Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Bajeti ya Wizara ya Maji jioni hii. Kwanza nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza ndoto yake ya vitendo kwa kumtua mama ndoo kichwani kwa kupitia Serikali yake anayoongoza ya Awamu ya Sita, tumpigie makofi kwa wingi Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niwapongeze Wizara ya Maji, kaka yetu Juma Aweso, lakini pia na Naibu Waziri Mheshimiwa Mahundi, Katibu Mkuu ambaye aliteuliwa hivi karibuni Engineer Kemikimba, Naibu Katibu Mkuu ambaye alikuwa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Luhemeja, lakini pia na wasaidizi wao wote wakiwepo Katibu wa Waziri Ndugu Gibson ambaye anaendelea kutupa sana ushirikiano na pia Mkurugenzi wa Mamlaka Maji, CPA Grace Msiru naye anatupa sana ushirikiano.
Kiukweli niwapongeza kama Wizara wanatupa ushirikiano mkubwa. Wasituchoke waendelee kutuvumilia, sisi siasa zetu zinabebwa na maji. Kwa hiyo, kwa kiwango kikubwa sana Wizara hii tunaitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowapongeza RUWASA Mkoa wa Tabora ambayo iko chini ya Mhandisi Kapufi, lakini pia Mamlaka ya Maja Igunga (IGUWASA) ipo chini ya Mtendaji Mkuu, ambaye tunamwita Murugenzi Mkuu pale Mhandisi Humphrey, lakini pia na Mamlaka ya Maji ya Vijijini Igunga RUWASA iko chini ya Meneja wetu pale anaitwa Mulaza. Wanatupa ushirikiano mkubwa kwa kweli, wanaendelea kutuunga mkono katika utekelezaji wa Ilani yetu kuhakikisha tunapeleka maji vijijini na mijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jioni hii sitakuwa na mambo mengi sana ya kuchangia, lakini nina mambo takribani mawili, moja ni shukrani, lakini pia na mradi mkubwa ambao ningependa kuusemea ambao ningeomba Wizara wausimamie kwa makini kuhakikisha unakamilika. Mwaka jana walitupatia mradi mkubwa sana wa maji kwa kutumia maombi maalum wa kwenda Kijiji fulani kinaitwa Mwamashimba, ni takribani kilometa 45 kutoka Igunga Mjini kule ndio chimbuko langu mimi kama Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunakunywa maji kutoka kwenye kitu tunaita malonga, mnachimba maji, mnatumia ng’ombe na binadamu. Tunashukuru tulileta special request Wizara, walitupatia fedha takribani milioni 800, ule mradi umekamilika na sasa tunapata maji. Tunashukuru sana kwa moyo wao wa upendo waliotujalia Wanaigunga. Pia nishukuru Mamlaka ya Mji Mdogo pale Igunga walitupatia fedha takribani bilioni 1.8 kwa ajili ya mradi wa maji taka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wetu wa Igunga unakuwa sana, ni moja ya miji inayokuwa kwa kasi na ni mji wa kijanja, biashara ni kubwa. Kwa hiyo tumepata mradi wa maji safi na maji taka pale, tunawashukuru Wizara kwa kuliona hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi, nimpongeze Waziri, wamekuwa wasikilizaji wazuri wa maoni ya Wabunge. Mwaka jana moja ya eneo ambalo pia nililichangia sana ni suala la kubadilisha utaratibu wa manunuzi kwa Mamlaka ya Vijijini RUWASA. Nimeona hivi karibuni kuna taarifa ya Waziri inatembea, inasema kwamba wameruhusu manunuzi kwenda mpaka ngazi za mkoa kwa Mamlaka ya Maji RUWASA. Hongera sana kwa Wizara kwa hili wametusaidia, kwa sababu tulikuwa tukikwama, tulikuwa tunatoa mifano kwamba inahitajika hata motor ya milioni tatu, milioni nne, lakini idhini mpaka itoke Wizarani. Sasa wameamua kulishusha mpaka ngazi ya mikoa, naamini litaongeza ufanisi na miradi mingi itakwenda kwa wakati. Hongera sana kwa Wizara waendelee kufanya kazi kwa bidii wamsaidie Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi miwili ambayo tunategemea kwa mwaka huu wa fedha pale Igunga. Kwa Mamlaka ya Maji ya Mjini kwa maana IGUWASA kuna mradi mmoja unahitaji milioni 840. Tunafanya upanuzi wa Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria kutoka sehemu moja inaitwa Makomero kwenda Mgongolo. Kwa hiyo tunapitisha bajeti ya Waziri na naiunga mkono kwa asilimia 100 ili niweze kupata hizi fedha, tukakamilishe huu mradi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa pili pale wa kufanya maboresho. Tuna chanzo kimoja cha Bwawa la Bulenya ambapo tumeomba milioni 521. Naamini pia kwa kuwa naenda kuunga mkono hii bajeti kwa asilimia mia moja, basi na zenyewe tutazipata kupitia Mkurugenzi wa Mamlaka za Maji, Ndugu Joyce ili tuweze kukimbizana tuweze kuendelea kumtua mama ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo ningependa kuchangia jioni hii pale tuna mradi mmoja wa RUWASA ambao ni wa bilioni 20. Kuna kampuni moja inaitwa Help Desk Engineering, naona wapo site na wameshasaini nao mkataba lakini spidi yao sio nzuri sana. Naamini Mheshimiwa Waziri hili watalifanyia kazi, tusirudi kule kwenye ile miradi chechefu ambayo walipambana nayo takribani kwa miaka miwili. Haya makampuni au hawa wakandarasi ndio watamfelisha Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, ajitahidi kuwa makini. Tunapotoa ushauri kwa kuwa anaupokea, mimi ningeshauri kitu kimoja, aweke utaratibu kupitia Kitengo chao cha Monitoring and Evaluation Wizarani. Wanatoa mkataba, mkandarasi akipewa mkataba ndani ya miezi mitatu hajaanza kufanya utekelezaji kwa kiwango wanachoridhika nacho, wavunje mkataba, watoe tenda upya ili tuweze kwenda kwa kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyeyere aliwahi aliwahi kusema; “we must run while others are walking”, kwa lugha nyepesi ya Kiswahili ni kwamba lazima tukimbie wakati wengine wanatembea. Tunaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, siasa yetu inabebwa na maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)