Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia Fungu 49 - Wizara ya Maji ya Ndugu yangu Comrade Aweso. Nisiwe mchoyo wa fadhila ya kuwapongeza sana. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kufanya na ni ukweli Wananchi wa Kibamba wanajua kabisa kazi kubwa ambayo ameifanya Mheshimiwa Rais kwenye Jimbo letu la Kibamba. Ni kwa sababu maelekezo yake pia yanapokelewa vizuri na hawa ndugu zetu ambao wanatafsiri maelekezo, Ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, Waziri na Naibu wake, dada yangu Mheshimiwa Maryprisca Mahundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema, mwishoni kwenye shukrani. Sasa anayo timu nzuri hapo Wizarani, sina shaka kabisa juu ya Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Sadiki Kemikimba na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Cyrpian Luhemeja, kaka yangu anao wasaidizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni shuhuda nimekwenda ofisini kwa Waziri mara nyingi na nyingine ambayo amenikutanisha na menejimenti yake yote juu ya changamoto ya Jimbo za Kibamba, lakini leo nieleze kidogo juu ya mafanikio ya Mheshimiwa Rais katika miaka yake miwili. Naingia hapa Jimbo la Kibamba lina changamoto chini ya asilimia 30 maji wanayapata, kabisa. Wananchi wengi hawana maji, wanapatapata maji pale barabarani, kwenye matanki makubwa Luguruni kwenye mita 20 au 30, lakini leo ninavyozungumza tayari Mheshimiwa Rais alikubali kilio changu humu ndani cha kujenga Tanki la Mshikamano kwa bilioni 5.4, lakini alitumia fedha za UVIKO bilioni 2.5 akazileta. Katika zile bilioni 139, bilioni 2.5 akasema mpeni Kibamba hata tanki lake la Mshikamano liweze kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tanki limeshajengwa limezinduliwa na wananchi wanaendelea kuunganishiwa maji, lakini pongezi nyingine kwa Mheshimiwa Rais, upo mradi wa zaidi ya bilioni 65 kutoka World Bank. Mradi wa chuo kikuu kuelekea Bagamoyo, lakini tumefaidika na tanki la Tegeta A, ujazo wa tanki ile milioni tano, tayari tanki limekamilika. Wananchi wa Goba yote wanaendelea kuunganishiwa maji. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, sana kwa jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambayo mimi na Waziri hata jana nilimwomba niende na akanialika kwenye menejementi yake yote, yote kueleza changamoto mbili ambazo nijue kama amezifanyia kazi au bado. Moja ni wananchi wetu wa Msumi, Kata ya Mbezi, wananchi hawa ni wengi, ndio Jimbo lile lina watu 650,000, jimbo la tano Tanzania nzima kuwa idadi ya watu na wananchi ni wengi kweli, lakin hawana hata chanzo cha maji. Nimshukuru kwa majibu aliyonipa. Tayari wameelekeza fedha katika matanki mawili ya Mshikamano na Tanki la Tegeta A kuunganisha nguvu ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ili watengeneze matanki mawili ya bilioni 13.6. Nawashukuru sana. Najua sasa wananchi wa Mbezi, eneo la Msumi lote linaenda kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho lenye changamoto ni King’azi A, nimezungumza hapa miaka miwili mfululizo kwenye Hansard ipo. Niliwahi kusema viongozi watapigwa mawe humu, lakini leo Waziri amenipa majibu. Katika eneo lile kuna eneo linaitwa Bangalo Kilimahewa, eneo la kwao, watu wa DAWASA, sasa hivi wanaelekeza bilioni 42 pale. Sasa faida yake nini? Mradi mkubwa chini ya Benki ya Dunia, wananchi wa Kibamba, King’azi A na B wanaenda kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna wananchi wa Bangulo, Kinyerezi Jimbo la dada yangu, lakini kuna wananchi wa Kinyerezi, Majohe, Pugu Kipunguni, Ukonga, tunaona mradi mkubwa unaenda kuwasaidia watu wa Dar es Salaam, wananchi wa majimbo matatu. Nimshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Aweso, sina sababu ya kusema mengine, ni kumpongeza kama kijana, anaendelea kuonesha vijana wakipewa nafasi wanavyoweza kufanya kazi. Nampa pongezi sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli katika muda nilionao baada ya hilo, Mheshimiwa Waziri taarifa yake yote kwa nafasi aliyonayo eneo lake ni maji safi na majitaka, lakini eneo hilo la majitaka halizungumzi vizuri sana kwenye taarifa zake kwa nyakati zote. Najua wameelekeza mitambo mizuri ya kubebea uchafu ule katika maeneo machache, lakini nimwambie takwimu zinavyosema kwenye taarifa yake, kwamba mpaka sasa ana kilometa 1,385 kwa mwaka uliopita mpaka sasa hivi 1,416. Huo ndio mtandao wa kilometa za maeneo za maji taka, lakini ameweza kuwaunganishia wateja 53,000… (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Mheshimiwa Saashisha.
TAARIFA
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa kaka yangu taarifa tu kwamba, ni kweli eneo hili la maji taka limesahaulika. Hapo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna eneo wanamwaga majitaka, eneo la Swaswa. Serikali imejenga barabara nzuri mbele na nyuma na majumba yamejengwa mazuri ya ghorofa, lakini yale majitaka usiku yanatoa harufu kali, hawayatibu vizuri. Kwa hiyo, nilikuwa nampa taarifa kwamba ni kweli, watazame na eneo hili. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Mtemvu, unapokea hiyo taarifa?
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuendelea na mchango wangu eneo hili, inawezekana ni gharama sana, sijui lakini niwashauri kwa sasa. Kwa sensa ya mwaka 2020, tumefikia takribani watu milioni sita ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, majumba mengi yamejengwa ya maghorofa Kariakoo na maeneo mengine, lakini ukweli miundombinu ya majitaka haijawekwa vizuri. Sasa niwashauri kwa sababu nyumba nyingi za Kariakoo zinajiunganishia katika mifumo ya maji taka katika mifereji ya majisafi, kwa hiyo ni changamoto, lakini kuna eneo lingine ni mfumo wa majitaka usiotumia chemba, jinsi unavyofanya kazi. Wanaweza kutoa elimu hii kwa watu wengi sasa hivi wanavyojenga, wajenge mifumo ile ya maji taka ambayo haihitaji kutumia chemba inaweza pia ikatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuna jambo hili ni changamoto sana, taka ngumu pia kutupwa kwenye vyanzo vya maji. Dar es Salaam hii hali mbaya na sasa niwaambie kipindupindu kimeanza kuingia, yote hii ni kwa sababu hatujajielekeza vizuri. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri achukuea na wataalam wake, eneo hili la kwake la pili, nashangaa sana hizi Wizara, nitakuja kuchangia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inakaa kwenye ardhi, makazi inaacha. Hili la kwake la maji na mambo ya taka, maji yuko vizuri, taka anaziacha. Ajielekeze huko vizuri, najua ameanza lakini aongeze nguvu, nina imani sana atafanikiwa kama alivyofanikiwa kwenye maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi, naunga mkono bajeti hii ya Wizara ya Maji kwa asilimia zote. Ahsante sana. (Makofi)