Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameendelea kupambania Taifa hili la Tanzania katika nyanja zote kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee sana napenda kumpongeza Waziri wa Maji pamoja na Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi katika Wizara hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi katika Mji wetu wa Mpanda tuna changamoto kubwa sana ya maji. Ukizingatia Mji wetu wa Mpanda ni mji ambao unakua sana kwa kasi na ongezeko kubwa sana la watu katika Mji wetu wa Mpanda. Katika Mji wetu wa Mpanda na Mkoa wetu wa Katavi, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana wa bandari, lakini changamoto ya maji katika mji huu bado ni kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wananchi wa Katavi tulikuwa tunaomba, tunafahamu kabisa mwarobaini wa kutatua changamoto katika Mji wetu wa Mpanda na Mkoa wetu wa Katavi ni kutoa maji katika Ziwa Tanganyika na kuyaleta katika Mji wetu wa Mpanda na kuhakikisha kwamba yanasambazwa katika Mkoa wetu wa Katavi. Mheshimiwa Waziri anatambua kabisa mradi huu muhimu utaenda kuikomboa mikoa mitatu, ukiwemo Mkoa wetu wa Katavi, Mkoa wetu wa Kigoma pamoja na Mkoa jirani wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka yote tangu tumeingia hapa Bungeni, Mheshimiwa Waziri amekuwa akituchenga sana kuhusiana na mradi huu. Sasa hivi tuko Bungeni tuna karibu takribani miaka mitatu. Tunataka aje atueleze sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi, wananchi wa Mkoa wa Kigoma, na wananchi wa Mkoa wa Rukwa, ni lini mradi utaanza; na ni lini mradi huu utatekelezwa katika Mkoa wetu ili wananchi waweze kuondokana na kadhia kubwa wanayoipta ya kupata maji yasiyo safi na salama?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ni shahidi, amekuwa akifanya ziara katika Mkoa wetu wa Katavi, ameona changamoto ya maji ni kubwa sana, na Serikali imekuwa ikileta pesa nyingi sana katika Mkoa wetu wa Katavi, lakini pesa hizo zimekuwa hazileti matunda kutokana na kwamba miradi mnayoenda kuielekeza ni miradi ambayo haiendi kuwa endelevu katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana 2022 tulimwambia Mheshimiwa Waziri, tulikuwa tunaomba kwamba mradi wa Milala usitekelezwe, na badala yake hii pesa ambayo tunakwenda kuielekeza katika mradi ule, ni kwa nini Serikali isiwekeze kitu ambacho kitakuwa ni uhakika, ambapo ni kutoa maji haya kutoka Ziwa Tanganyika ambapo ni takribani kilometa 100 mpaka mji wetu wa Mpanda? Jambo hilo limekuwa kimya. Sasa Mheshimiwa Waziri ni kijana mwenzangu, tunaheshimiana sana. Tunaomba sisi wananchi wa mikoa hii mitatu aje atueleze, mradi huu utawezekana au hauwezekani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwa imewezekana kutoa maji katika Ziwa Victoria na kuleta katika Mkoa wa Tabora, Mkoa wa Shinyanga na sasa hivi mna mpango wa kuleta katika Mkoa wa Dodoma. Nini kinashindikana katika Mkoa wetu wa Katavi, katika Mkoa wetu wa Kigoma na katika Mkoa wetu wa Rukwa?

Mheshimiwa Waziri hapa ni lazima kije kieleweke, utueleze ni lini mradi huu utaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ni kuhusiana na wakandarasi chechefu. Katika Mkoa wetu wa Katavi kuna Wakandarasi ambao kwa kweli wamekuwa wakiwakwamisha sana wananchi wa Mkoa wa Katavi, hususan mama zangu wa Mkoa wa Katavi. Wakandarasi ambao mnawapa miradi ya maji, wengi wamekuwa hawakamilishi miradi hiyo kwa wakati. Hapa nina mifano ya baadhi ya Wakandarasi ambao kwa kweli wamekuwa wakitukwaza sana wananchi wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, ni mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji maeneo ya Mishamo eneo la Ifumbulwa. Mkandarasi huyu anaitwa HAMWA Construction ana mradi wa thamani ya shilingi milioni 886. Mkandarasi huyu imefikia kipindi mpaka anawatelekeza vijana wale ambao wanafanya vibarua hawalipi, na amekuwa akiwaudhi sana wananchi wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwomba Mheshimiwa Waziri aweze kuzungumza na watendaji wa maji waweze kushughulika na mkandarasi huyu. Mkandarasi mwingine anaitwa HAMATEC mwenye mradi wa zaidi Shilingi milioni 480. Mkandarasi huyu anatekeleza mradi wake katika Kata ya Katuma, Wilaya ya Tanganyika. Naibu Waziri, Mheshimiwa Maryprisca Mahundi ni shahidi, Makamu wa Rais alipofanya ziara katika eneo hili alisisitiza kwamba mkandarasi huyu achukuliwe hatua, na mpaka sasa hivi mkandarasi huyo hamjamchukulia hatua, na wananchi wa kata ya Katuma na Wilaya ya Tanganyika mpaka sasa hivi wanashindwa kupata maji. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri naomba watakapokuja kuhitimisha watueleze nini kinakwamisha kumshughulikia Mkandarasi huyu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkandarasi mwingine, ni yule anayekamilisha mradi wake katika eneo la Milala katika Mji wetu wa Mpanda. Zoezi lile limesimama hamna kinachoendelea pale site. Mheshimiwa Waziri nakujua wewe ni mchapakazi, naomba ushughulike na wakandarasi hawa wanaokuwekea doa. Tunakujua wewe ni mchapakazi mzuri sana, ila ukiwashughulikia wakandarasi hawa, wananchi wa Mkoa wa Katavi tukapata maji. Hakika tutaiona kazi ambayo unaifanya wewe kama kijana, na vijana wote wa Taifa hili ambao tunakuona wewe kama mfano, tutaamini kweli vijana ukiwapa kazi, inafanyika kwa usahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, sisi wananchi wa Katavi hususan ni Jimbo la Kavuu katika Kata ya Majimoto na Kata ya Chamaland. Mji wa Majimoto ni mji ambao unakua sana kutokana na kilimo cha mpunga. Mji huu umekuwa ukiongezeka sana, watu ni wengi wanaoenda kufanya shughuli za kununua mazao katika mji wa maji moto. Mheshimiwa Waziri nakuomba katika Kata hii ya Majimoto, mama zangu wa Mkoa wa Katavi wanaotoka kata hii, tunakuomba uweze kutupatia kisima kimoja kiweze kukaa Kata ya Majimoto na kingine katika Kata ya Chamaland.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante. Ni kengele ya pili.

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Tunampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nashukuru kwa kunipatia nafasi. (Makofi)