hili, lakini ni kazi ngumu sana. Waitara nimemfundisha siasa akiwa CCM, leo tena yuko CHADEMA nitaendelea kumsaidia taratibu lakini asifikie huko; Rais ni matawi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, humu ndani tunafanya kazi mbili tofauti. Wako Wabunge ambao kazi yao tangu anasimama mwanzo, ataponda halafu mwishoni anakuja kwenye kiti, nisaidie maji. Yupo Mbunge atasimama, atasifu halafu baadaye atatoa shida zake. Ndiyo tofauti! Ninyi Mawaziri mtapima, yupi anayezungumza vitu vya msingi? Mtapima maana mimi siamini, hata kutafuta mchumba umkute msichana wa watu, umwambie dada una sura mbaya, lakini naomba nikuoe. Akikubali, ujue huyo hana akili. Hana akili huyo! Lazima umsifu kwanza! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaeleza juzi kwa uchungu sana, nikasema nchi yetu tunajenga demokrasia, tuangalie kwa umakini sana. Hii nchi inapita kwenye mawimbi makubwa ya kujengwa demokrasia. Tunapojenga demokrasia, ni lazima hivi vyama tuvipe uhuru mkubwa wa kufanya mambo yao kama ambavyo tunafanya. Ndiyo maana nikawashtua wenzangu, Chama cha CUF, nikawashtua NCCR Mageuzi; siamini kwamba katika ndoa waliyonayo wanajenga demokrasia. Naamini wanakwenda kuuawa! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaweza kumwona Mheshimiwa Zitto hana akili, yuko peke yake, lakini nawaambia katika miaka ijayo, pengine chama chake ndiyo kitakuwa maarufu kuliko vyama vingine hivyo. Maana kinapata muda wa kufanya siasa. Leo kuna watu wanazuiwa na Mwenyekiti, usiseme; wanakaa kimya. Sema, wanasema! Watu wa namna hii ni watu wanaoendeshwa kwa remote, hawawezi kuwa wanasiasa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia Tanzania ina Chama cha Upinzani pengine kimoja tu, ACT, vingine vyote ni vyama shindikizo. Ni Vyama vinavyokwenda na hoja. Meli ikizama, wanahamia kwenye meli; ikitokea kashfa, wanahamia kwenye kashfa. Serikali hii inaziba kila kitu. Wamehamia kwenye tv live. Hebu ngoja nizungumze kidogo hapa! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wasomi mnasema nchi ina Executive, Parliament na Judiciary, hebu tujiulize; mbona Executive mambo yao hayaoneshwi live kila siku? Nayo ndiyo Executive inayoongoza nchi! Mbona hatuoni live kila siku mambo ya Ikulu? Mbona hatuoni Mahakimu wakiendesha kesi live kila siku na wao ni mhimili? Mbona hatuoni Majaji Mahakamani wakiamua mashauri wakiwa live na wao ni mhimili? Iweje watu wang’ang’anie mhimili mmoja? Huku ni kufilisika! Watu wamefilisika, hawana nafasi, wanataka kwenda kujitangaza kwa njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema leo nitoe somo. Katika nchi yenye mfumo wa vyama vingi tuangalie hivi vyama, tuangalie hata aina ya Wabunge. Mimi nawaambia tutakwenda mahali tutajikuta tunatumia resource kubwa, kupoteza muda hapa, hatuisaidii Serikali. Kwa hiyo, naomba niwaambie Waheshimiwa Mawaziri, tunapokuja kuwaambia shida zetu na juzi nilisema, hapa mnatukanwa, mnadharauliwa, halafu wakija wanasema naomba maji. Leo nchi ielewe hakuna Jimbo lolote la mpinzani linalopelekwa maendeleo. Maendeleo katika Majimbo yao tunapeleka sisi CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ndio tunakubali bajeti itekelezwe. Leo tunamwomba Waziri wa maji apeleke maji Moshi, Arusha; Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa huo wanakataa. Mwisho wa siku wanasema tumeleta maendeleo. Unaleta maendeleo kwa kusema hapana? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ifahamu maendeleo yanaletwa na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Aah, niendelee! Niliona Mheshimiwa Mch. Msigwa amesimama nami namheshimu kwa sababu nimeoa kwao. Unajua mimi nimeoa Iringa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu waelewe hata barabara zilizojengwa Iringa Mjini aliposimama Mheshimiwa Msigwa, mimi nilitetea humu ndani ya Bunge. Maana mke wangu anatoka pale.
KUHUSU UTARATIBU.......
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru na nimshukuru hata Mheshimiwa Mch. Msigwa. Mheshimiwa Msigwa na mimi hatujawahi kupingana, sijui leo kimemkuta nini? Mimi juzi nimemwacha ameongea propaganda zake hapa, lakini leo yeye kashindwa kuvumilia. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa George Simbachawene, Mheshimiwa Waziri kupitia Bunge hili, aitazame Halmashauri mpya. Tumezungumza kuhusu mgawanyo wa nchi yetu. Tumeomba Halmashauri mpya ya Mtera, lakini atazame hata jina la Jimbo la Mtera. Kata ya Mtera iko kwako, Kijiji cha Mtera kiko kwako, mimi naitwaje Jimbo la Mtera? Haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikasema Mheshimiwa George hakuna sababu ya Jimbo langu kuitwa Jimbo la Mtera. Unanipa jina la utumwani. Mimi ningependa Jimbo langu liitwe Jimbo la Mvumi ambako anatoka Chifu Mazengo. Kwa hiyo, naomba Halmashauri yetu uitazame, Jimbo letu libadilishwe jina, lisiitwe jina la kijiji kilichoko kwako, kwa sababu sisi hatuwezi kuitika kwako. Watu wengi wanafikiri sisi tuko Mtera; Mtera ni ya George Simbachawene. Sielewi mzee alipoiita, aliita kwa sababu gani.
Mheshimiwa Mweyekiti, naomba kwenye Bunge hili uturudishie majina ya kwetu ya asili. Sisi pale tuna Mvumi karibu ziko 20. Kwa hiyo, ungetuita Jimbo la Mvumi ungekuwa umetutendea haki zaidi kuliko kutuita Jimbo la Mtera ambalo liko kwako wewe Mheshimiwa Simbachawene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaloliomba, kuna barabara za TANROADS na kuna barabara za Halmashauri. Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kujenga barabara ndefu.
Kwa hiyo, naomba kwa niaba ya Wabunge wenzangu, angalia kila Jimbo lenye barabara ndefu, badala ya kuiachia Halmashauri ambayo haina uwezo, zipandishwe hadhi ziende TANROADS ili ziweze kutengenezwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza hivi kwasababu tuna uzoefu; kuna barabara nyingine Halmashauri hazina mapato ya kuweza kutengeneza urefu wa hizo barabara, lakini mkiwapa TANROADS wana uwezo. Kwa mfano, chukulia barabara inayotoka Dodoma Mjini. Kuna barabara inatoka Dodoma Mjini, inapita moja kwa moja kwenye Jimbo la Bahi kwa Mheshimiwa Badwel, inaenda moja kwa moja tena kwenye Jimbo langu la Mtera, halafu ndiyo inaenda kupakana ng’ambo kule kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ile barabara tuipandishe hadhi iwe barabara ya Mkoa kwasababu inapita kwenye Manispaa na kwenye Halmashauri mbili. Ukipata hela Chamwino ukitengeneza kipande, wenzako Bahi wanakosa, panabaki mashimo; kunakuwa hakuna mtengenezaji. Kwa hiyo, naomba kupitia Wizara yako, barabara tulizoziombea zipandishwe hadhi, mzipandishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie, kuna Halmashauri nyingine, kata nne Halmashauri; kata tatu Halmashauri; hebu tuangalie, sisi tuna Jimbo lina kata 22. Tumeomba tugawanywe Wilaya, mkasema hapana tutawapa Halmashauri. Tupeni Halmashauri ili tuweze kusukuma maendeleo mbele. Tunataka kuendelea kufanya kazi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tulisema…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Aaah, naendelea, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. Naona jamaa wanasema umemaliza. Ahsanteni, nimemaliza.